KITUO CHA TAALUMA USAFIRI WA ANGA KUBORESHWA
Na Wellu Mtaki, Dodoma
TAKRIBANI shilingi bilioni 49 zimekopwa tutoka benki kuu ya Dunia kwa ajili ya kituo cha umahiri cha mafunzo ya taaluma za usafiri wa anga kwa ajili wa utekelezaji wa miundombinu ya chuo hicho.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa chuo cha taifa cha usafirishaji (NIT) Prof.Zacharia Mganilwa wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya chuo hicho na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2022/23.
Mganilwa amesema kuwa fedha hizo zimegawanyika katika upande wa ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kufundishia wataalam ambapo jumla ya majengo matano yatajengwa Dar- es Salaam kwa gharama ya shilingi bilioni 21 na baadaye kujenga majengo mkoa wa kilimanjaro kwa sababu lazima marubani wafundishwe ndani ya viwanja vya ndege.
Amesema kuwa chuo kimenunua ndege mbili zenye injini moja za mafunzo ambazo ziko njiani zinatazamiwa kuletwa Tanzania kwa gharama ya shilingi dola za Marekani milioni 12 huku akieleza kwamba kumfundisha rubani mmoja nje ya nchi ni shilingi milioni 200 hivyo Serikali inapofanya uwekezaji huu inalifanya shirika la ndege nchini kuleta matumaini ya nchi katika kukuza utalii na uchumi kwa sababu wataalam wa usafiri wa anga watafundishwa hapa hapa nchini.
Aidha amesema kuwa Tanzania ina zaidi ya ndege 400 zilizosajiliwa na mamlaka ya usafiri wa Anga ambapo asilimia 60 ya marubani ni wageni,hivyo ndege hizi zitakapofika vijana wa kitanzania wenye sifa za kusomea urubani watafundishwa na kupata ajira ndani ya nchi.
Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 chuo kinanunua tena ndege yenye injini mbili kwa ajili ya mwanafunzi kukamilisha mafunzo yake kwa sababu mafunzo ya urubani yanamtaka mwanafunzi ajifunze ndege yenye injini moja na injini mbili.
NIT watawawezesha vijana wengi kunufaika na miradi mikubwa inayoendelea nchini mathalani ndege tano zinatarajiwa kuja nchini,ambapo kwa mwaka 2023 ndege nne zitaingia nchini.
No comments:
Post a Comment