VIJANA WAJITOKEZE KUCHANJA COVID-19
VIJANA nchini wametakiwa kujitokeza kupata chanjo ya ugonjwa COVID 19 na waachane na dhana potofu kuwa hawawezi kuambukizwa ugonjwa huo.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mtaalam wa chanjo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Caroline Akim alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na chanjo ya COVID 19.
Akim alisema kuwa moja ya kundi kwenye jamii ambalo halijitokezi kuchanja wakidhani kuwa hawawezi kupatwa na ugonjwa huo hivyo kuwa hatarini kuambukizwa ugonjwa huo.
"Vijana wanadhana kuwa hawawezi kupata ugonjwa huo kwani baadhi hawana dalili ya maambukizi licha ya kuwa wao ndiyo wenye pilika pilika nyingi,"alisema Akim.
Alisema kuwa vijana ni kundi ambalo linahimizwa kupata chanjo kutokana na kuwa na mizunguko mingi kwenye jamii na kuwa rahisi zaidi kueneza ugonjwa huo pale wanapoupata.
"Wajawazito pia wanahimizwa kupata chanjo ya COVID-19 kwani wakipata ugonjwa huu wako kwenye hatari ya mimba kutoka au mtoto kuzaliwa kabla ya wakati na hata wanaonyonyesha wanakumbushwa kuwa chanjo ni salama kwao haina madhara kwa mtoto" alisema.
Aidha alisema kuwa waandishi wanatakiwa sasa kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kuchanja lakini pia faida zake ili kuepuka kuingia kwenye athari wanapopata ugonjwa huo.
Naye Mratibu wa chanjo mkoa wa Pwani Abas Hincha alisema kuwa wanatarajia kuanza kampeni ya chanjo ya COVID-19 inaanza Novemba 25 na watawafikia wananchi ambao bado hawajapata chanjo.
Hincha alisema kuwa Mkoa huo unatarajia hadi kufikia Desemba 30 kuwafikia wananchi 757,465 na kwamba hadi kufikia Novemba 22 walengwa 468,187 tayari wamepata chanjo sawa na asilimia 63.
No comments:
Post a Comment