BARAZA LA MADIWANI LATOA ADHABU KWA MTUMISHI WA HALMASHAURI KUKATWA MSHAHARA.
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha limemchukulia hatua Mhandisi wake Brighton Kishoa kwa kumkata asilimia 15 ya mshahara kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya kushindwa kusimamia mradi wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi.
Akitoa maazimio ya kikao hicho cha baraza la madiwani cha robo mwaka Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Musa Ndomba alisema kuwa mtumishi huyo alisababisha mradi huo kuwa na gharama kubwa.
Ndomba alisema kuwa moja ajenda iliyojadiliwa na baraza hilo ni makosa ya kinidhamu ya kiutumishi yaliyofanywa na Mhandisi huyo wa Halmashauri hiyo ambaye hakufuata utaratibu wa manunuzi (BOQ) ya ujenzi wa nyumba hiyo.
"Kutokana na kutofuata taratibu za manunuzi kulitokea changamoto kwenye ununuzi wa vifaa kwani haukufuata bajeti iliyopangwa hivyo gharama za ujenzi kuwa kubwa,"alisema Ndomba.
Alisema baada ya changamoto hiyo kutokea ilibainika kuwa katika usimamizi wa miradi ilionekana kuna maeneo kafanya uzembe hivyo baraza la madiwani na kamati ya fedha ziliamua kumchukulia hatua za kinidhamu.
"Taratibu zote zimefuatwa kwa kamati za uchunguzi na kufanya kazi yake na zikapendekeza adhabu hiyo na hilo litakuwa fundisho kwa watumishi wengine kwa kutakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazowaongoza," alisema Ndomba.
Aidha alisema kuwa anawakata watumishi wote kuanzia Halmashauri hadi kwenye Mtaa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na wasipingane na miongozo ya kazi zao kwani miradi ya maendeleo itakuwa haina tija na kurudisha nyuma utoaji huduma kwa wananchi.
"Sisi kama baraza hatutarudi nyuma kwani tutachukua hatua kali kadiri inavyowezekana kwa mtumishi yoyote atakayeonyesha utovu wa nidhamu katika utendaji kazi wake na tutatoa adhabu kali zaidi kwa mtumishi atakayekwenda kinyume na taratibu za kazi yake na kuzorotesha utoaji huduma kwa makusudi,"alisema Ndomba.
Alibainisha kuwa hawapendi kutumia muda mwingi kujadili mtu bali wanapenda muda mwingi wautumie kujadili masuala ya kuwaletea maendeleo wananchi.
No comments:
Post a Comment