BODI YA WAHANDISI YASEMA MIRADI YA KIMKAKATI IMEWAONGEZEA UJUZI
Na Wellu Mtaki, Dodoma
BODI ya Wahandisi Nchini (ERB) imesema kuwa uwepo wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa hapa nchini imekuwa na manufaa kwa Wahandisi wazawa hasa vijana kupata ujuzi na teknolojia mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma wakati akielezea shughuli mbalimbali za Bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wake kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Msajili wa Bodi hiyo Mhandisi Bernard Kavishe amesema kuwa miradi hiyo imekuja na teknojia mpya kabisa.
Mhandisi Kavishe amesema kuwa kwa sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya Wahandisi 33,773 kati yao 26,000 wapo katika soko la ajiri huku wenye leseni za Uhandisi wakiwa ni 10,000 na wengi wao wanashiriki kwa namna moja au nyingine katika utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa inayoendelea.
Amesema kuwa malengo ya Bodi hiyo ni kuongeza ushiriki wa bidhaa za ndani (Local content) katika miradi yote inayoendelea hapa nchini ambapo matarajio makubwa ya Bodi hiyo ni kujenga kituo Cha Umahiri Jijini Dodoma.
Aidha amesema kuwa kutokana na kuwepo kwa Vijana wengi wenye mawazo ya kibunifu ila wanakosa namna ya kuendeleza mpaka kufika sokoni hivyo kituo hicho kitakuwa eneo sahihi la kuendeleza mawazo hayo.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa amesema kuwa kwa sasa nchi ina miradi mingi hivyo Bodi ya Wahandisi ina nafasi kubwa katika kutoa ushauri wa namna nzuri ya kutekeleza miradi hiyo kwa uhakika.
No comments:
Post a Comment