IMEELEZWA kuwa uanzishwaji wa madawati kwenye shule na makundi mbalimbali ya jamii kutasaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa matukio yanayohusiana na vitendo hivyo.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mwanasheria wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) Tanzania Zakia Msangi wakati wa kupita msafara unaotoa elimu ya kupambana ukatili wa Kijinsia ikiwa ni sehemu ya siku 16 za kupinga vitendo hivyo.
Alisema kuwa moja ya makundi yanayoathirika na vitendo hivyo ni watoto ambapo madawati hayo yataundwa kwa kushirikiana na walimu wa malezi kwenye shule.
"Madawati haya yatakuwa yakitoa elimu juu ya kupambana na ukatili wa Kijinsia na kuripoti vitendo hivyo kwenye vyombo husika ikiwemo dawati la jinsia na vyombo vingine vya sheria,"alisema Msangi.
Msangi alisema kwa shule kutakuwa na wanafunzi wawili vinara ambao watakuwa na ujasiri wa kujieleza na wenye usiri pia kutakuwa na sanduku la siri la kutolea maoni.
"Makundi mengine ndani ya jamii kama vile waendesha pikipiki nao wataunda madawati kwa ajili ya kupambana na matukio hayo ambapo itasaidia kukabili kwani ni kundi linalokumbana na mambo mengi,"alisema Msangi.
Aidha alisema kuwa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) Tanzania ni waratibu wa kampeni hiyo ambapo wameungana na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) ambao ndani yake kuna mashirika zaidi ya 100 kupambana na suala hilo.
Kwa upande wake ofisa Mawasiliano wa Shirika linalosaidia mashirika yanayotoa msaada wa sheria (LSF) Wilson Mtapa alisema kuwa wamewezesha msafara huo ili kupinga vitendo hivyo kwa kutoa elimu ya kupinga vitendo hivyo kwa kushirikiana na serikali na wadau wa maendeleo.
Mtapa alisema kuwa elimu hiyo inatolewa kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwa ni pamoja na mashuleni madokoni na kwa vikundi vya waendesha bodaboda kwenye Wilaya msafara huo utakapopita kauli mbiu ikiwa ni Kila uhai unathamani tokomeza mauaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Alisema kuwa mashirika hayo mbali ya kupambana na vitendo hivyo pia yanatetea haki za binadamu ambapo wanatoa elimu ya namna ya kukabiliana na vitendo hivyo ndani ya jamii na msafara huo ulioanzia Dar es Salaam Pwani utapita mikoa ya Morogoro, Singida, Shinyanga, Arusha na Musoma.
Naye mwakilishi wa Shirika la Maendeleo kwa Vijana YPC ambalo liko chini ya MKUKI ambao ndiyo walikuwa wenyeji wa msafara huo Fred Mtei alisema kuwa ujumbe uliotolewa wa kukabiliana na vitendo vya ukatili umewafikia watu wengi.
Mtei alisema kuwa wao kama wana harakati wataendelea kutoa elimu na kuielimisha jamii namna ya kukabiliana na vitendo hivyo.
Mkurugenzi wa Kituo Cha Msaada wa Kisheria Kibaha (KPC) Catherine Mlenga alisema kuwa wamekuwa wakipokea wateja ambao wengi wao ni wa vitendo vya ukatili wa Kijinsia.
Mlenga alisema kuwa wamekuwa wakishirikiana na vyombo vya sheria ikiwemo Polisi na mahakama kupambana na vitendo hivyo kwenye Wilaya na Mkoa mzima wa Pwani na wanatoa elimu kwenye maeneo mbalimbali na makundi ya kijamii.
Kwa upande wake Mratibu wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania kwa Mkoa wa Pwani Honorina Kambadu alisema kuwa wanazingatia haki na usawa mbele ya sheria na kukabili matukio ya ukatili wa Kijinsia.
Kambadu alisema kuwa baadhi ya matukio ni kama vile vipigo, unynyasaji na mauaji na kunyimwa haki zingine kwa wanawake na watoto ambao ndiyo waathirika wakuu wa vitendo hivyo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment