Sunday, March 10, 2013
STORY ZA PWANI
Na John Gagarini
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu
Mahiza amesema kuwa serikali haitakaa kimya kuona baadhi ya kinamama wakifanya
vitendo vya kinyama ikiwa ni pamoja na kutupa watoto wanaowazaa.
Mahiza aliyasema hayo wakati wa hafla fupi ya kusherehekea
siku ya Wanawake Duniani kwenye Halmashauri ya Mji wa Kibaha na kusema kuwa
baadhi wanawake wamekuwa wakiwafanyia ukatili hata watoto wao wa kuwazaa.
Alisema kuwa moja ya ukatili ambao umekithiri mkoani Pwani ni
kuwatupa watoto jambo ambalo limekuwa likishika kasi siku hadi siku kwenye mkoa
huo.
“Serikali haitaweza kuvumilia kuona baadhi ya akinamama
wakitenda vitendo vya ukatili kwa watoto wao kwani nao wana haki ya kulelewa na
wana haki ya kupata matunzo pamoja na kuishi hivyo ni vema kila mtu akatimiza
wajibu wake kwani hiyo ni haki ya msingi ya mtoto,” alisema Mahiza.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa haipendezi kuona wanawake
wanakuwa mstari wa mbele kufanya vitendo vya ukatili kwa watoto wao.
“Kama unaona bado hujajianda kulea kwanini uzae kama wewe
ungefanyiwa hivyo sasa hivi ungekuwa wapi na mtu wa aina gani ni lazima
mjilinde na kuachana na vietendo hivyo kwani ni ukatili ambao hutaweza
kuvumiliwa na serikali na hatua kali zitachukuliwa kwa wanaofanya vitendo hivyo,”
alisema Mahiza.
Aidha alisema vitendo hivyo ni vibaya kwani mbali ya kuwaua
watoto pia ni kuwafanya wawe watoto wa mitaani na kuathirika kisaikolojia na kuwajengea mazingira mabaya ya kuishi.
Kwa upande wake mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina
Koka alisema kuwa aliamua kuwakusanya wanawake kwa pamoja ili kubadilishana
mawazo na kutafakari siku hiyo katika kutimiza majukumu yao kama mama.
Koka alisema kuwa siku hiyo ina maana kubwa kwa akinamama
katika kuihudumia jamii na Taifa ambalo linawategemea katika kujenga uchumi wa
nchi.
Mwisho.
WAANDISHI wa Habari wa Kanda ya Mashariki wametakiwa kutoa
elimu ya kutosha kwa Jamii inayowazunguka ili kuondokana na dhana juu ya chanjo
mbalimbali zinazotolewa na serikali kwa watoto kuwakinga na magonjwa
yanayosababisha vifo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na kaimu katibu Tawala mkoa wa
Pwani Injinia Michael Mrema wakati akifungua mafunzo ya siku moja juu ya chanjo
mpya ya magonjwa ya Nimonia na Uti wa Mgongo ya Rotavirus kwa waandishi wa
Kanda ya Mashariki.
Injinia mrema alisema kuwa jamii imekuwa na dhana mbaya kuwa
baadhi ya chanjo zina athari kwa watoto hivyo kushindwa kuwapeleka kupata
chanjo.
“Waandishi ni watu wanaoaminiwa na jamii hivyo kwa kutumia
kalamu zenu mnaweza kutoa elimu juu ya umuhimu wa chanjo hizo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambao
wanakufa kutokana na maambukizi ya magonjwa mbalimbali,” alisema Injinia Mrema.
Alisema kuwa magonjwa kama hayo husababisha vifo kwa asilimia
80 hivyo lazima itumike nguvu ya ziada ya kutoa elimu ili jamii ione umuhimu wa
kuwapeleka watoto wao kupata chanjo kwa lengo la kupunguza vifo hivyo visivyo
vya lazima.
“Chanjo hii mpya inatoa kinga kwa asilimia 87 hadi 88 ambapo
nchi imejitahidi sana kwani imeweza kupunguza vifo toka 99 hadi 51 kwa watoto
1,000 kwa mwaka 2010,” alisema Injinia Mrema.
Aidha alisema kuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara
yoyote na endapo jamii itapata taarifa sahihi hawataweza kupotoshwa na
watawapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo ambayo ni bure na haina gharama
zozote.
Kwa upande wake ofisa habari idara ya habari maelezo Veronica
Kazimoto alisema kuwa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yatasaidia kufikisha
ujumbe sahihi na haraka kwa walengwa hivyo wanaamini kuwa waandishi ni njia
sahihi ya kutoa elimu. Mafunzo hayo ya siku moja waliwahusisha waandishi toka
mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.
Mwisho.
WAKAZI wa Mji wa Kibaha waliojenga vibanda na nyumba kwenye
maeneo ya barabara wametakiwa kuvunja mara moja kabla serikali haijavunja ili
kupisha matengenezo ya barabara za kuingia kwenye mitaa ya mji huo.
Hayo yalisema na Injinia wa Halmashauri ya Mji huo Ezekiel
Kunyaranyara alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa tayari
watendaji kwenye mitaa hiyo walishapewa barua ya kuwajulisha walengwa.
Kunyaranyara alisema kuwa baadhi ya watu wamejenga vibanda
vya biashara na nyumba kwenye eneo la barabara za mitaani na kufanya barabara
hizo kushindwa kupitika hasa pale yanapotokea madhara mbalimbali yakiwemo ya
moto.
“Athari za watu kujenga kwenye maeneo zinakopita barabara ni
nyingi lakini mojawapo ni magari kushindwa kupita hata pale kunapotokea mfano
mgonjwa anatakiwa kuchukuliwa na gari na kupelekwa hospitali au moto unapotokea
gari la zimamoto linashindwa kupita hivyo kuleta athari kubwa,” alisema
Kunyaranyara.
Alisema walitoa maelekezo kwa watendaji wa mitaa yote kwenye
maeneo husika na walitoa miezi sita tangu mwaka jana hadi Machi mwaka huu
ambapo endapo hawatafanya hivyo wakati wowote watatekeleza kazi hiyo.
“Katika awamu hii tulitenga kiasi cha shilingi milioni 9 kwa
ajili ya kuchonga barabara zote za Mji wa Kibaha kwani lengo ni kuhakikisha mji
unakuwa na barabara ambazo zinapitika kwa mkipindi chote cha mwaka,” alisema
Injinia Kunyaranyara.
Alisema kuwa hivi karibuni halmashauri ilinunua greda lake
hivyo kuanza kukarabati barabara zote kwenye kata zote za halmashauri hiyo 11
zenye mitaa 53.
KUFUATIA kilio cha mkuu wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza
kuiomba ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
kuisaidia kupata fedha kiasi cha shilingi miloni 160 kwa ajili ya kukarabati
mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Tumbi hatimaye kilio hicho kimesikika ambapo
ofisi hiyo imeahidi kutoa fedha hizo.
Akizungumza juzi mara baada ya kutembelea Shirika la Elimu
Kibaha (KEC) lililopo wilayani Kibaha mbele ya viongozi wa shirika hilo ambalo
linamiliki hospitali hiyo, Kaimu katibu mkuu TAMISEMI Alafayo Kidata alisema
watatoa fedha hizo ili kufanya ukarabati wa chumba hicho.
Kidata alisema kuwa chumba hicho ni muhimu hivyo Wizara
imeona kuna umuhimu wa kutoa fedha hizo ili kufanya ukarabati kwani haipendezi
kuona chumba hicho kikiwa kwenye hali mbaya ambapo marehemu wanahifadhiwa humo.
“CHumba cha maiti ni muhimu sana na kila mtu atapitia hapo
hivyo kiubinadamu lazima mazingirra yake lazima yawe mazuri kutokana na maombi
toka kwa viongozi wa shirika tumeona mahali hapa panahitaji kuangaliwa mapema
huku sehemu nyingine zikifanyiwa kazi,” alisema Kidata.
Aidha alisema kuwa kutokana na umuhimu wa hospitali hiyo
kupokea majeruhi wengi wa ajali pamoja na maiti zinazopokelewa hapo ni vema
ukarabati ukafanyika ili kuondoa hali mbaya iliyopo.
“Tunatarajia mwishoni mwa mwezi huu fedha zitatolewa ili
kuboresha chumba hicho ambacho kwa sasa ni kidogo na kinapokea marehemu wengi,”
alisema Kidata.
Alibainisha kuwa madeni mbalimbali ambayo yanafikia kiasic ha
shilingi bilioni moja watahakikisha yanalipwa hadi ili huduma ziendelee
kutolewa kwani kuna hatari ya baadhi ya watoa huduma kusitisha.
Awali akitoa taarifa ya shirika kwa kaimu katibu mkuu,
mkurugenzi wa KEC Dkt Cyprian Mpemba alisema kuwa chumba cha maiti kwa sasa
kinahifadhi miili miwili miwili kutokana na udogo wake jambo ambalo si zuri.
Dkt Mpemba alisema kuwa chumba hicho hakijafanyiwa
matengenezo tangu hospitali hiyo ilipoanzishwa miaka ya 70 na wafadhili wa nchi
za Nordic, pia linakabiliwa na madeni makubwa yanayofikia zaidi ya bilioni
moja.
Mwisho.
Thursday, March 7, 2013
RC AOMBA MSAADA CHUMBA MAITI
Na John Gagarini, Kibaha
MKUU wa mkoa wa Pwani Mwantumu Mahizaameiomba ofisi ya Waziri
Mkuu (TAMISEMI) kuipatia hospitali ya wilaya ya Tumbi kiasi cha shilingi
milioni 160 kwa ajili ya kukarabati chumba cha kuhifadhia maiti ambacho kiko
kwenye hali mbaya.
Aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa ziara ya siku moja ya
Waziri wa TAMISEMI Hawa Ghasia alipotembelea Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ambalo
linamiliki hospitali hiyo ambalo liko chini ya Wizara hiyo.
Mahiza alisema kuwa chumba hicho kiko kwenye hali mbaya kwani
kimekuwa ni kidogo na kimechakaa na hakijafanyiwa ukarabati tangu kuanzishwa
miaka ya 70.
“Waziri tunaomba utusaidie kuweza kupata fedha hizo kwani
licha ya kuwa na madeni makubwa na mahitaji ya fedha, kikubwa ni chumba hichi
ambacho kinahitaji kufanyiwa ukarabati kwani kiko kwenye hali mbaya na kinahitaji
msaada wa haraka,” alisema Mahiza.
Alisema maiti zinahitaji kuhifadhiwa katika mazingira mazuru
ili kuzienzi lakini kwa hospitali yetu hali si nzuri kwani tutakuwa
hatuzitendei haki kwa kuzitunza kwenye mazingira mabaya.
Kwa upande wake mganga mkuu wa hospitali Peter Datan alisema
kuwa tatizo la chumba hicho ni kubwa kwani kwa sasa maiti zinakaa mbili mbili
ambapo kwa utaratibu wanapaswa kukaa mwili mmoja kutokana na udogo wake.
“Kwa sasa chumba kimekuwa ni kidogo kwani maiti zimeongezeka
tofauti na zamani ambapo zilikuwa chache kwani kwa sasa maiti zinazohifadhiwa
ni 20, pia maiti nyingine zinakaa muda mrefu hasa zile ambazo zinakuwa
zimeokotwa,” alisema Dkt Datan.
Dkt Datan alisema kuwa chumba hicho kinapata mzigo mkubwa wa
maiti kutokana na baadhi ya maeneo ya mikoa kama vile Dar es Salaam, Morogoro
na Tanga kuletwa TUmbi.
Naye Mkurugenzi wa KEC Dkt Cyprian Mpemba alisema kuwa
wanakabiliwa na madeni makubwa ambayo kwa sasa yanafikia zaidi ya bilioni moja
hali ambayo ni madai ya wafanyakazi na wazabuni ambao wanatoa huduma kwao.
Kwa upande wake waziri Ghasia alisema kuwa atayafanyia kazi
maombi hayo kwa kupeleka ombi maalumu hazina ili kuweza kutatua chanagamoto
zilizopo kwenye shirika hilo la Umma ambalo lilianzishwa miaka ya 70 na nchi za
Nordic kwa ushirikiano na serikali.
Mwisho.
WAWILI WAFA
Na Mwandishi Wetu, Kibaha
MLINZI
wa kampuni ya ulinzi ya S&M ambaye alikuwa akilinda ofisi ya DAWSCO
wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Juma Hassan (45) ameuwawa na watu wanaodhaniwa
kuwa majambazi baada ya kuvamia ofisi hiyo.
Kamanda
wa Polisi mkoani Pwani Ulrich Matei alisema kuwa watu hao ambao idadi yao
haikuweza kufahamika mara moja walimteka kasha kumtupa baada ya kumfunga kamba
miguuni na mikononi pia walimziba na plasta mdomoni na puani.
Alisema
kuwa baada ya kumteka waliingia kwenye ofisi hiyo na kuiba kompyuta nne ambazo
thamani yake haikuweza kufahamika mara moja kasha kutoweka.
“Tunaendelea
na upeelelezi kujua ni watu gani waliofanya tukio hilo la kusikitisha na
tunawaomba wananchi kutoa taarifa endapo watasikia juu ya watu walio husika na
tukio hilo.
Alisema
kwenye tukio linguine makazi wa Mkoani Kibaha Amani Aidan au Mgaya (24) amepoteza
maisha baada ya pikipiki aliyokuwa amepanda kugongana na gari.
Kamanda
Matei alisema tukio hilo lilitokea Machi 5 saa 1 usiku eneo la TAMCO barabara
ya Dar es Salaam – Morogoro ambapo pikipiki hiyo ili gongana na gari namba T
787 AWC aina ya Toyota Coaster lililokuwa likiendeshwa na Thadei Makala (58).
Aidha
alisema katika ajali hiyo mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Amina (22)
mkazi wa Picha ya Ndege Kibaha alikimbizwa hospitali ya Tumbi kwa matibabu
zaidi baada ya kupata majeruha sehemu za kichwani kulia.
Mwisho.
Na
Mwandishi Wetu, Kibaha
JESHI
la Polisi mkoani Pwani linamtafuta Ramadhan Mfaume maarufu kama Ngosha kwa
tuhuma za kukutwa na silaha aina ya Short Gun na fuvu la mnayama aina ya Fungo
na Ngiri.
Akizungmza
na waandishi wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani hapo Ulrich Matei
alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 4 mwaka huu.
Kamanda Matei alisema kuwa vitu hivyo
vilikamatwa nyumbani kwake kwenye eneo la Fitina haina Posho Kijiji cha Mwavi
kata ya Fukayosi wilaya ya Bagamoyo.
Aidha
alisema kuwa mbali ya silaha hiyo ambayo namba zake hazikuweza kufahamika mara
moja pia kulikutwa risasi 29.
Alisema
mtuhumiwa huyo alitoroka na anatafutwa kuhusiana na tukio hilo na kuwataka
wananchi kutomiliki silaha hizo bila ya kibali ili kuepukana na mkono wa sheria.
Mwisho.
Tuesday, March 5, 2013
MADENI MAKUBWA SHIRIKA
WAAFANYAKAZI na Wazabuni mbalimbali wa Shirika la Elimu
Kibaha (KEC) mkoani Pwani wanalidai shirika hilo kiasi cha zaidi ya shilingi
biloni moja.
Hayo yalisemwa juzi na mkurugenzi wa shirika hilo Dkt Cyprian
Mpemba, wakati wa ziara ya siku moja ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia.
Dkt Mpemba alisema kuwa madeni hayo ni ya wazabuni wanaodai
kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 286, wafanyakazi wanaodai zaidi ya shilingi
milioni 277 na makandarasi mshauri wa hospitali ya Tumbi anayedai kiasi cha
zaidi ya shilingi milioni 600.
“Madeni hayo ni changamoto kwetu kwani ruzuku inayotolewa na
serikali haitoshelezi kabisa ambapo kwa bajeti ya mwaka 2010/2011 fedha
zilizotolewa na serikali zilikuwa ni pungufu kwa asilimia 15 huku bajeti ya
mwaka 2011/2012 ilikuwa pungufu kwa asilimia 48,” alisema Dkt Mpemba.
Alisema mbali ya madeni hayo pia shirika lina mahitaji
makubwa ambapo wanahitaji kiasi cha shilingi bilioni 11 kwa ajili ya kumalizia jengo
la hospitali, zaidi ya bilioni moja, milioni 500 kwa ajili ya mafunzo kwa
madaktari bingwa na wasaidizi, uchakavu wa majengo kiasi cha shilingi milioni
300, matengenezo ya magari na majengo zaidi ya milioni 131, maji, umeme, bima,
madawa na shajala shilingi zaidi ya milioni 143, chumba cha kuhifadhia maiti
shilingi milioni 160 kwa ajili ya ukarabati.
“Kutokana na changamoto ya fedha ripoti ya mkaguzi mkuu wa
serikali ya mwaka huu imetahadharisha kuwa shirika lipo kwenye hatari ya
kushindwa kabisa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwani inaonekana mahesabu
ya shirika yana mwelekeo mkubwa wa uhaba wa kumudu kulipa watoa huduma wastani
wa bilioni moja,” alisema Dkt Mpemba
Aidha alisema wastani wa mapato ya ndani ya shirika hilo ni
kati ya shilingi milioni 800 na bilioni moja kwa mwaka ambazo hazikidhi
matumizi stahiki kwa idadi ya watumishi waliopo 985 hivyo kuiomba serikali
kuongeza ruzuku ya mwaka kutoka bilioni 1.9 na kufikia bilioni 3.6.
Akijibu hoja hizo Waziri Ghasia alisema kuwa kuhusu madeni
watalifanyia kazi suala hilo ili kuweza kupunguza chanagamoto ya ukosefu wa
fedha kwenye shirika hilo la Umma ambalo limekuwa na mchango mkubwa ambayo ni
kutoa huduma za kielimu, afya na kupambana na umaskini.
‘Pia ifike wakati
mwende kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya kukopa kuliko kutegemea ruzuku ya
serikali ambapo kwa bajeti iliyopita hali ya kifedha haikuwa nzuri, kwani
mashirika ya umma yanatakiwa yajiendeshe yenyewe na si kuisubiri serikali pekee,”
alisema Ghasia.
Alisema KEC ina vyanzo vingi vya mapato ikiwemo ufugaji kuku
na ng’ombe endapo vitapatiwa fedha litaweza kujiendesha kwa kiasi fulani hivyo
kumudu kufanya shughuli zake za kila siku, awali Waziri alitembelea mashamba ya
kuku, kiwanda cha kutengenezea trei za mayai na hospitali ya Tumbi akiwa na
uongozi wa shirika na bodi.
Mwisho.
Subscribe to:
Posts (Atom)