Wednesday, April 19, 2023

WAZIRI JAFO AUPONGEZA MKOA WA PWANI KWA KAMPENI YA UPANDAJI MITI



WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Suleiman Jafo ameupongeza Mkoa wa Pwani kwa kuweka kampeni ya upandaji miti ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Jafo aliyasema hayo kwenye shule ya sekondari Ruvu Mlandizi Wilayani Kibaha wakati akizundua Kampeni ya utunzaji mazingira na matumizi ya nishati mbadala kwa mkoa huo iliyoandaliwa na benki ya NMB Wakala wa Misitu Tanzania TFS Mkoa wa Pwani, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na Taifa Gesi.

Alisema kuwa kwa kampeni hiyo kwani itasaidia kutunza mazingira pia utasaidia kutangaza teknolojia mbadala ya matumizi ya nishati mbadala baada ya kupunguza matumizi ya miti kama nishati kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine ya binadamu ya kila siku.

Aidha alisema kuwa mkoa wa Pwani ni moja ya mikoa minne ambayo imeathirika kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira lakini baada ya kupata maelekezo kutoka kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kutaka mikoa hiyo iweke mipango ya kukabili hali hiyo mkoa umejiongeza kwa kuwa na kampeni hizo za kukabili changamoto za mazingira.

Awali akimkaribisha Waziri Jafo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani  Abubakar Kunenge Mkuu wa wilaya ya Kibaha Nickson John alisema kuwa mkoa umeweka mikakati mbalimbali ili kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti million 13.5 lakini hadi sasa wameshapanda miti milioni 9.7 ikiwa ni zaidi ya asilimia 70 ya malengo ili kurejesha uoto wa asili.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Taifa gesi Anjela Bhoke alisema kuwa kila mwaka hekari 400,000 za miti zinapotea kutokana na matumizi mbalimbali ya miti ambapo moja ya mikakati yao ni kujenga kiwanda cha kutengeneza mitungi ya gesi ambapo wako tayari kusambaza gesi majumbani na kwenye taasisi za umma.

Mwakilishi wa benki ya NMB Seka Urio alisema kuwa wametenga kiasi cha shilingi milioni 470 kwa ajili ya shule zitakazopanda miti 2,000 na kuitunza kwa asilimia 80 ambapo itapatiwa milioni 50, huku mshindi wa pilia kwa kupanda miti 1,500 akipata milioni 30 akiitunza kwa asilimia 70 na watatu akipata milioni 20 kwa kupanda miti 1,000 itakayokuwa imetunzwa kwa asilimia 70.


No comments:

Post a Comment