Wednesday, April 26, 2023

MILIONI 2.9 HUPOTEZA MAISHA



TAKWIMU za kidunia zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani mwaka 2022 zinaonesha kwamba zaidi ya watu milioni 2.9 hupoteza maisha kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Aidha zaidi ya wafanyakazi milioni 402 huumia wakiwa kazini na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kipindi chote wanachopatiwa matibabu hadi hapo watakapopona.

Akizungumza  na Waandishi wa habari Tarehe 26 April 2023 Jijini Dodoma kuelekea maadhimisho ya siku kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana,Ajira, na Wenye Ulemavu Prof Joyce Ndalichako amesema Kwa upande wa Tanzania jumla ya ajali na magonjwa yaliyoripotiwa katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuanzia Julai 2019 hadi Juni 2021 ni ajali 4,993 na magonjwa 249. Katika ajali hizo vifo vilikuwa 217.

Prof Ndalichako amesema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa Mkoani Morogoro katika viwanja vya Tumbaku Aprili 28,2023 na lengo kubwa la maadhimisho hayo ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha na kuweka mazingira salama katika sehemu za kazi miongoni mwa wadau kupitia kauli mbiu mbali mbali ambazo hutolewa na Shirika la Kazi Duniani ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Mazingira Salama na Afya kazini ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahali pa Kazi” (A Safe and Health Working Environment is a Fundamental Principle and Right at Work).

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda amesema kuwa moja kati ya eneo ambalo ajali nyingi zinaripotiwa ni katika sekta ya Uzalishaji ambapo imeajiri vijana wengi huku wengine wakiwa hawana ujuzi wa kutosha katika nafasi wanazofanyia kazi.

Mwenda amesema kuwa OSHA imejipanga vyema kuelekea maadhimisho hayo ya 19 ambapo washiriki wote watapatiwa Mafunzo ya Usalama na Afya miongoni mwa makundi mbali mbali wakiwemo wajasiriamali wadogo, wafanyakazi wa viwandani, wachimbaji wadogo pamoja na watu wenye ulemavu.

Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani ilianza mwaka1996 Nchini Marekekani Katika Jiji la New York, ambapo waathirika wa watu walioumia na kupoteza maisha wakiwa kazini hukumbukwa. Maadhimisho hayo yalikuwa yakifanywa na Chama Cha Wafanyakazi Duniani. Ilipofika mwaka 2001,Shirika la Kazi Duniani liliona kuwa ni busara kubadilisha madhumuni ya siku hiyo na kuiita “Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani


Mwisho.

No comments:

Post a Comment