Na Wellu Mtaki, Dodoma
SERIKALI ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada kubwa katika kufanya mabadiliko na maboresho makubwa katika Sekta ya Maji ikiwa pamoja na kuongeza uwekezaji katika sekta hiyo ili kukabiliana na changamoto zilizoko.
Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Sinyamule wakati wa ufunguzi wa tafiti juu ya maombi ya kurekebisha bei za huduma ya maji safi iliyoletwa na mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Dodoma ( DUWASA)
Sinyamule amesema kuwa lengo kubwa la Serikali katika kufanya mabadiliko na kuongeza uwekezaji katika sekta ya Maji ni kuongeza ubora na upatikanaji wa huduma ili kuboresha maisha ya Wananchi wake na hatimaye kufikia lengo la asilimia 95 (kwa mijini) lililowekwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ifikapo mwaka 2025.
Awali mwakilishi wa Mkurugezi mkuu wa Ewura George Kabelwa katika maombi hayo Mamlaka ya Maji Dodoma imeomba kufanya marekebisho ya bei zitakazotumika kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2023/24 hadi 2025/26 kwa mujibu wa maombi yaliyowasilishwa EWURA, Mamlaka ya Maji Dodoma imebainisha kuwa marekebisho ya bei ya maji yanalenga kupata fedha za kutosha kukidhi gharama halisi za uendeshaji na matengenezo kwa lengo la kuboresha huduma zitolewazo.
Aidha Mamlaka ya Maji Dodoma imeeleza kuwa bei zinazopendekezwa zitaiwezesha mamlaka kumudu gharama zote za utoaji huduma pamoja na mambo mengine, kuendelea kuongeza ubora wa maji, kuiwezesha mamlaka kuwa endelevu na kukidhi matarajio ya wana Dodoma.
Kwa upande wa wakilishi wa wananchi Revina Petro Lamiula ametoa maoni kwa kusema kuwa pamoja na bei kupandishwa ila wanaitaka mamlaka ya maji safi (Duwasa) kuhakikisha wanaboresha huduma zao.
No comments:
Post a Comment