Thursday, July 27, 2017

AOMBA WALIMU WA SEKONDARI HURIA WAPEWE MOTISHA

Na John Gagarini, Kibaha

SERIKALI imeombwa kuwalipa walimu wanaofundisha vituo vya shule huria ambazo ziko chini ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ili kuwapa motisha walimu hao.

Hayo yalisemwa na meneja wa shule ya Pangani Remedial Open School iliyopo wilayani Kibaha Ally Mohamed na kusema kuwa kuwalipa walimu hao itakuwa moja ya motisha kuwafanya wafundishe kwa moyo.

Mohamed alisema kuwa shule hizo zimekuwa mkombozi kwa wanafunzi ambao wamekosa nafasi za kwenda shule za sekondari na watu wazima waliokosa nafasi hiyo.

“Shule hizi ambazo zamani zilikuwa ni kwa ajili ya watu wazima kwa sasa zimeboreshwa na zinatoa elimu ya sekondari kama kawaida na wanapofaulu mitihani ya kidato cha nne wanakwenda kidtao cha tano kama wale walio kwenye mfumo rasmi hivyo kuna haja ya walimu wake kulipwa kama walimu wenzao wa shule za serikali,” alisema Mohamed.

Alisema kuwa walimu hao kwa sasa wanalipwa na shule hizo lakini kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakijitolea kwani uwezo wa kuwalipa mishahara hawana ambapo Taasisi hiyo imekuwa ikisimamia mitihani ya Kujipima huku ile ya kidato cha pili na ile ya kidato cha nne ikisimamiwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NACTE).

“Shule hizi kwa sasa zimekuwa mkombozi kwa wanafunzi hao ambao zamani walikuwa hawana pa kwenda hivyo tunaomba serikali kuliangalia suala la kuwalipa walimu hao ili kuwapa hamasa ya kufundisha ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule hizo,” alisema Mohamed.

Alisema kuwa mfumo huo uliboreshwa mwaka 2014 ambapo ulisajili vituo hivyo ambavyo vinachukua wanafunzi ambao walishindwa kuendelea na masomo kama vile ukosefu wa ada, mimba, mazingira magumu, yatima na watu wazima waweze kujiendeleza.

Aidha alisema kuwa kwa sasa zinachukua wanafunzi wenye umri kati ya miaka 12 hadi 24 ambao wanasoma kwa miaka minne huku wale wenye kuanzia miaka 25 husoma kwa miaka miwili,shule hiyo ilianza mwaka 1997 na ina wanafunzi 100.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment