Thursday, July 27, 2017

WATAKIWA KUEPUKA NYAMA ZA MITAANI

Na John Gagarini, Kibaha

WANANCHI wa kata ya Picha ya Ndege wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kuacha kununua nyama zinazouzwa mitaani kwa bei nafuu kwani ni hatari kwa maisha yao.

Hayo yalisemwa na diwani wa kata hiyo Robert Machumbe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kufuatia kuenea kwa taarifa kuwa kuna watu wanauza nyama mitaani zikiwa zimewekwa kwenye ndoo.

Machumbe alisema kuwa watu hao wamekuwa wakichukua ngombe ambao wamekufa maeneo mbalimbali kisha kuwauzia wanachi nyama hiyo kwa baei nafuu ya shilingi 2,000.

“Wananchi nawaomba mjihadhari na nyama hizi zinazouzwa mitaani ni hatari kwa afya zenu kwani hamjui nyama hizo zinatoka wapi kwani hazijapimwa na daktari hali ambayo ni hatari,” alisema Machumbe.

Alisema kuwa wananchi wasipende kununua nyama hizo bali wanunue sehemu maalumu ambako ni kwenye mabucha ya kuuzia nyama ili wale nyama ambayo imepimwa na ni salama kwa afya zao.

Kwa upande wake ofisa mifugo wa kata ya Picha ya Ndege Mlaki alisema kuwa alipata taarifa wiki iliyopita kuwa kuna ngombe walikufa kwa moja ya wafugaji wa Lulanzi na watu hao waliichukua nyama hiyo na kuiuza mtaani.

Mlaki alisema kuwa kuna athari ningi zinazotokana na watu kula nyama ambazo hazijapimwa kwani wanaweza kuambukizwa magonjwa mbalimbali kama vile tb, tumbo, kuharisha na magonjwa mengine.   

Mwisho.

No comments:

Post a Comment