Thursday, July 27, 2017

DEREVA AFA AJALINI

                                 Na John Gagarini, Kibaha

DEREVA wa gari la mizigo ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja amekufa baada ya gari alilokuwa akiliendesha kugongwa na gari lingine kwenye ajali iliyosababisha magari matatu kugongana.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mjini Kibaha kwa vyombo vya habari na kamanda wa polisi mkoani Pwani Jonathan Shana ilisema kuwa katika tukio hilo mtu mmoja alijeruhiwa.

Kamanda Shana alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 20 majira ya saa 4:20 usiku barabara kuu ya Dar es Salaam Morogoro eneo la Picha ya Ndege wilayani Kibaha.

Shana alisema kuwa gari aina ya Scania lenye namba za usajili T 774 BBU likiendeshwa na dereva asiyefahamika liligonga gari lililokuwa likiendeshwa na dereva asiyefahamika lenye namba za usajili T 678 BRD lenye tela namba T 293 BVA na Scania T 188 AVN likiendeshwa na Hashimu Mhina (36) wa Dar es Salaam.

“Chanzo cha ajali hii ni dereva wa gari la kwanza kuyapita magari mengine bila ya kuchukua tahadhari ambapo alikimbia mara baada ya ajali hiyo na tunamtafuta tumempa siku tatu ajitokeze na asipojitokeza tutamtafuta ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema Shana

Mwisho

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia wahamiaji 44 kutoka nchi ya Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa wahamiaji hao haramu walikamatiwa wilayani Bagamoyo.

Kamanda Shana alisema kuwa wahamiaji hao haramu walikamatwa eneo la Razaba kata ya Makurunge Tarafa ya Mwambao wilayani humo wakiwa wametelekezwa kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Alisema kuwa  kufuati tukio hilo jeshi lake linaendelea na uchunguzi kujua watu waliohusika na tukio la kuwasafirisha wahamiaji hao haramu kisha kuwatelekeza.

“Tunafuatilia kujua vitu vingi ikiwa ni pamoja na wanaowafadhili wahamiaji hao haramu kwani kumekuwa na baadhi ya watu wanaowasafirisha wahamiaji hao ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao,” alisema Shana.


Mwisho

No comments:

Post a Comment