Thursday, July 27, 2017

WAZIRI WA AFYA ARIDHIA MLANDIZI HOSPITALI WILAYA





                                       Na John Gagarini, Kibaha

WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amekubali maombi ya Kituo cha Afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani kuwa Hospitali ya wilaya.

Alitoa tamko hilo kwenye uwanja wa Mtongani Mlandizi wilayani Kibahya wakati akipokea Magari mawili ya kubeba wagonjwa na vitanda vitatu vya kuzalishia mama wajawazito kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa na gari moja kutoka kwa Rais Dk John Magufuli.

Alisema kuwa ombi lililotolewa na Mbunge huyo kwa viongozi wa ngazi za juu na kwake amelikubali hivyo mganga mkuu wa wilaya anapaswa kuandika barua na kuzipeleka sehemu husika kisha zifikishwe wizarani kwa ajili ya utekelezaji.

“Mbunge wenu amekuwa akipigania kituo hichi kwa muda mrefu kama alivyosema hivyo naona hakuna kipingamizi ili mradi tu taratibu zifuatwe ili kufikia hatua hiyo lengo kubwa ni kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Mwalimu.

Awali mbunge wa Jimbo hilo Hamoud Jumaa lisema kuwa maombi hayo alishayatoa kwa viongozi mbalimbali ikiwemo kwa Rais wa Awamu ya nne Dk Jakaya Kikwete na Rais Dk John Magufuli.
Jumaa alisema kuwa kituo hicho kwa sasa kinahudumia watu wengi tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo kwa sasa wanakaribia watu 100,000 hivyo kuna haja kabisa ya kuwa hospitali ya wilaya.

“Tuliambiwa tufanye maboresho mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga jengo la upasuaji, chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na kuweka uzio vitu vyote hivyo tayari tumevifanya hivyo ombi letu hilo tunaomba ulifanyie kazi kwani tunaamini huduma zitaboreka,” alisema Ummy.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Beda Mmbaga alisema kuwa watahakikisha wanaboresha mahitaji yote yanayotakiwa ili kutoa huduma za ubora kwa wananchi wanaokwenda kuhudumiwa hapo.


Mwisho.   

No comments:

Post a Comment