Thursday, July 27, 2017

POLISI PWANI WAKAMATA VIFAA VYA UVUVI HARAMU




                          Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia Makamba Sixbert (32) na Doto Mwinyi (45) wakazi wa Mlingotini wilayani Bagamoyo kwa tuhuma za kukutwa na vifaa vya uvuvi haramu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana alisema kuwa watu hao walikamatwa kwenye msako.

Shana alisema kuwa mtuhumiwa Sixbert  na Mwinyi walikamatwa Julai 25 majira ya saa 8 usiku maeneo ya Mlingotini kata ya Zinga baada ya msako maalumu wa makosa mbalimbali ukihusisha askari wa Jeshi la polisi wilaya ya Bagamoyo, Polisi Makao makuu, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na maofisa uvuvi na mifugo wa wilaya hiyo.

“Mtuhumiwa huyo wa kwanza alikutwa na Scoopy Net moja, vioo vya kuogelea vitatu, mitarimbo mitatu, bunduki moja ya kuulia samaki, mikuki ya kuulia samaki mitatu na viatu vya kuogelea (Slipers) pea tatu huku mtuhumiwa wa pili akishikwa na Cylinder Gas walivyokuwa wakivitumia kwenye uvuvi haramu,” alisema Shana.

Kwenye tukio lingine madereva wawili wa pikpiki Juma Ally (37) na Mduga Agustino (25) kwa tuhuma za kupatikana na mitambo mitano ya kutengenezea pombe ya Moshi maarufu kama Gongo.

Kamanda Shana alisema kuwa tukio hilo limetokea Julai 25  majira ya saa tano asubuhi maeneo ya Lugoba kata ya Lugoba wilaya ya Kipolisi Chalinze wilayani Bagamoyo.

“Madereva hao wa pikipiki pia walikutwa na pombe ya Moshi lita 40 na lita 60 za Molasesi wakiwa wamezipakiza kwenye pikipiki yenye namba za usajili T 399 BHS aina ya Sanlg,” alisema Shana.

Aidha walifanikiwa kuwakamata Ahmada Hassan (45) mkazi wa Gogoni na wenzake watano kwa tuhuma za wizi wakiwa na Sabufa aina ya Kodec inayodhaniwa kuwa ni ya wizi.

Shana alisema watu hao walikamatwa maeneo ya Dunda kata ya Dunda Tarafa ya Mwambao wakituhumiwa kujihusisha na matukio ya uhalifu ikiwa ni pamoja na uporaji nyakati za usiku kwenye maeneo mbalimbali wilayani

“Misako wanayoifanya ni endelevu na askari shupavu wametawanywa kila kona kuhakikisha hali ya amani inakuwepo kwenye makazi ya wananchi na sehemu za biashara,” alisema Shana.

Aliwataka watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwa kutafuta shughuli nyingine za kufanya za kuwaingizia kipato halali kwani hawatasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Mwisho 


No comments:

Post a Comment