Na John
Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha
Soka wilaya ya Kibiti (KFA) mkoa wa Pwani kimemshukuru mwanasoka anayecheza soka
la kulipwa kwenye timu ya KRC Genk ya Ubelgiji Mbwana Samatta kwa kuwapatia
jozi za jezi kwa ajili ya washindi wa ligi daraja la nne.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katibu wa chama hicho Rashid Mkinga alisema kuwa
wanashukuru msaada huo utakaozisaidia timu zitakazoshinda na kuwakilisha wilaya
hiyo kwenye mashindano ya mkoa.
Mkinga
alisema kuwa waliandika barua kwa Samata kwa ajili ya kuomba vifaa mbalimbali
vya michezo ambapo aliwajibu na kusema kuwa atawapatia.
“Samatta kwa
kupitia mwakilishi wake Said Ngulupi alitupatia jozi ya seti tatu ambazo
tutawakabidhi washindi watatu wa juu ambao ni wawakilishi wa wilaya yetu,”
alisema Mkinga.
Alisema kuwa
hawana cha kusema zaidi ya kushukuru kwa msaada huo mkubwa aliowapatia licha ya
yeye kuwa mbali lakini anathamini vijana wenzake ambao wanacheza soka hapa
nchini.
“Tunamshukuru
Samatta kwa mchango wake kwani awali tulikuwa hatuna zawadi za kuwapa washindi
zaidi ya kombe kwa ajili ya mshindi wa kwanza kwani ametukomboa kwa kutupa
msaada huo,” alisema Mkinga.
Aidha alisema
kuwa mpira unachezwa kama kawaida na kuna amani kubwa siyo kama watu
wanavyofikiria kwani ulinzi uko wa kutosha na hadi sasa hakuna tukio lolote la
kutishia lililotokea.
“Kupitia
michezo amani imetawala na hakuna vurugu zozote au tishio lolote la kutishia
amani hivyo watu wasiwe na wasiwasi kwenye wilaya yetu ambayo ilikumbwa na
mauaji na kuwafanya watu kuwa na hofu,” alisema Mkinga.
Alibainisha
kuwa ligi ya Kibiti ndiyo yenye timu nyingi ndani ya mkoa wa Pwani ambapo
kwenye ligi daraja la nne jumla ya timu 19 zinachuana na timu zilizosajiliwa ni
31 na bado kuna zingine zinahitaji usajili.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment