Thursday, July 27, 2017

GARI LATUMBUKIA MTO WAMI WAWILI WAFA

                                   
                                         Na John Gagarini,Kibaha

MADEREVA wawili wamekufa baada ya gari walilopanda kugonga kingo za daraja la mto wa wami na kuangukia mtoni

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kamanda wa polisi mkoa wa Pwani Jonathan Shana amesema kuwa gari lililopata ajali ni mali ya kampuni ya Usangu Logistics.

Shana amesema kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa saba usiku na kulihusisha gari lenye usajili namba T 857 ARP aina ya Scania likiendeshwa na Yahaya Karimu miaka kati ya (30)  na (35) akiwa na dereva mwenzake ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja likitokea Dar es Salaam kwenda Arusha.

Amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni breki za gari hilo kukatika na kugonga kingo za daraja hilo kisha kuanguka mtoni 

Na John Gagarini, Kibaha

MTU mmoja aliyetambulika kwa jina la Mwesigwa Mberwa (23) amekutwa amekufa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Msukuma iliyopo Mlandizi wilayani Kibaha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jonathan Shana zimesema kuwa marehemu alikuwa amelala chumba namba 38.

Shana amesema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 22 majira ya saa 12 jioni eneo la kitongoji cha Usalama wilaya ya Kipolisi Mlandizi ambapo marehemu alipanga kwenye nyumba hiyo tangu Julai 19.

Amebainisha kuwa muhudumu Kulekwa Kulwa ndiye aliyegundua kufa kwa marehemu baada ya kutia mashaka kutokana na kutomwona kutoka nje mteja wake tangu alipoingia na kwenda kutoa taarifa polisi.

Amesema kuwa polisi walipofika kwenye chumba hicho iliwabidi kuvunja mlango na kuukuta mwili wa marehemu ukiwa hauna jeraha lolote mwilini mwake na kupelekwa hospitali Teule ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi na ulifanyiwa uchunguzi na utakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

ABIRIA waliokuwa wakisafiri na basi la kampuni ya Tashirifu waliokuwa wakisafiri kutokea Dar es Salaam kwenda mkoani Tanga wamenusurika kifo baada ya basi hilo kuwaka moto.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi mkoani Pwani kwa vyombo vya habari Jonathan Shana imesema kuwa basi hilo liliteketea lote na moto huo haukuleta madhara yoyote kwa binadamu na kusababisha hasara ikiwemo mizigo ya abiria.

Kamanda Shana amesema kuwa ajali hiyo ilitokea Julai 22 majira ya usiku eneo la Kwa Zoka kata ya Vigwaza wilaya ya Kipolisi Chalinze barabara kuu ya Dar es Salaam Morogoro.

Amesema kuwa basi hilo lenye namaba za usajili T 681 DFX aina ya Yutong lilikuwa likiendeshwa na dereva aitwaye Salum Issa (42) liliwaka moto hata hivyo chanzo cha moto huo hakikuweza kufahamika mara moja na polisi wanaendelea na uchunguzi kujua chanzo cha moto huo.

Mwisho.

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba za watu watatu na kusababisha hasara ikiwa ni pamoja na pikipiki mbili zenye thamani ya shilingi milioni 3.8

Kamanda wa polisi mkoani humo Jonathan Shana amesema kuwa mbali ya kuchoma nyumba hizo pia waliingia kwenye mazizi na kuchinja ngombe ambao idadi yao haijajulika kisha kuondoka na nyama na kubakiza utumbo.

Shana amesema kuwa tukio hilo lilitokea Kijiji cha Vikumburu kata ya Vikumburu Tarafa ya Chole wilaya ya Kisarawe ambapo hata hivyo haikuweza kufahamika chanzo cha uhabifu huo wa mali ambao thamani yake haijajulikana.

Amewataja watu waliochomewa nyumba zao kuwa ni Joseph Simboyi (55), Rebeka Yona (23) na Selina Simon (28).

Aidha amewataja watuhumiwa wa tukio hilo kuwa ni Abdala Shomary (53), Omary Athuman (42) Seifu Shomary (38), Uzalimata Selasela (36) Salum Shomary (40) na Jumanne Omary (49) wote wakazi wa Vikumburu.


Mwisho. 

No comments:

Post a Comment