Na John
Gagarini, Kibaha
HATIMAYE
Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani imeanza mradi wa ujenzi wa stendi ya
kisasa wenye thamani ya shilingi billion 3.4.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ofisa habari wa Halmashauri
hiyo Innocent Byarugaba amesema kuwa stendi hiyo itaondoa tatizo la mji huo
kutokuwa na stendi ya uhakika kwa kipindi cha takribani miaka 40.
Byarugaba alisema
kuwa stendi ambayo inatumika kwa sasa ni ndogo na imejengwa kwenye hifadhi ya
barabara na ambapo iko ndani ya mita 60 ikitakiwa kuondolewa na ina hudumia mabasi
ya mikoa 24.
“Stendi mpya
mara itakapokamilika inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 60 kwa
wakati mmoja na itajengwa kipindi cha miezi sita na kukamilika mwishoni mwa
mwaka huu au Januari mwakani,” alisema Byarugaba.
Alisema kuwa fedha
zinazotumika kwenye ujenzi huo ni ufadhili kutoka benki ya dunia kupitia benki
kuu ya Tanzania kwenye mradi wa uendelezaji wa Miji (ULGSP) unaoendeshwa kwenye
miji 18 hapa nchini.
“Stendi itakuwa
na miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kituo cha polisi, ofisi za mabasi,
sehemu ya texi, Bajaji, pikipiki, huduma ya vyoo, vibanda vya kupumzikia
abiria, Atm, kituo cha mafuta,gereji, hoteli na kizimba cha kuhifadhia takataka
na huduma nyingine muhimu,” alisema Byarugaba.
Aliwataka
watu wenye viwanja vinavyozunguka stendi hiyo kujenga ambapo ramani iliyopitishwa
ni kuanzia ghorofa moja na kuendelea pamoja na wale walioko kwenye eneo la
kitovu cha mji kufanya ujenzi kama sheria zinavyowataka.
Aidha alisema
kuwa ujenzi huo unafanywa na kampuni ya Group Six International Ltd ambayo
ilijenga stendi ya kisasa ya Msamvu mkoani Morogoro chini ya wataalamu washauri
Ace Consult, Lupta Consult na Mhandisi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment