Monday, July 20, 2015

BARABARA YATENGEWA BILIONI MUFINDI KASKAZINI



Na John Gagarini, Iringa
BARABARA ya Kinyanambo C hadi Kisusa yenye urefu wa kilometa 131kwenye Jimbo la Mufindi Kaskazini wilaya ya Mufindi mkoani Iringa imetengewa kiasi cha shilingi billioni 1.2 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida.
Hayo yalisemwa na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini Mahmoud Mgimwa wakati akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mpanga Tazara akielezea juu ya kukabiliana na changamoto ya barabara katika Jimbo hilo.
Mgimwa alisema kuwa fedha hizo zimetengwa katika kipindi cha bajeti ambayo imeanza mwezi huu na tayari ujenzi wa barabara hiyo umeshaanza kwa kuweka makalavati ikiwa ni hatua za mwanzo za ujenzi huo.
“Barabara hii tayari imeshakabidhiwa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) mkoa kutoka Halmashauri ya mji wa Mafinga hali ambayo sasa imeipandisha hadhi hivyo itakuwa kwenye mikakati ya kuwekewa lami kupitia kampuni ya (MCC),” alisema Mgimwa.
Alisema kuwa matengenezo hayo yataboresha ubora wa barabara hiyo ambayo ni tegemeo na kuifanya kupitika wakati wote bila ya usumbufu na kurahisisha mawasiliano kwa wananchi na kwa wakulima ili waweze kupeleka mazao yao kwenye masoko baada ya kuvuna.
“Barabara hii ambayo inapita kwenye maeneo ya Itimbo, Ihalimba, Usokamu, Mapanda na Kisusa itakuwa ni moja ya barabara amabzo ziko kwenye mpango wa kuboreshwa na baada ya kupandishwa hadhi halmashauri itapata unafuu ambapo fedha ambazo zingetumika kuitengeneza sasa zitatumiwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo,” alisema Mgimwa.
Aidha alisema kuwa barabara nyingine ni Kinyanambo A yenye urefu wa kilometa 151 ambayo inapita maeneo ya Msavanu, Mkombavanu, Sadani na Madibila nayo ujenzi wake tayari umeanza.
Pia alisema kuwa barabara ya Johns Corner yenye urefu wa kilometa 107 tayari imejengwa kwa kiwango cha lami urefu wa kilometa tano nab ado ujenzi wake unaendelea.
Alibainisha kuwa barabara hiyo inapita kwenye maeneo ya Mtili, Ifwagi, Mdabulo, Ihanu, Lulanga hadi Mpanga Tazara iko kwenye mpango wa kupandishwa hadhi ili ichukuliwe na (TANROADS), na barabara ya Mpanga Tazara hadi Mlimba ambayo imetengwa kiasi cha shilingi milioni 800.
“Barabara ya Mpanga Tazara hadi mlimba kwani inaunganisha wilaya mbili za Mufindi na Kilombero ni muhimu sana kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa wakulima kupeleka mazao yao kwenye masoko ambayo yana bei nzuri kama vile Makambako, Kilombero, Mbeya na Dar es Salaam,” alisema Mgimwa.
Mgimwa alisema kuwa barara nyingine ziko kwenye mchakato wa kuwapata makandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi katika bajeti inayoanzia mwezi huu wa Julai.
Mwisho.
Na John Gagarini, Iringa
JIMBO la Mufindi Kaskazini wilayani Mufindi mkoani Iringa linahitaji Transfoma 60 ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa umeme kwenye kata tatu za Mpanga Tazara, Ikwea na Ikongosi.
Changamoto hiyo ya ukosefu wa umeme iko kwenye kata hizo kati ya kata 13 za Jimbo hilo ambapo upatikanaji wa Transfoma hizo utasaidia kuondoa kabisa ukosefu wa nishati hiyo kwa baadhi ya vitongoji.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya changamoto kwenye Jimbo la Mufindi Kaskazini, Mbunge wa Jimbo hilo Mahmoud Mgimwa alisema kuwa kwa sasa mchakato wa kutafuta Transfoma unaendelea.
“Thamani ya Transfoma moja ni kati ya shilingi milioni 40 na 60 na tunaendelea kuhakikisha vinapatikana ili kuondoa kabisa tatizo la umeme ndani ya jimbo letu lakini eneo kubwa tayari wanapata umeme,” alisema Mgimwa.
Alisema kuwa anaamini kuwa umeme utapatikana muda si mrefu na kuwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi juu ya upatikanaji wa nishati hiyo muhimu ya umeme.
Aidha alisema kuwa maeneo mengi kwa sasa yanapata umeme hadi vijijini na sehemu chache zilizobaki tatizo hilo litakwisha na jitihada zinaendelea ili kufanikisha suala hilo.
Mwisho.    

No comments:

Post a Comment