Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani
limefanikiwa kukamata silaha aina ya Sb Mchine Gun (SMG) ikiwa na risasi 30
kwenye magazini ambayo majambazi waliwapora askari eneo la Yombo Jijini Dar es
Salaam Aprili 15 mwaka huu.
Mbali ya silaha hiyo pia walikamata
silaha nyinge mbalimbali zikiwemo bunduki nne, risasi 153, mabomu na nyaya za
milipuko katika msako maalumu wa kusaka wahalifu wanaodaiwa kuhusika katika
matukio kadhaa yakiwemo ya uvamizi wa vituo vya Polisi na taasisi za fedha
Mkoani humo na mikoa jirani ukiwemo wa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi mkoani
humo Jafari Ibrahim alisema silaha hiyo iliporwa na majambazi hayo kutoka
mikononi mwa polisi waliokuwa doria kisha kutoweka nayo ambayo ilikuwa ni ya
kituo cha polisi cha Tazara.
Kamanda Ibrahimu alisema kuwa silaha hiyo
ilikuwa na namba 14302621 pia silaha nyingine iliyokamatwa ni Short Gun yenye
namba G 74533 ambayo iliporwa Juni 10 mwaka huu kwenye kituo cha mafuta cha
Mogas kilichopo Mkata wilaya ya Handeni mkoani Pwani.
“Kukamatwa silaha hizi ni mafanikio ya
operesheni iliyofanywa na jeshi katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita na
tunawapongeza wananchi kwa ushirikiano waliouonyesha uliofanikisha kukamatwa
kwa silaha hizi na vitu vingine,” alisema Ibrahim
Alisema kuwa mbali ya silaha
zilizotajwa hapo juu pia waliweza kukamata silaha nyingine ambazo ni Visu 11,Mapanga
4,Majambia 3,Risasi 20 za SMG, Risasi 103 za Shortgun, Milipuko ya mabomu 3,Vipande
vidogo vya nondo 42,fyuzi zilizotegwa 24,Fyuzi tupu 56,Water Gel Explosive 3, Silicon
Rubber 100% moja, Nyaya 3 za Milipuko, Bunduki 2 zilizotengezwa kienyeji pamoja
na bunduki moja aina ya Rifle.
"Sihala hizi zote zipo hapa kwetu
na kwa kweli ndugu waandishi kama silaha zingeendelea kuwa mikononi mwa
wahalifu ni wazi kuwa madhara kwa mali na maisha yetu yangekuwa hatarini,ninyi
kama wadau muhimu katika jitihada za kupambana na wahalifu kupitia vyombo vya
habari mnao wajibu wa kuendelea kuelimisha jamii kuendelea kushirikiana na
jeshi la Polisi katika mapambano haya yanayohitaji nguvu ya pamoja,” alisema
Ibrahim
Aidha alisema kuwa ni wazi kuwa
mafanikio haya yametokana na jamii kutoa ushirikiano mkubwa kwa polisi katika
kuwabaini wahalifu,kubaini matishio ya kiusalama na maficho ya magenge ya
kihalifu kwenye mapori mbalimbali yaliyopo mkoani Pwani.
Alibainisha kuwa mbali ya kukamata
silaha hizo pia wamekamata wahalifu 27 wanaotuhumiwa kuhusika katika matukio
mbalimbali ikiwemo la uporaji silaha kituo cha polisi Yombo Dar es Salaam na
waliohusika kwenye uporaji taasisi za kifedha na taratibu za kuwafikisha
mahakamani zimekamilika.
Mwisho
Na John Gagarini, Kibaha
HUKU mchakamchaka wa kuwania
nafasi za ubunge na udiwani zikiwa zinaendelea nchini jumla ya wagombea wanne
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM)Jimbo la Kibaha Mjini watachuana kupata
mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa katibu wa CCM
Kibaha Mjini Abdala Mdimu alisema kuwa wagombea hao ndani ya chama ndiyo
waliorejesha fomu za kuomba ridhaa ya kuchaguliwa na Wanaccm ili kugombea
nafasi hiyo.
Mdimu alisema kati ya wagombea
hao waliorejesha fomu ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Silvestry
Koka ambaye atachuana na wanaccm wengine watatu ambao nao wameomba kuwania
nafasi hiyo.
Aliwataja wagombea wengine
kwenye kinyanganyiro hicho kuwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa NEC
Jimbo hilo Rugemalila Rutatina, Idd Majuto, Rashid Bagdela na Abdulaziz Jaab.
Katika Jimbo la Kibaha Vijijini
jumla ya wagombea sita wamejitokeza kuwania nafasi hiyo akiwemo aliyekuwa
Waziri wa Nishati na Madini Dk Ibrahim Msabaha watakaopambana na Mbunge wa
Jimbo hilo Hamoud Jumaa.
Katibu wa CCM Kibaha Vijijini
alisema kuwa wengine wanaowania nafasi hiyo ndani ya chama ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu Taifa NEC Jimbo hilo Allen Bureta, Hussein Chuma, Janeth
Munguatosha na Shomary Sangali.
Mwisho.
Na John Gagarini, Bagamoyo
JUMLA ya wagombe 10 wa nafasi
ya Ubunge wamerejesha fomu za kuwania kuchaguliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kwenye Jimbo la Bagamoyo Mkoani Pwani ambalo nafasi yake inatetewa na Waziri wa
Elimu na Mafunzo Dk Shukuru Kawambwa.
Kwa mujibu wa katibu wa CCM
wilaya ya Bagamoyo Kombo Kamote alisema kuwa wengine waliorejesha fomu ni
pamoja na Meya wa Mji Mdogo wa Bagamoyo Abdul Sharifu.
Kamote aliwataja wengine kuwa
ni Muharami Mkenge, Salim Abeid, Mbonde Mbonde, Methew Yungwe, Maulid Mtulya,
Fabian Said, Lekesani, Mvule na Chacha Wambura.
Katika Jimbo la Chalinze mbunge
wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete anatarajiwa kupambana na aliyewahi kuwa
Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga Iman Madega.
Wengine ni pamoja na Mbaraka
Tamimu, Changwa Mkwezu, Omar Kabanga. Katika hatua nyingine jumla ya
wagombea 18 wa ubunge viti maalum mkoani Pwani watawania kuchaguliwa bada ya
kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo ndani ya chama.
Mwisho.
Na John Gagarini, Iringa
WAFADHILI toka nchi ya
Australia wametoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 11 kuchangia mradi mkubwa wa
maji kwenye Jimbo la Mufindi Kaskazini wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Akizungumza na waandishi wa
habari mjini Mafinga Mbunge wa Jimbo hilo Mahmoud Mgimwa alisema kuwa wafadhili
hao wametoa fedha hizo ili kukabiliana na changamoto za maji kwenye Jimbo hilo.
Mgimwa ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii alisema kuwa fedha hizo zitatumika kwenye mradi
mkubwa ambao utaondoa kabisa tatizo la maji kwenye Jimbo hilo.
“Mradi huu ni mkubwa na
utaondoa kabisa changamoto hii ya maji kwani baadhi ya maeneo hayapati maji
lakini mara utakapokamilika utakabili tatizo hilo na kubaki historia kwani
maeneo yote yatapata maji ya uhakika,” alisema Mgimwa.
Alisema kuwa huku wafadhili hao
wakitoa fedha hizo serikali nayo itachangia kiasi cha shilingi milioni 130
ambapo wafadhili hao watakuja na kuangalia mradi huo jinsi utakavyoendeshwa.
“Katika bajeti ya mwaka
2014/2015 serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kununua
pampu tatu kutoka nchini Afrika Kusini na Arusha ambazo zitafanya maji yaweze
kutoka kwa uhakika ambapo kwa sasa utokaji wake si mzuri kutokana na uchakavu
wa miundombinu yake zikiwemo pampu hizo,” alisema Mgimwa.
Aidha alisema kuwa katika
bajeti ya mwaka 2015/2016 serikali imetoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya
kuboresha miundombinu ya maji ili kukabiliana na uchakavu.
Mwisho.
Na John Gagarini, Iringa
MBUNGE wa Jimbo la Mufindi
Kaskazini na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mamhoud Mgimwa amewaomba wadau
mbalimbali wa maendeleo kusaidia kupatikana kwa vifaa vya X-Ray kwenye
hospitali ya Mafinga ambayo ni ya Wilaya ya Mufindi ili iweze kutoa huduma zake
kwa uhakika.
Mgimwa alisema kuwa hospitali
hiyo ambayo imeboreshwa na kuwa ya kisasa kupita hospitali zote za mkoa wa
Iringa inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa hivyo.
Alisema kuwa Mgimwa yeye pamoja
na wananchi wa Jimbo hilo pamoja na serikali wamefanikiwa kuifanya hospitali
hiyo kuwa ya kisasa na kutoa huduma bora lakini changamoto yake ni X-Ray.
“Tunaishukuru serikali kwani
ilitoa kiasi cha shilingi milioni 600 ambazo zilitumika kufanya kazi mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kujenga wodi nzuri hivyo tunaomba wadau mbalimbali waendelee
kujitokeza kuisaidia kukabilina na changamoto zilizopo,” alisema Mgimwa.
Aidha alisema kwa sasa
hospitali hiyo ina jumla ya vitenda 10 vya kujifungulia akinamama ambapo kila
kitanda kina thamani ya shilingi milioni 1.2.
“Kwa jumla huduma ya afya
kwenye hospitali yetu ya wilaya ni nzuri licha ya kwamba kuna changamoto kidogo
lakini hata hivyo tunaendelea kukabiliana nazo ili ziweze kuboreka,” alisema
Mgimwa.
Alibainisha kuwa kwa
kushirikiana na wadau wa maendeleo watazikabili changamoto zilizopo ili
wananchi waweze kupata huduma bora mara waendapo kupata huduma.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment