Na John Gagarini, Iringa
KATIKA kukabiliana na
changamoto za ukosefu wa nyumba za walimu Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini wilayani
Mufindi mkoani Iringa Mahamoud Mgimwa ametoa bati 70 na mifuko 30 ya Saruji kwa
ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu wa shule ya Msingi ya Mpanga Tazara.
Akizungumza na wakazi
wa Kijiji hicho alipotembelea kuangalia shughuli za maendeleo alisema kuwa
ameamua kutoa vifaa hivyo ili kuhakikisha wlaimu wanakaa kwenye mazingira
mazuri.
Mgimwa ambaye ni Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii alisema kuwa wananchi wa Kijiji hicho walikuwa na
kilio cha muda mrefu cha walimu kukosa nyumba za kuishi hivyo ameona ni vema
akatoa vifaa hivyo ili viweze kusaidia katika ujenzi wa nyumba za walimu.
“Kama mnavyojua
mazingira ya huku yako pembezoni hivyo lazima kuyaweka vizuri ili watumishi hao
waweze kukaa sehemu ambayo ni nzuri ili waweze kufanya kazi zao kwa amani,”
alisema Mgimwa.
Alisema kuwa sekta ya
elimu ina changamoto nyingi lakini yeye kwa kushirikiana na wananchi
atahakikisha wanazikabili kwa kutoa misaada mbalimbali ili kuboresha mazingira
ya usomaji.
“Awali shule hii
ilikuwa na tatizo la choo lakini tulipigana na kuhakikisha choo kimejengwa
tunakwenda kutatua changamoto zilizopo hatua kwa hatua ili kuhakikisha sekta ya
elimu inapata mafanikio,” alisema Mgimwa.
Aidha alisema kuwa
wazazi nao wanapaswa kuhakikisha wanachangia michango mbalimbali kwa ajili ya
wanafunzi ili waweze kupata elimu inayotakiwa kwani kuna baadhi ya changamoto
zinaweza kutatuliwa na wazazi.
Kwa upande wake Diwani
wa kata ya Mpanga Tazara Flavian Mpanda alimshukuru mbunge huyo kwa kutoa vifaa
hivyo na kusema kuwa vimekuja wakati muafaka kwani ujenzi wa nyumba za walimu
ilikuwa ni changamoto kubwa.
Mpanda alisema
jitihada zinazofanywa na mbunge huyo kuhakikisha shule hiyo inakuwa na
mazingira mazuri zinapaswa kupongezwa na wapenda maendeleo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment