Tuesday, July 28, 2015

CCM JITOKEZENI KWA WINGI KWENYE KURA ZA MAONI NA UCHAGUZI MKUU

Na John Gagarini, Kibaha
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kibaha Mjini wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kujitokeza kwa wingi ili kukipigia kura chama hicho kwenye uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu na si kujitokeza kwa wingi kwenye kura za maoni pekee.
Hayo yalisemwa na katibu wa CCM jimbo la Kibaha Mjini Abdala Mdimu wakati akiwanadi wagombea watano wa chama wanaowania kuteuliwa Ubunge wa Jimbo hilo kwenye kata ya Picha ya Ndege na Lulanzi.
Mdimu alisema kuwa wanachama wanaotarajiwa kupiga kura za maoni watakuwa wengi ikiwa na maana kwenye uchaguzi wa ndani ya chama lakini nje ya chama yaani uchaguzi mkuu wanachama hawajitokezi kwa wingi.
“Sasa tubadilike kwani CCM ndicho chama chenye wanachama wengi ikilinganishwa na vyama vingine lakini utashangaa wapinzani wanashinda kwa kura nyingi ambazo nyingine zinatoka humuhumu huku wengine wakiwa hawajitokezi kupiga kura lakini kura ndani ya chama ni nyingi sana,” alisema Mdimu.
Alisema kuwa wanachama wote ambao wamekidhi vigezo wanapaswa kujitokeza kupiga kura kwa wingi ndani ya chama na kwenye uchaguzi mkuu kwani kutojitokeza kwenye uchaguzi mkuu utasababisha ushindi kuwa mdogo.
“Tunataka ushindi wa kishindo kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo mlijitokeza kwa wingi na chama kushinda kwa kishindo tunataka wembe huo huo muuendeleze kwani ushindi uko dhahiri,” alisema Mdimu.
Aidha alisema kuwa Wanaccm hawapaswi kuimba wimbo wa ushindi huku hawafanyi kazi kwani wanatakiwa kufanya kazi ili baadaye waje kuimba wimbo wa ushindi kwani moja wapo kati ya wanaowania nafasi ya kuwakilisha chama nafasi ya ubunge ni wazuri.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MUWANIA Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kibaha Mjini wilayani Kibaha mkoani Pwani Rugemalila Rutatina amesema kuwa endapo atateuliwa atakuwa kiongozi na si mtawala.
Aliyasema hayo juzi kwenye kata ya Picha ya Ndege mjini Kibaha wakati akiomba kura kwa wanachama wa matawi ya kata hiyo na kusema kuwa uongozi bora ndiyo utakaowaletea maendeleo wananchi wa Jimbo hilo.
Rutatina ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM NEC kutoka Jimbo hilo alisema kuwa nafasi hiyo ni uongozi wa kuonyesha njia na si kuwa mtawala kwani mtawala yeye ni kutumia nguvu na kuelekeza pasipo yeye kuwajibika.
“Kiongozi ni kuwajibika wewe mwenyewe na kuwaonyesha njia watu unaowaongoza lakini mtawala yeye hana muda wa kutumikia wananchi zaidi ya kuamrisha jambo ambalo halifai kwani si shirikishi kwa wananchi,” alisema Rutatina.
Alisema kuwa ilani inajibu masuala yote ya maendeleo kwani imegusa sekta zote ikiwemo afya, elimu, ardhi, barabara, umeme, maji, mawasiliano na huduma zote za kijamii.
“Endapo mtanichagua nitazingatia mambo matatu ambayo ni ushirikishaji wananchi, ardhi, siasa safi na uongozi bora naamini katika haya yatasaidia kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuwaletea maendeleo,” alisema Rutatina.
Wagombea wengine wanaowania nafasi hiyo ya kukiwakilisha chama kwenye kinyanganyiro cha Ubunge kwenye Jimbo hilo ni Silvestry Koka anayetetea kiti hicho, Abdulaziz Jab, Rashid Bagdela na Idd Majuto.
Mwisho 

No comments:

Post a Comment