Tuesday, July 7, 2015

RAIS KIKWETE AJIANDIKISHA DAFTARI LA KUDUMU ATAKA WANANCHI WAJITOKEZE KWA WINGI

Na John Gagarini, Msoga
RAIS Dk Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kwani ni haki ya  Kikatiba kwa kila mwananchi mwenye sifa.
Aliyasema hayo jana kwenye Kijiji cha Msoga kata ya Msoga wilaya Bagamoyo mkoani Pwani wakati alipojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga kura na kusema kuwa amefurahi kutimiza haki yake.
Dk Kikwete alisema kuwa kwa kujiandikisha huko kutamsaidia mwananchi kuchagua kiongozi anayempenda na si baadaye kulalamika kuwa kiongozi fulani hafai.
“Mimi tayari nimeshapata kitambulisho cha kuweza kumchagua Rais wangu, Mbunge wangu na Diwani wangu kama mtu humtaki mnyime kura kwa kumpigia umtakaye,” alisema Dk Kikwete.
Aidha aliipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kuendelea kupambana kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa licha ya kuwa na maneno mengi kazi yenu ni nzuri na tunaithamini.
“Chapeni kazi changamoto ni kawaida na ni sehemu ya maisha na mtakaposhindwa tuambieni kwani kazi yenu ni nzuri na tunaithamini sana chapeni kazi,” alisema Dk Kikwete.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi nchini Damian Lubuva alisema kuwa licha ya changamoto zilizojitokeza lakini zoezi linakwenda vizuri na matarajio ni makubwa ya kulifanikisha.
Lubuva alisema kuwa hadi sasa mikoa 13 tayari imeshakamilisha zoezi hilo ambapo changamoto inatokana na mfumo mpya wa BVR na tayari watu zaidi ya m 11 wameshaandikishwa.
“Malengo ni kuandikisha watu m 21 hadi 23 mara litakapokamilika mwishoni mwa Julai au Agosti mwanzoni kama mambo yatakwenda vizuri,” alisema Lubuva.
Mkoa wa Pwani una jumla ya vituo 1,752 na mashine za BVR 932 ambapo kata ya Msoga kuna jumla ya vituo 17 zoezi hilo kwa mkoa wa Pwani lilianza jana na litamalizika Julai 20.   
Mwisho.


No comments:

Post a Comment