Na John Gagarini, Kibaha
WATU zaidi ya watano wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamevamia benki ya NMB tawi la Mkuranga,mkoani Pwani na kufanikiwa kuua askari mmoja na kujeruhi watu watatu kisha kupora fedha kiasi ambacho hakijafahamika.
Majambazi hayo walifanikiwa kumuua askari huyo aliyekuwa kavaa kirai kwa kumpiga risasi kichwani baada ya mapambano ya kurushiana risasi.
Askari aliyefariki dunia alitajwa kwa jina la PC Alfred ambaye hakuwa kazini bali alikwenda katika benki hiyo kufuata huduma na kati ya waliojeruhiwa ni pamoja na PC James.
Tukio hilo limetokea mapema leo, baada ya watu hao kufika katika benki hiyo na kuanza kuwashambulia askari wanaolinda katika benki hiyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda walielezea kuwa baadaye watu hao walihamia katika gari lililokuwa linapeleka fedha benki na kuchukua fedha zote kisha kuchukua silaha mbili aina ya SMG na kutokomea kusikojulikana.
Aidha inasadikiwa watu hao walifika katika benki hiyo wakiwa na pikipiki tatu aina ya boksa wakiwa wamebebana mshikaki na walipofanikisha tukio hilo waliondoka.
"Majambazi hayo yalipofika eneo la tukio walianza kufanya mashambulizi kwa askari ambapo walifanikiwa kuwadhibiti askari waliokuwepo kwa kuanza kuwashambulia na kupiga risasi hewani"alisema mmoja wa mashuhuda hao.
Alielezea kuwa askari waliokuwepo eneo la tukio walikimbia na kumuacha mmoja kupambana nao ambapo alizidiwa.
Aidha alieleza kuwa dakika chache baada ya mashambulizi hayo liliingia gari lililobeba fedha ambapo walivamia gari hilo bila kuwepo kwa mtu yeyote na kufanikiwa kubeba fedha zote.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,ACP Jafari Ibrahim alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa kamili mara atakapopata taarifa hizo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment