Tuesday, June 9, 2015

REJESHENI HESHIMA YA RIADHA BALOZI ALI IDD

Na John Gagarini, Kibaha
WANARIADHA wa Tanzania wametakiwa kujiandaa kimataifa zaidi ili kuiletea heshima nchi kama ilivyokuwa miaka ya 70 ambapo Tanzania ilikuwa ikitamba kimataifa na kuipeperusha vema bendera ya Taifa.
Hayo yalisemwa juzi mjini Kibaha na makamu wa pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Idd wakati akifunga mashindano ya riadha ya Taifa ya 54 kwenye viwanja vya Filbert Bayi na kusema kuwa kwa sasa mchezo huo umedorora.
Balozi Idd alisema kuwa wanariadha hao wanapaswa kuweka malengo ya kushindana kimataifa na si kuridhika na kukimbia hapahapa nchini kwani nafasi ya kufanya vizuri kimatiafa bado ipo kinachotakiwa ni kuwekwa mipango mizuri.
“Miaka ya nyuma kulikuwa na wakimbiaji wengi wazuri ambao walikuwa wakikimbia kimataifa na kuiletea sifa nchi yetu na sasa tunapaswa kulenga kimataifa zaidi kwani inasiadia kuitangaza nchi yetu kama ilivyo kwa wenzetu ambao ni majirani zetu Kenya ambao kwa sasa wanatamba kwenye mchezo huo,” alisema Balozi Idd.
Alisema miaka ile kulikuwa na akina Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Juma Ikangaa na wengi waliweka historia ya nchi duniani kwa kufanya vyema kwenye mashindano ya kimataifa hata wakati huu bado nafasi ipo ya kufanya hivyo.
“ Fanyieni kazi Kisayansi mapungufu yaliyojitokeza hadi kusababisha tushindwe kufanya vema katika mashindano ya kimataifa pia wekeni malengo ya muda mfupi na muda mrefu hasa kwa mashindano ya Kimataifa yajayo ili kuweza kurejesha heshima ya mchezo huo kwa Taifa letu,” alisema Idd.
Aidha alisema kuwa serikali zote zimekuwa zikifanya kazi kubwa ya kuwekeza kwenye michezo ambapo hali hiyo imefanya Muungano uendelee kudumu na kujenga mshikamano baina ya Watanzania na zitaendelea kusaidia sekta hiyo ya michezo.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania RT Antony Mtaka alisema kuwa moja ya changamoto inayowakabilini na kukosa mdhamini wa moja kwa moja hali ambayo inasababisha maandalizi ya mashindano kuwa mabaya.
Mtaka ameiomba serikali kuwasaidia wanariadha wa zamani wanaoanzisha shule za Michezo ili waweze kufungua shule nyingi kwa lengo la kuinua michezo hapa nchini kwnai uwekezaji unapaswa kuanzia ngazi ya chini.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
NAIBU Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Juma Nkamia amewataka viongozi wa timu mbalimbali kuhakikisha wanapeleka wanamichezo kwenye mashindano badala ya kupeleka viongozi jambo ambalo linafanya timu hizo zisiweze kufanya vizuri.
Waziri Nkamia aliyasema hayo juzi mjini Kibaha wakati wa kufunga michezo ya Taifa ya Riadha ya 54 kwenye viwanja vya shule ya Filbert Bayi na kusema kuwa baadhi ya timu zilipeleka viongozi badala ya wachezaji.
Alisema kuwa ni vema wachezaji wakapewa nafasi zaidi kwani wao ndiyo wanaokwenda kushindana na viongozi wao wanasimamia masuala ya kiutawala lakini fursa kubwa iwe kwa wachezaji ili kutimiza malengo yao.
“Hapa kwenye mashindano hayo tumesikia kuna timu wamekuja viongozi ni vema nafasi hiyo wakapewa wachezaji ili washindane na si kuleta viongozi ambao hawatashiriki kwa hiyo ushiriki wa timu hiyo haupo,” alisema Waziri Nkamia.
Aidha alisema kuwa mchezo huo unapaswa kuwekewa mikakati ya kuboreshwa ili uweze kurudia kwenye hadhi yake ya zamani ambapo Tanzania ilikuwa ikitamba vilivyo na kuiletea sifa kubwa nchi lakini kwa sasa hali ni tofauti.
Aliwataka wanariadha kuongeza jitihada ili waweze kufikia viwango vitakavyowafanya waweze kushiriki mashindano ya Kimataifa na kuleta medali kama walivyofanya wanariadha wakongwe ambao rekodi za kimataifa hadi leo zimedumu.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI imeombwa kupunguza ushuru wa vifaa vya michezo ili kusaidia malengo ya uanzishwaji wa shule na vituo vya michezo kuinua vipaji vya vijana wadogo ili waje kuwa wachezaji watakaotegemewa na Taifa.
Akizungumza wakati wa ufungaji wa michezo ya Riadha ya Taifa mjini Kibaha mkurugenzi wa shule za Filbert Bayi Ana Bayi alisema kuwa ushuru wa vifaa hivyo vya michezo ni mkubwa sana hivyo azma ya kukuza vipaji kushindwa kufikiwa.
Bayi alisema kuwa uwekezaji kwenye michezo hususani kwa vijana wadogo wakiwemo wanafunzi ndiyo chimbuko la wanamichezo tofauti na sasa ambapo wachezaji wengi hawajaanzia kwenye shule au vituo vya michezo.
“Wachezaji wote wanaotamba sehemu mbalimbali duniani walianzia kwneye shule au vituo vya michezo hivyo ili na sisi tuweze kufanikiwa lazima tuwekeze kwa watoto ili wakue kwenye michezo na si kuanza kuwafundisha ukubwani lakini tunakwazwa na ushuru mkubwa wa vifaa vya michezo ,” alisema Bayi.
Alisema kuwa wao kama wanamichezo waliamua kuwekeza kwa kujenga viwanja vya kisasa vya michezo yote nab ado wanendelea na ujenzi lakini vifaa vinavyotumiwa na wanamichezo vina ushuru mkubwa ambapo hata baadhi ya wanamichezo wamekuwa wakishiriki peku peku.
“Tunapokwenda kwenye michezo mbalimbali hasa kwenye nchi zilizojuu kimichezo tunaumia sana kwani wenzetu wamewekeza kwa vijana wadogo na mafanikio ya uwekezaji huo yanaonekana kwani wanafanya vizuri sana,” alisema Bayi.
Aidha alisema kuwa fedha wanazotumia kwa ajili ya ujenzi wa viwanja ni mikopo hivyo serikali iangalie namna ya kupunguza ushuru ili waweze kuweka vifaa ambavyo ni vya kisasa ambavyo vitawafanya wachezaji kutoshangaa wanapokwenda kwenye michuano ya kimataifa kwani wataona vifaa hivyo na mazingira ya viwanja ni ya kawaida.
Akijibu suala hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Seif Ali Idd alisema kuwa ataongea na Waziri wa Fedha ili kuangalia namna ya kuwawasidia wanamichezo ili kuwapunguzua gharama kubwa za ushuru wa vifaa hivyo vya michezo.
Makamu wa Rais alimpongeza Filbert Bayi kwa kuanzisha shule ya michezo ambayo itajibu tatizo kubw ala kuandaa vijana kwa ajili ya kuwa wachezaji wazuri watakaorudhisha hadhi ya michezo hapa nchini ikiwemo riadha.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
IMEELEZWA kuwa uwekezaji kwenye sekta ya michezo kwa michezo ya mchezaji mmoja mmoja inaweza kuinua sekta hiyo kwa haraka tofauti na michezo inayoshirikisha wachezaji wengi.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na msiadizi wa mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka, Method Mselewa wakati wa tamasha la mchezo wa Karate lililoandaliwa na klabu ya KAMBOJI ya wilayani Kibaha na kushirikisha wachezaji toka mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani.
Mselewa alisema kuwa wachezaji wanaocheza michezo ya mchezaji mmoja wana uwezo wa kufanya vyema endapo wataandaliwa vizuri kushiriki michezo hiyo kama ilivyo kwa michezo kama ya ngumi, kareti, riadha, tenisi, michezo ya mitupo na michezo mingine ambayo inashirikisha mchezaji mmoja.
“Hatusemi kuwa michezo inayoshirikisha wachezaji wengi haina nafasi ya kufanya vizuri bali kuna haja ya michezo ya mtu mmoja mmoja nayo kupewa nafasi kwani inaonyesha kuwa ndiyo iliyowahi kufanya vema kimataifa,” alisema Mselewa.
Alisema kuwa mfano wa michezo ya ngumi na riadha kwa miaka ya nyuma ilifanya Tanzania itambuliwe duniani ambapo wachezaji wake walifanikiwa kutwaa medali mbalimbali kwenye michuano kama ile ya Jumuiya ya Madola, Olimpiki na michezo ya kimataifa.
“Tunapaswa kueiendeleza michezo yote lakini pia kuwekeza kwenye michezo kama hii itasaidia nchi kuwa kwenye ramani ya michezo ambapo tumeona uwekezaji kwenye michezo ya watu wengi licha ya kusaidiwa lakini bado mafanikio hayajaonekana,” alisema Mselewa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa klabu hiyo ya Kamboji Kachingwe Kaslenge alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutokuwa na ofisi pamoja na sehemu yao binafsi ya kufanyia mazoezi ambapo kwa sasa wanaomba.
Kaselenge alisema kuwa changamoto nyingine ni ukosefu wa vifaa kutoakana na vifaa kuuzwa kwa gharama kubwa hivyo wachezaji wengi kushindwa kuvinunua kutokana na bei kuwa juu ambapo wakati mwingine mchezjai hujikuta na kifaa kimoja kwa ajili ya mazoezi na mashindano.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment