Tuesday, June 9, 2015

HABARI MPYA

Na John Gagarini, Kibaha
ZOEZI la kuandikisha wananchi kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Pwani linatarajiwa kuanza Juni 14 mwaka huu kwa watu wenye sifa wakiwemo wale waliokuwa na umri chini ya miaka 18 wakati zoezi hilo lilipofanyika miaka ya nyuma.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mchambuzi wa mfumo wa kompyuta wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Mariam Rajab alisema kuwa zoezi hilo litadumu kwa kipindi cha siku 28 kwenye maeneo yote ya mkoa huo.
Rajab alisema kuwa zoezi hilo ni kwa watu wote wenye sifa wakiwemo wale wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea ambao ni raia wa kuzaliwa au kuandikishwa kisheria.
“Zoezi hili ni muhimu kwa wananchi hivyo wanapaswa kujitokeza kwa wingi ili waweze kujiandikisha kwa lengo la kupata fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” alisema Rajab.
Alisema kuwa zoezi hili litawahusisha hata wale ambao walijiandikisha kwenye daftari hilo kabla ya uchaguzi mkuu uliopita kwani vitambulisho hivyo havitatumika tena ambapo uchaguzi huu utatumia vitambulisho vipya.
“Tunawashauri wananchi wajitokeze kwa wingi kwenye uandikishaji huu kwani endapo hawataandikishwa watakosa fursa ya kupiga kura ambayo ni haki yao ya msingi,” alisema Rajab.
Aidha alisema Tume imeshaleta vifaa kwa ajili ya zoezi hilo na hakutakuwa na tatizo la vifaa kwa ajili ya kujiandikisha kama ilivyotokea kwa baadhi ya mikoa kuwa na upungufu wa vifaa.
“Changamoto mbalimbali ambazo tulizipata wakati wa zoezi hili kwenye ile mikoa ya awali tayari zimefanyiwa kazi hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi juu ya vifaa kikubwa ni kushiriki kwa wingi,” alisema Rajab.
Alisema kuwa tayari maofisa wa uchaguzi kwenye mkoa huo wameshapatiwa mafunzo kwa ajili ya kutumia mashine zitakazotumika kuandikishia BVR na kinachosubiriwa ni muda kufika.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kisarawe
SHIRIKA la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) limeanzisha mitandao kwa ajili ya ulinzi wa misitu hiyo ili kukabiliana na uharibifu unaofanywa na watu wanaotumia mazao ya misitu kwa ajili ya kujipatia kipato.
Hayo yalisemwa wilayani Kisarawe na mratibu wa shirika hilo Yahaya Mtonda wakati wa sherehe za kuwapa zawadi washindi wa Insha juu ya umuhimu wa misitu zilizoambatana na siku ya mazingira duniani.
Mtonda alisema kuwa TFCG imehamasisha kuanzishwa kwa mitandao ipatayo 93 ijulikanayo kwa kifupi (MJUMITA).
“Mbali ya mitandao hii kulinda misitu hiyo pia tumewawezesha wananchi wanaozunguka misitu hiyo kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa (Vicoba) ili waweze kukopeshana ili kufanya shughuli nyingine za kujiongezea kipato badala ya kutegemea misitu kama chanzo chao cha mapato,” alisema Mtonda.
Mtonda alisema kuwa pia wamewapatia mafunzo walimu wanaofundisha masomo yahusuyo utunzaji wa mazingira ili kuwa na uelewa juu ya masuala ya kuhifadhi mazingira ili wawafundishe wanafunzi wa shule za msingi.
“Tunatoa mafunzo kwa walimu wa shule za msingi ili kuwarithisha wanafunzi tangu wakiwa wadogo waweze kuona umuhimu wa tangu wakiwa wadogo misitu ili waweze kuitunza na kuhamasisha jamii kupanda miti,” alisema Mtonda.
Aidha alisema kuwa lengo la kuwafundisha ni kuwafanya wawe mabalozi wazuri wa kulinda misitu na kutunza mazingira ambayo yamekuwa yakiharibiwa kwa kasi na waharibifu wa mazingira.
Juu ya Insha alisema ilikuwa ni kuataka kujua uelewa wa wanafunzi kutoka shule nane kutoka wilaya za Ilala, Temeke, Kinondoni, Kibaha Mjini, Kibaha Vijijini na Kisarawe ambapo Januari Eric wa Shule Msingi Mtamba alijinyakulia 100,000, Catherine Mbelwa wa Kongowe 70,000 na Prisca Joseph wa Soga 50,000.
Mwisho.  
Na John Gagarini, Kisarawe
WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani unatarajia kubadilisha sehemu ya msitu wa Pugu kuwa sehemu ya Utalii na kuwa hifadhi asilia kutokana na vivutio vilivyopo kwenye msitu huo ambavyo baadhi havipo sehemu yoyote duniani.
Hayo yalisemwa na meneja wa (TFS) wilaya ya Kisarawe Andrew Mwenuo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi wilayani humo.
Mwenuo alisema kuwa kwa sasa tayari wameshaweka baadhi ya maeneo kwa ajili ya watu kupumzika na njia za kutembea kwa miguu na baiskeli ili watu waweze kuutembelea msitu huo na kuona mandhari na vivutio vilivyopo.
“Kuna wanyama wadogo wadogo akiwemo aina ya nyani mwenye aibu kwani amuonapo mtu huficha uso wake kwa aibu na hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani zaidi ya hapa,” alisema Mwenuo.
Alisema kuwa mbali ya nyani huyo pia kuna aina ya tembo mdogo ambao sehemu nyingine hapatikani zaidi ya kwenye msitu huu pia kuna wanyama wengine, ndege, wadudu kama vipepeo na wengine ambao ni vivutio.
“Hii itakuwa fursa kwa Watanzania na raia wan je ambao wanataka kupumzika na kuona mazingira mazuri ya msitu wakiwemo wasafiri wanaotumia njia ya ndege wanaweza kuja hapa na kupumzika wakisubiri muda wa kuondoka kwa njia ya anga kwani ni jirani na uwanja wa ndege,” alisema Mwenuo.
Aidha alisema kuwa watu wataruhusiwa kuweka mahema na kupumzika na kujipumzisha huku wakila vyakula pamoja na vinywaji ambapo kiingilio kitakuwa kwa wageni ni dola 10 huku kwa Watanzania ni 1,500 huku wanafunzi wakitozwa 500.
Mwisho.
  




No comments:

Post a Comment