Sunday, May 31, 2015

PWANI WAANZISHA WILAYA MPYA YA KIBITI NA MAJIMBO MAPYA


Na John Gagarini, Kibaha

MKOA wa Pwani umepitisha mapendekezo ya kugawanywa kwa Wilaya ya Rufiji kuwa wilaya mbili za Rufiji na Kibiti na kuligawa Jimbo la Chalinze kuwa majimbo mawili ya Chalinze na Saadani.

Mbali ya kupitisha wilaya mpya ya Kibiti na Jimbo la Saadani umepitisha mapendekezo yaliyowasilishwa na Halmashauri ya Kibaha Mji ya kugawa Tarafa ya Kibaha na kuwa na  Tarafa mpya ya Kongowe.

Maamuzi hayo yalifanywa mjini Kibaha kwenye Kiko cha Usahauri cha Mkoa (RCC) kilichokaa mwishoni mwa wiki chini ya kaimu mkuu wa mkoa wa Pwani ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Kibaha Halima Kihemba
Kihemba alisema kuwa mapendekezo hayo yamefuata sheria na taratibu zinazostahili kwa upande wa wilaya na Jimbo ni pamoja na Jimbo kuwa ndani ya wilaya moja ama Halmashauri moja, idadi kubwa ya watu ,upatikanaji wa mawasiliano ikiwemo mitandao ya simu, barabara, huduma za kiuchumi na jiografia ya eneo husika.
Naye Mkuu wa wilaya ya Rufiji Nurdin Babu alisema kuwa anpongeza kikao hicho kuweza kupitisha uanzishwaji wa wilaya mpya ya Kibiti kwani itawasogezea huduma mbalimbali za kijamii karibu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga alisema kugawanywa kwa Jimbo la Chalinze ni mchakato wa wilaya ya Bagamoyo kugawanywa katika wilaya mbili

Mwanga alisema kuwa endapo utaratibu huo utakuwa umekamilika wilaya hiyo itakuwa na majimbo matatu ya uchaguzi ambayo ni Bagamoyo,Saadani na Chalinze kutokana na ukubwa wa wilaya hiyo.

Jimbo la Bagamoyo litakuwa na kata za Dunda,Magomeni,Nia Njema ,Kisutu, Makurunge, Kiromo,Zinga ,Kerege, Mapinga, Yombo na Fukayosi ambayo itatolewa kutoka jimbo la Chalinze.

Huku Jimbo la Chalinze likiwa na kata za Vigwaza ambayo imeondolewa katika Jimbo la Bagamoyo, Kiwangwa, Msata, Lugoba,Talawanda, Ubena, Pera, Bwiringu na Msoga na Jimbo jipya la Saadani makao makuu yatakuwa Miono na Jimbo hilo likiwa na kata za Kibindu, Mbwewe, Kimange, Mandela, Miono na Mkange.


Mwisho

No comments:

Post a Comment