Tuesday, May 19, 2015

HABARI MOTOMOTO

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Wasioona Nchini kimewataka vijana wenye ulemavu huo kuachana na dhana ya kuwa mara wamalizapo elimu mbalimbali ni laziwa waajiriwe badala yake wajiandae kwa kufanya shughuli za kujiajiri wenyewe.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na makamu mwenyekiti wa chama hicho Taifa Robert Bundala wakati wa mafunzo ya sera ya ajira kwa watu wenye ulemavu kwa vijana wanachama wa chama hicho wilayani Kibaha.
Bundala alisema kuwa soko la ajira kwa sasa ni gumu sana hivyo lazima vijana wajiwekee malengo ya kujiajiri wao wenyewe kupitia fursa zilizopo kwenye maeneo yao kuliko kusubiri kuajiriwa serikalini au sekta binafsi.
“Vijana wasioona wanapaswa kuachana na dhana hiyo badala yake wajiajiri kwa kupitia shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujasiriamali na si kutegemea kuajiriwa kwani upatikanaji wa ajira kwa sasa ni mgumu,” alisema Bundala.
Alisema kuwa ushindani wa soko la ajira hapa nchini kwa sasa ni mkubwa sana kwani hata watu wasiona na ulemavu wamekuwa wakilalamika hivyo lazima vijana hao watumie mafunzo mbalimbali wanayoyapata ili kujiajiri.
“Kwa sasa ubaguzi umepungua lakini kikubwa kinachoangaliwa ni uwezo wako wa kielimu kwani kwa wale wenye elimu nzuri wamepata ajira lakini lazima wabadili mfumo wa kusubiri ajira badala yake wajiajiri,” alisema Bundala ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi.
Naye Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye naye ni mlemavu asiyeona Greyson Mlanga alisema kuwa ni vema vijana wakaangalia fursa za ajira zilizopo kwenye maeneo wanayoishi na kuwaondolea fikra kuwa lazima waajiriwe.
Mlanga alisema kuwa kutokana na ugumu wa ajira vijana wasioona wanapaswa kuangalia suala la kujiajiri kwani kutegemea ajira za kuajiriwa itakuwa ni vigumu sana kuweza kufanikiwa kujiletea maendeleo.
 Kwa upande wake moja ya washiriki wa mafunzo hayo Zuhura Omary alisema kuwa changamoto kwao ni nyingi kutokana na hali waliyonayo pia ni kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha hivyo kujikuta wakikosa ajira.
Mafunzo hayo yaliwahusisha vijana wasioona wapatao 60 kutoka kata nne za Misugusugu, Visiga, Kibaha na Kongowe na kufadhiliwa na The Foundation for Civil Society
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WANANCHI wametakiwa kuhakikisha wanazingatia matumizi ya dawa za minyoo kila baada ya miezi mitatu ili kuepukana na athari ikiwa ni pamoja na magonjwa ya Kisukari na Presha.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Ofisa afya Mstaafu Allice Bakari alipozungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa minyoo ni chanzo cha magonjwa hayo makubwa ambayo yanasababisha vifo.
Bakari alisema kuwa kutokana na watu kutotumia kabisa dawa za kuua minyoo kumesababisha watu kupata athari kubwa za kiafya kutokana na ulaji wa vyakula ambao husababisha watu kupata minyoo.
“Minyoo ni chanzo cha magonjwa mengi makubwa yakiwemo moyo kutanuka, kuchanganyikiwa, mba na baadhi ya viuongo vya ndani kuathirika na kushindwa kufanya kazi na hatimaye ni kifo,” alisema Bakari.
Alisema kuwa tatizo la minyoo linazidi kuwa kubwa kutokana na baadhi hata ya wahudumu wa afya kuumwa kutokana na kutotumia dawa za minyoo kutokana na kutotambua ukubwa wa tatizo hilo.
“Hata baadhi ya madaktari wameathiriwa na hali hiyo kutokana na kutoona kuwa minyoo ni tatizo lakini ukweli ni kwamba hili ni tatizo kubwa sana na inabidi wahudumu wa afya kulifuatilia kwa umakini ili kuwanusuru watu,” alisema Bakari.
Ofisa afya huyo ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye hospitali ya Tumbi iliyopo wilayani Kibaha alisema kuwa minyoo inapokuwa imekithiri mwilini hushambulia viungo mbalimbali vya ndani ya mwili na kuleta athari hizo.
“Ushauri ni kwamba madaktari wanapaswa kuwa makini kwa kuwashauri wagonjwa kutumia dawa za kuwaua wadudu hao kwa kujua kuwa endapo walishawahi kutumia dawa kwani watu wanafikiri minyoo ni kwa watoto pekee,” alisema Bakari.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
MRADI mkubwa wa Maji wilayani Kibaha mkoani Pwani unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu na kuondoa tatizo la ukosefu wa maji ambapo baadhi ya vitongoji wananchi wameanza kukimbia bili za maji.
Akizungumza na wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa uzinduzi wa matawi ya chamaa hicho Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa mara mradi huo utakapokamilika tatizo hilo itakuwa ni historia.
Koka alisema kuwa mradi huo wa maji ambao chanzo chake ni mto Ruvu utapitia kwenye mitaa yote ya Jimbo hilo ambapo kwa kipindi kirefu wananchi wamekuwa wakilalamika upatikanaji wa maji.
“Tunashukuru kuwa kwenye mradi uliotokea wilaya ya Bagamoyo baadhi ya mitaa ikiwemo ya Vikawe, Vikawe shule maji yanapatikana kwa wingi ambapo sasa watu wanakimbia bili kutokanana kushindwa kulipa kwani awali walikuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji,” alisema Koka.
Alisema kwa sasa maji yamesambazwa kwenye mitaa 14 na mara mradi huo utakapokamilika wakazi wa Kibaha hawatanyanganyana maji na Jiji la Dar es Salaam ambao wanategemea chanzo kimoja hivyo maji kuwa ya mgao.
“Nawaomba msiwe na wasiwasi kwani mradi huo unaendelea vizuri ambapo kwa sasa wanatandaza mabomba ambayo kwa sasa yamefika eneo la Kongowe kilometa 10 kutoka hapa mjini hivyo Mungu akipenda wakati huo uliotajwa maji yatapatikana,” alisema Koka.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WANAWAKE wajawazito wilayani Kibaha mkoani Pwani wametakiwa kuacha kutumia dawa za kienyeji za kuongeza uchungu ili kupunguza vifo vya watoto wachanga.
Hayo yalisemwa na ofisa muuguzi wa kituo cha afya cha Mkoani, Prisca Nyambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea kituo hicho hivi karibuni na kusema kuwa dawa hizo zianasababisha watoto kufia tumboni.
Nyambo alisema kuwa dawa hizo za kuongeza uchungu za kienyeji ni mbaya kwa watoto waliotumboni kwani wengi wamekuwa wakipoteza maisha.
“Tatizo la watoto kufia tumboni kwa sasa ni kubwa kutokana na wajawazito kutumia dawa hizo ili waweze kujifungua endapo muda umefika na hakuna dalili za kufanya hivyo,” alisema Nyambo.
Alisema kuwa wajawazito wanapaswa kwenda hospitali wanapoona muda wa kujifungua umefika lakini hawajifungui kuliko kutumia dawa hizo ambazo zinasabisha vifo vya watoto.
Aidha alisema vifo vya watoto wachanga ni kati ya saba na tisa kwa kila mwezi kutokana na sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni matumizi ya dawa hizo za kienyeji za kuongeza uchungu ambapo wastani wa wanawake wanaojifungua kwa kipindi hicho ni zaidi ya 300.
Alibainisha kuwa akinamama wajawazito wanaokwenda kujifungua hapo ni wengi kwani baadhi yao wanatoka maeneo ya Jiji la Dar es Salaam kama vile Mbezi, Kibamba, Kimara na Ilala kutokana na ukaribu.
Mwisho.




   

    

No comments:

Post a Comment