Tuesday, July 28, 2015

LIGI NETBALL PWANI KUFANYIKA AGOSTI 3 MWAKA HUU

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA Cha Mpira wa Pete mkoani Pwani kinatarajia kufanya mashindano ya mchezo huo Agosti 3 mwaka huu ili kupata timu itakayopanda ligi daraja la pili Taifa itakayowakilisha mkoa huo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha mwenyekiti wa chama hicho Fatuma Mgeni alisema kuwa jumla ya timu 14 zitachuana kwenye michuano hiyo itakayofanyika kwenye uwanja wa Bwawani maili Moja Kibaha.
Mgeni alisema kuwa wanatarajia kila wilaya itatoa timu mbili ili mashindano yawe na uhalisia wa mkoa kwa kushirikisha timu za wilaya hizo.
“Tayari tumeshawapa taarifa wilaya zote waandae timu ili ikifika wakati walete timu zao ziweze kuwakalisha wilaya zao nah ii ni moja ya kuhamasisha mchezo huo maeneo mbalimbali ya mkoa,” alisema Mgeni.
Alisema kuwa awali mashindano hayo yalikuwa yafanyike Julai 10 mwaka huu lakini kutokana na sababu ambazo zilishindwa kuzuilika ilibidi mashindano hayo yasogezwe mbele.
“Maandalizi yako vizuri na tayari timu zimeshaplekewa taarifa za kushiriki mashindano hayo ambayo yatapandisha timu moja kwenda daraja la pili Taifa japo kuna uwezekano wa kupandisha timu mbili ila hilo bado halijawa wazi sana,” alisema Mgeni.
Aidha alizitaka timu zinazotarajiwa kushiriki michuano hiyo kujiandaa kikamilifu ili kushirikia michuano hiyo ili mkoa uweze kupata timu nzuri.
Mwisho.

     

No comments:

Post a Comment