Thursday, July 30, 2015

HABARI ZA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
MGOMBEA Ubunge anayewania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye Jimbo la Kibaha Mjini Abdulaziz Jad Maarufu kama Mwarabu amesema kuwa wana CCM wasichague mbunge ambaye ni sawa na mfadhili kwani atakwamisha shughuli za maendeleo katika Jimbo hilo.
Jad aliyasema hayo juzi mjini Kibaha kwenye mkutano wa wagombea wa ubunge wa CCM kuomba kura kwenye kata ya Maili Moja na kusema kuwa baadhi ya wabunge ni sawa na wafadhili ambao hutoa misaada kwa msimu.
Alisema kuwa wabunge wa namna hiyo hujitokeza wakati wa vipindi vya uchaguzi lakini wakishachaguliwa na uchaguzi ukipita hawaonekani tena kwani maendeleo yake yatakuwa ya msimu na si endelevu.
“Sisi wakazi wa Jimbo la Kibaha tunahitaji Mbunge wa kutuletea maendeleo na si mfadhili ambaye anatoa misaada kwa msimu hasa ule wa uchaguzi na mkishamchagua hamuoni tena hadi baada ya miaka mitano,” alisema Jad.
Aidha alisema kuwa wabunge wa namna hiyo wanaleta maendeleo ya msimu lakini endapo watamchagua yeye atawaletea maendeleo endelevu na si ya msimu kama wanavyofanya baadhi ya wafadhili.
“Baadhi yao ni wafadhili lakini wanavaa kofia ya uongozi hawa hawatufai lakini mkinichagua mimi nitawaletea maendeleo enedelevu na si yale ya msimu ambayo yametudumaza,” alisema Jad.
Alibainisha kuwa endapo ilani ya chama itatekelezwa kwa ufanisi basi maendeleo yatapatikana kwani inajibu changamoto zilizopo kwenye sekta zote za maendeleo pia aliahidi kuondoa makundi yaliyojitokeza katika kipindi hichi cha uchaguzi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Bagamoyo
SERIKALI imeombwa kuajiri watu wenye taaluma ya sheria kwenye mabaraza ya ardhi ili kupunguza migogoro ya ardhi iliyopo kwenye maeneo mengi ya miji na vijiji.
Hayo yalisemwa Bagamoyo na Raya Fereji makamu mwenyekiti wa asasi isiyo ya kiserikali ya Mkombozi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati wa mafunzo ya sheria ya ardhi kwa waandishi wa habari na wadau wa ardhi wilayani humo.
Fereji alisema kuwa mabaraza ya ardhi yanaendeshwa na watu wasiokuwa na taaluma ya sheria wakati masuala yenyewe ni ya kisheria hali ambayo inasababisha migogoro ishindwe kwisha.
“Mabaraza haya yanaundwa na watu maarufu kwenye maeneo yao lakini hawana taaluma ya kisheria licha ya kuwa utatuzi wa migogoro ya ardhi unakwenda kisheria,” alisema Fereji.
Alisema kuwa ili migogoro hiyo ipungue hakuna budi kuwatumia watu wenye taaluma ya sheria ili kukabiliana na migogoro hiyo am,bayo imekithiri.
“Hata kama itashindwa kuwatumia watu wenye taaluma hiyo basi iyapatie mafunzo ya sheria mabaraza hayo kwani uzoefu unaonyesha kuwa maamuzi mengi yanayotolewa ya utatuzi wa migogoro ya ardhi inakuwa na kasoro nyingi,” alisema Fereji.
Kwa upande wake mwanasheria wa Kujitegemea Boka Lyamuya alisema kuwa migogoro mingi ya ardhi inashindwa kutatuliwa kutokana na baadhi ya watendaji  kwenye maeneo hayo kupindisha sheria.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
WAGOMBEA wa nafasi za Ubunge na Udiwani mkoani Pwani wametakiwa kuweka ajenda ya kuhifadhi misitu kama sehemu ya kampeni zao za kuomba nafasi za uongozi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ofisa Mradi wa  Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) Yahaya Mtonda alisema kuwa misitu hiyo endapo itaundiwa sera nzuri itasaidia kurejesha uoto wa asili ambao umetoweka kutokana na uharibifu wa mazingira.
Mtonda alisema kuwa misitu hiyo imekuwa ni chanzo kikuu cha upatikanaji wa mvua pamoja na hali ya hewa nzuri pia kukabiliana na mmomonyoko wa ardhi hivyo wawania nafasi za uongozi lazima watoe kipaumbele cha jinsi gani ya kukabiliana na hali hiyo ya uharibifu wa mazingira.
“Mabadiliko ya tabianchi  yanatokana na uharibifu wa misitu hivyo wawania nafasi za uongozi lazima wabebe suala hilo kama ajenda muhimu wanaponadi sera zao ili kuokoa misitu ya asili na ile isiyo ya asili,” alisema Mtonda.
Aidha alisema kuwa moja ya misitu ya asili hasa ile iliyojirani na Jiji la Dar es Salaam ambayo ni Kazimzumbwi na msitu wa Pugu iliyopo wilayani Kisarawe ni muhimu kwani ndiyo inayochuja hali ya hewa na kuifanya iwe nzuri.
“Kama mnavyofahamu Jiji la Dar es Salaam lina zalisha hewa mbaya kutokana na magari, viwanda na shughuli mbalimbali za kimaendeleo hivyo misitu hii ni kama mapafu ya kupumulia hivyo kutufanya tupate hewa nzuri lakini endapo isingekuwepo basi athari za kiafya zingekuwa kubwa sana,” alisema Mtonda.
Aliwataka wananchi kuwauliza wagombea kuwa wameweka mikakati gani ya kuhifadhi misitu na utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na uvunaji holela wa misitu kwenye mkoa huo.
Mwisho.   
  Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI wa Kijiji cha Minazimikinda kata ya Ruvu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani wamemwomba Waziri wa Ardhi na Makazi Wliam Lukuvi kutembelea Kijiji chao ili kukabiliana na mgogoro wa muda mrefu baina yao na Kijiji cha Kwala.
Moja ya wakazi wa Kijiji hicho Mohamed Palu alisema kuwa mgogoro huo ni wa muda mrefu na umekuwa ukiwachukulia muda mrefu kuutatua bila ya mafanikio hivyo kushindwa kufanya shughuli za maendeleo.
Palu alisema kuwa mgogoro huo umesababisha shughuli za kimaendeleo katika eneo hilo kukwama kutokana na kila upande kudai eneo hilo ni la upande mwingine.
“Tumetumia njia nyingi za kusuluhisha mgogoro huu lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizofikiwa kuumaliza mgogoro huo hivyo tunaona endapo waziri atakuja anaweza kuutatua,” alisema Palu.
Alisema kuwa kamati ya Bunge inayoshughulikia migogoro ya ardhi ilifika Kijijini hapo mwezi Machi mwaka huu lakini hadi sasa hakuna taarifa yoyote juu ya suluhu ya mgogoro huo.
“Mgogoro huu na mingine iliyopo Kijijini ni moja ya changamoto kubwa zinazotukabili hivyo endapo waziri atakuja atatusaidia kuitatua na hivyo itasaidia wananchi kuendelea na shughuli za maendeleo,” alisema Palu.
Aidha alisema kuwa baadhi ya viongozi wa Vijiji wamekuwa wakichangia migogoro hiyo kutokana na kutozingatia ramani za vijiji hivyo hali inayosababisha kuwa na migogoro hiyo.

 Baadhi ya wanachama wa CCM kata ya Maili Moja wakiwasikiliza watia nia wa CCM walipokuwa wakimwaga sera jana mjini Maili Moja
Mwisho.    
Wawania nafasi ya Ubunge kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kibaha Mjini mkoani Pwani kuanzia kushoto Rashid Bagdela Iddi Majuto, Abdulaziz Jad, Silvestry Koka na Rutatina Rugemalila

No comments:

Post a Comment