Monday, August 10, 2015

HABARI ZA PWANI


Na John Gagarini, Bagamoyo
KATIKA kukabiliana na changamoto ya huduma ya afya kwa wananchi wa kijiji cha Kidomole Kata ya Fukayosi, wilaya ya Bagamoyo, mkoa wa Pwani, wamejenga zahanati kwa thamani ya 58.7
Akizungumzia kuhusu ujenzi huo ofisa mtendaji wa Kijiji hicho Sef Mayala alisema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo unaondoa adha ya kufuata huduma ya afya nje ya kijiji hicho.
Mayala alisema kuwa katika kufanikisha ujenzi huo kila mwananchi wa Kijiji hicho alitoa kiasi cha shilingi 5,000 kabla ya kuungwa mkono na wadau wengine na kufanikiwa kukamilisha ujenzi huo.
“Mradi huu wa ujenzi wa zahanati uliibuliwa na wananchi kupitia mkutano ulioitishwa na uongozi wa serikali ya kijiji ambao ulianza mwaka 2009 na kukamilika mwaka huu 2015,” alisema Mayala.
Alisema kuwa kuwa katika kuhakikisha ujenzi wa zahanati hiyo unakamilika kwa wakati Halmashauri kupitia ruzuku ya maendeleo ya serikali ilichangia pia kwenye ujenzi huo.
“Ujenzi wa zahanati hii umetokana na utekelezaji wa sera ya afya ya kijiji kuwa na zahanati na pia kuwepo kwa ongezeko la watu katika kijiji cha Kidomole na uhitaji mkubwa wa huduma za afya,,” alisema Mayala.
Aidha alisema kwenye ujenzi huo nguvu za wananchi wamechangia kiasi cha shilingi milioni 45.9, wadau mbalimbali shilingi. milioni 2.8, ruzuku ya serikali shilingi milioni 10 huku Mbunge jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akichangia bati 129.
Diwani wa kata ya Fukayosi Ally Issa aliwashukuiru wananchi wa kijiji hicho na Kata kwa ujumla kwa kuwa na mwamko wa kimaendeleo kwa kuchangia ujenzi wa zahanati hiyo hadi kukamilika.
Issa alisema kuwa anawashukuru wananchi kwa kujitolea pia kwani niaba ya viongozi ngazi mbalimbali anawashukuru kwa michango yao ya hali na mali kwa kujitolea kwa ajili ya shughuli za maendeleo kwenye Kijiji na kata kwani zahanati hiyo ni faida kwa wanancho wote.
Mwisho 
Na John Gagarini, Kibaha
WAUMINI wa Kanisa la Angikana na Watanzania kwa ujumla wametakiwa kutunza vitambulisho vyao vya kupigia kura ili waweze kushiriki kikamilifu zoezi la upigaji kura kwa ajili ya kuwapata viongozi mbalimbali akiwemo Rais atakayeongoza Taifa letu kwa amani na utulivu.
Aidha kanisa linaamini kuwa kutokana na baadhi ya watu kufunga kwa ajili ya kuombea uchaguzi huo kuwa wa amani ni dhahiri Watanzania wasiwe na wasiwasi wakati wa uchaguzi kikubwa ni kuepukana na watu wanaohamasisha uvunjifu wa amani.
 Hayo yalisemwa na Mchungaji wa Kanisa la  Anglikana Tumbi wilayani Kibaha Mkoani Pwani Methew Mwela kwenye baraza  la Halmashauri  kuu ya kanisa hilo lililoketi kwaajili ya kujadili maswala ya maendeleo ya Kanisa hilo na waumini  wake ambapo alisema kuwa kinachotakiwa kufanywa na waumini hao ni kutunza  vitambulisho vyao vya mpiga kura na kushiriki zoezi hilo kikamilifu siku itakapofika.
"Nawakumbusheni waumini na Watanzania kwamba dhambi ya manung'uniko ni mbaya sana na hata kwenye vitabu vitakatifu imeandikwa kuwa iliwatafuna wana wa Israel hivyo kama mtakaa bila kwenda kupiga kura kisha akachaguliwa kiongozi  ambaye hamkupenda achaguliwe na mkaanza kunung'unika mtakuwa mnajitafutia dhambi,"alisema Mch Mwela.
Mch Mwela alisema kuwa wanachopaswa kufanya hivi sasa waumini hao ni kutunza vitambulisho vyao vya mpiga kura na siku ikifika wafike mapema kwaajili ya kupiga kura na kwamba ili kuwawezesha waumini wake kushiriki kikamilifu ibada ya siku hiyo itaanza mapema na kuisha mapema .
"Ili kuhakikisha wote mnapata haki yenu ya msingi  ya kupiga kura ibada ya tarehe hiyo ya siku ya uchaguzi itaanza mapema hapa kanisani kwetu ili waumini wangu wote wenye kadi ya mpiga kura aende akapige kura ili kuchagua viongozi anaowapenda kadri Mungu atakavyomuonyesha,”alisema Mch Mwela.

Aliwashauri waleambao kwa bahati mbaya ama kwa sababu mbalimbali walishindwa kufanikiwa kupata kadi za mpiga kura kuwa watulivu na wanayopaswa kufanya ni kumuomba Mungu ili viongozi watakaochaguliwa waiongoze nchi kwa haki na kweli pasipo na upendeleo wa aina yoyote ili taifa liendelee kuwa na amani.

“Nawaomba Watanzania kuondoa hofu na mashaka juu ya kuwepo na uwezekano wa kuzuka vurugu kabla na baada ya uchaguzi huo mkuu nchini kwani wanachopaswa kutambua ni kuwa mungu amesha mchagua Rais atakayewaongoza watu wake,” alisema Mch Mwela.

MWISHO

Na John Gagarini, Kibaha

ABIRIA wanaosafiri kutumia vyombo mbalimbali vya vya moto mkoani Pwani wametakiwa kuacha tabia kuwashabikia madereva wanaoendesha mwendo wa kasi wakati wakisafiri kwani ni hatari kwa maisha ya wasafiri.

Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na mgeni rasmi kwenye kilele cha wiki nenda kwa usalama barabarani kimkoaFlorence Mwenda iliyofanyika mjini Kibaha na kusema kuwa kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa na Jeshi hilo kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua bado kuna changamoto mbalimbali hususa kwa  upande wa abiria ikiwemo kuhamasisha madereva kwenda na mwendo kasi wakiwa safarini.
Mwenda ambaye ni ofisa wa jeshi la polisi alisema kuwa kikosi cha usalama barabarani kimeendelea kutoa elimu kwa watumiaji wa barabara juu ya matumizi sahihi ya barabara lakini kumekuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya abiria kushangilia mwendo wa kasi.

“Vitendo kama hivi na vingine havipaswi kufumbiwa macho kwani vinahatarisha usalama wa abiria pamoja na uharibifu wa mali lakini endapo madereva watazingatia matumizi sahihi ya barabara itasaidia kupunguza ajali ambazo zimekuwa ni moja ya vyanzo vikuu vya vifo pamoja na ulemavu,” alisema Mwenda.

Aidha alisema kuwa kikosi cha usalama barabarani kimetoa  elimu ya matumizi sahihi ya   barabara  kwa wanafunzi  wa shule za msingi na sekondari  mkoani humo wapatao 1,568 lengo likiwa ni kuielimisha jamii na makundi mbalimbali   juu ya matumizi salama ya barabara ili kupunguza ajali zisizokuwa za lazima.

“Makundi mbalimbali yamepatiwa elimu hiyo ikiwa ni pamoja na madereva wa magari wapatao 905,waendesha pikipiki1,220 na abiria 16,802 wa magari  ya aina mbalimbali ambapo zoezi hilo litakuwa endelevu  hali itakayosaidia  kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikigharimu maisha na mali,” alisema Mwenda.

Alibainisha kuwa kamati ya usalama barabarani  ya Mkoa huo pia ilifanya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma ya  upimaji wa macho bure kwa wananchi wa kawaida na madereva wa vyombo vya moto.

MWISHO











No comments:

Post a Comment