> Na
John Gagarini, Kibaha
UJENZI wa madarasa manne kwenye shule ya msingi Maili Moja
umeanza ambapo kwa sasa wanafunzi 200 wanasoma kwenye darasa moja kutokana na
baadhi ya madarasa kushindwa kutumika kutokana na kuwa mabovu hivyo kuhatarisha
usalama wa wanafunzi.
Shule hiyo ambayo ndiyo shule ya kwanza kujengwa kwenye mji
wa Kibaha kwenye miaka ya 70 madarasa yake yamebomoka na baadhi yameanguka
kutokana na kutumika kwa muda mrefu sasa kwani yamefikisha umri wa miaka 40
sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari shuleni hapo mwalimu mkuu
wa shule hiyo Reginald Fanuel alisema kuwa ujenzi huo ambao ambao utaanza na
madarasa mawili tayari ujenzi umefikia hatua ya msingi na unatarajiwa
kukamilika baada ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Fanuel alisema kuwa fedha zilizotumika kujenga msingi huo wa
madarasa manne ni michango ya wazazi na wadau mbalimbali huku wakisubiria kutoa
fedha ambazo ziko benki kiasi cha shilingi milioni 36 zilizotolewa na
Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambazo ndiyo zitakamilisha ujenzi wa madarasa hayo
mawili
“Kwa kweli hali ni mbaya kwa sasa kwani darasa moja
linachukua wanafunzi 200 tofauti na wastani wa wanafunzi 45 kwa darasa moja
lakini kutokana na ubovu madarasa imebidi mengine yasitumike kutokana na
kubomoka na yanaweza kuanguka hivyo usalama wa wanafunzi na walimu kuwa mdogo,”
alisema Fanuel.
Alisema kuwa shule hiyo ina jumla ya madarasa 14 lakini
mazima ni manne tu ndiyo yenye unafuu kidogo licha ya kuwa si mazima huku
mawili ndiyo mazima na yako imara na yanafaa kwa matumizi ya kufundishia.
“Ujenzi ulisimama kidogo kutokana na kukosekana vitabu vya
hundi kutoka benki hivyo kushindwa kuwalipa wazabuni na wakandarasi na
tulitumia muda mrefu zaidi ya mwezi mmoja kupata vitabu hivyo kwani akaunti ya
shule ilikufa hivyo tukaanza kuifufua upya hali iliyotumia muda mrefu
kufunguliwa lakini kwa sasa zoezi hilo limekamilika na wataanza kulipwa ili
ujenzi uendelee,” alisema Fanuel.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo
Lusanda Wiliam alisema kuwa michango iliyochangwa ni mizuri kwani walitoa
mifuko 250 ya saruji ambayo iilifyatuliwa tofali zaidi ya 585 na mifuko 50
ilitumika kwa ajili ya msingi uliojengwa.
Wiliam alisema kuwa wazazi ambao watoto wao wanasoma shuleni
hapo walitakiwa kulipia shilingi 5,000 kila mmoja kwa ajili ya ujenzi huo na
walifanikiwa kupata kiasi cha shilingi 500,000 na kuwaomba wadau wengine
wajitokeze kuchangia ujenzi huo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment