Na John Gagarini,
Kibaha
WAWEZESHAJI wa mradi
wa kutoa ajira za muda kwa kaya maskini kwenye Halmashauri ya wilaya ya Kibaha
mkoani Pwani kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini (TASAF) wametakiwa
kutowapangia miradi kwa utashi wao bali wao wabaki kama washauri tu.
Hayo yalisemwa mjini
Kibaha na mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha Tatu Suleiman wakati
akifungua mafunzo kwa wawezeshaji wa mradi huo awamu ya tatu na kusema kuwa
wananchi ndiyo wenye kufahamu wanahitaji mradi gani.
Seleman alisema kuwa waratibu
hao kazi yao ni kutoa ushauri kwa wananchi wanapobainisha mradi wanaoutaka
kwani wanaopata changamoto ni wao na si kuelekezwa na wawezeshaji hao ila wao
wanatakiwa kushauri namna ya kutekeleza miradi hiyo.
“Nyie ni wataalamu
mnapaswa kuwapa ushauri wananchi ili wafanikishe miradi hiyo lakini siyo
kuwapangia kuwa wafanye mradi gani kwani wao ndiyo wanaojua mahitaji yao lengo
likiwa ni wao kutatua changamoto zinazowakabili,” alisema Suleiman.
Alisema kuwa
utekelezaji wa miradi ya kunusuru kaya maskini umefikia hatua nzuri ambapo kaya
maskini za vijijini zimeweza kuongeza kipato na kuzifanya zisiwe kwenye hali ngumu
wakati wa kaipindi cha Hari ambacho kinakuwa baada ya muda wa mavuno kupita.
“Tumeona akaya nyingi
sasa zimeweza kupita mwaka mzima zikiwa bado na hali nzuri ya chakula kwani kwa
kipindi cha nyuma zilikuwa zinaishiwa chakula kutokana na kuuza chakula ili
kupata kipato cha kujikimu,” alisema Suleiman.
Awali mwakilishi wa
mkurugenzi mkuu wa TASAF Mercy Mandawa alisema kuwa mradi huo wa awamu ya tatu
emelenga kaya maskini zenye hali duni kwa lengo la kuongeza kipato kwenye
mamlaka za serikali 161 nchini.
Mandawa ambaye ni
Mtaalamu wa Mafunzo na Ushirikishaji wa Jamii TASAF makao makuu alisema kuwa
hadi sasa miradi hiyo imeweza kuzifikia kaya milioni moja kote nchini tangu kuanzishwa
mpango wa kuzisaidia kaya maskini mwaka 2012 ambayo ilizinduliwa na Rais Dk
Jakaya Kikwete.
“Lengo la mradi huu ni
kuhakikisha kaya maskini zinakuwa na kipato cha kuweza kujikimu kwa kuwapa
ajira za muda ambapo mafanikio yameonekana kwani zimeweza kuwa na kipato na
kuondokana na umaskini,” alisema Mandawa.
Aidha alisema kuwa Halmashauri
zinatakiwa kuhakikisha zinapeleka fedha kwa wakati ili kuondoa malalamiko kwa
walengwa ambapo kulikuwa na tatizo la ucheleweshaji wa utoaji wa fedha za
ruzuku kwa kaya maskini.
Mradi huo kwa wilaya
ya Kibaha utazifikia kaya 5,690 kwenye miradi ya kuhifadhi maji ya mvua,
hifadhi ya misitu, miradi midogo midogo ya umwagiliaji, kilimo misitu cha
kuchanganya mazao na miti, usafi wa mazingira maeneo ya mjini (uzoaji wa taka ngumu), mafunzo hayo
yamewahusisha wawezeshaji 24.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment