Thursday, August 20, 2015

HABARI MBALIMBALI ZA PWANI

Na John Gagarini, Kibaha
UMOJA wa Wafanyakazi wa Viwanda na Biashara Tanzania (TUICO) kimewataka wanachama wake kukitumia chama chao ili kujileta maendeleo.
Hayo yalisemwa hivi karibuni mjini Kibaha na mwenyekiti wa chama hicho Betty Msimbe mara baada ya uchaguzi wa chama hicho ambapo alifanikiwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho
Msimbe alisema kuwa baada ya kupata nafasi hiyo ya kukiongoza chama hicho atahakikisha kuwa wanachama wanapata maendeleo kwa kutumia chama chao ambacho kina lengo la kuwaletea umoja na kutetea haki zao.
“Malengo yangu ni kuongeza wingi wa wanachama, kutetea haki za wafanyakazi kuhakikisha mkoa unavuka malengo yake ya kazi, haki na maslahi ya wafanyakazi sehemu za kazi,” alisema Msimbe.
Alisema kuwa atafanya mafunzo maeneo ya kazi ili wafanyakazi wapate elimu juu ya haki zao na elimu kwa viongozi wa matawi kuhusu kutetea maslahi ya wafanyakazi ili waweze kuboresha utendaji kazi wao.
“Kikubwa ninachokiomba toka kwa wanachama na viongozi wenzangu ni ushirikiano ambao utasaidia kukipeleka mbele chama na kufikia malengo ya kuhakikisha haki za wafanyakazi zinapatikana,” alisema Msimbe.
Naye Naibu Katibu Mkuu Msaidizi sekta ya biashara TUICO Taifa Peles Jonathan alisema kuwa atahakikisha anasimamia haki na maslahi ya wafanyakazi kwa nchi nzima na kufanya umoja huo kuwa na demokrasia ya uwakilishi wa kulinda na kutetea haki za wanachama.
Jonatahan alitoa wito  kwa sekretarieti kufanya kazi kwa pamoja ili chama kiweze kufikia malengo waliyojiwekea ili kuwaunganisha kwa pmoja wafanyakazi ili waweze kuwajibika vizuri.
Katika uchaguzi huo ambao ulisimamiwa na katibu wa chama hicho Kassim Matewele ambaye alimtangaza Msimbe kuwa mshindi kwa kura (41) ambaye alimshinda Abimelick Magoma aliyepata kura (18).
Kwenye nafasi ya wajumbe wa kamati ya utendaji mkoa nafasi mbili nafasi ya  Viwanda ni Hasan Kindagule aliyepata kura (35) na Msaidizi wake Athuman Makonga kura (22), upande wa Biashara Shukuru Goso aliyepata kura (32) na msaidizi wake Joyce Kalumuna kura (29).
Kwa upande wa Fedha Furaha Mbwambo  alishinda kwa kupata kura (45) na msaidizi wake ni Zaituni Mtoro aliyepata kura (41), Huduma na ushauri mshindi alikuwa ni Tumaini Kivuyo na msaidizi wake Kandrid Ngowi ambaye alipata kura (35).
Waliochaguliwa Mkutano Mkuu Kanda, Viwanda ni Masiku Serungwi aliyepata kura (35), biashara ni Kamatanda Kamatanda aliyepata kura (57), Fedha Furaha Mbwambo aliyepata kura (60), kwa upande wa huduma na ushauri mshindi alikuwa ni Kandrid Ngowi aliyepata kura (40).
Wajumbe wa mkutano mkuu Taifa upande wa Viwanda  mshindi ni Athuman Makonga kura (59), Biashara ni Shukuru Ngoso kura (58), Fedha Zaituni Mtoro kura (57) na huduma na Ushauri Margareth Chaleo kura ( 45).
Mwisho.

Na John Gagarini, Mkuranga

KIJIJI cha Mwanambaya Kata Mipeko wilaya ya Mkuranga kimewaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kuwasaidia kupata kiasi cha  milioni 150 kwa ajili ya mradi wa kuvuta maji kutoka kijiji jirani cha Kisemvule.

Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa kijiji hicho Abubakar Sisaga alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya maji hivyo wameanza mchakato wa kuvuta maji kutoka kijiji cha Kisemvule.

Sisaga alisema kuwa awali walikuwana wazo la kuchimba visima lakini kutokana na uwezo kutokana na gharama za uchimbaji kisima kuwa ni kubwa.

“Tunawaomba wadau mbalimbali wa maendeleo wajitokeze kutusaidia tufanikishe zoezi hilo la uvutaji maji ili kukabiliana na changamoto hiyo ya ukosefu wa maji kwani kwa sasa wanatumia maji ya visima vifupi ambavyo kipindi cha kiangazi hukauka,” alisema Sisaga.

Alisema kuwa endapo watafanikiwa kupata maji yatawasaidia kuweza kutumia muda wao kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo tofauti na sasa wanatumia muda mwingi kuhangaika na maji jambo ambalo ni changamoto kubwa.

“Mbali ya changamoto ya maji kijiji kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni za kawaida lakini wanakijiji wanajitahidi kuzitatua kadiri ya uwezo wao hivyo tunaomba wadau mbalimbali wajitokeze kutuunga mkono kwenye jitihada zetu za kuleta maendeleo,” alisema Sisaga.

Aidha alisema kuwa wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kwa pamoja waweze kufanikiwa na kujikwamua na hali duni na kujiletea maendeleo.

Naye Mwenyekiti wa kijiji hicho Leyla Chabruma alisema kuwa wana ushirikiano mkubwa na wadau wa maendeleo ambao wanashirikiana na wananchi kwa ujumla hali inayoleta maendeleo ndani ya kijiji hicho ambacho kinategemea mapato yake kwa mauzo ya bidhaa mbalimbali ikiwemo mashamba, viwanja na vitu mbalimbali.

MWISHO.

Na John Gagarini, Kibaha

BAADHI ya wafanyabiashara na wasafiri wanaotumia kituo cha mabasi cha Maili Moja wameiomba Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani kuhakikisha wanatatua tatizo la taa kutowaka kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na kuwasababishia usumbufu mkubwa wataumiaji wa stendi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari moja ya wafanyabiashara wanaofanya biashara kwenye stendi hiyo nyakati za usiku Said Pengo alisema kuwa wamekuwa wakifanya biashara kwenye mazingira magumu kwenye eneo hilo.

Pengo alisema kuwa ukosefu wa taa hapo stendi ni changamoto kubwa sana inayowafanya kushindwa kufanya biashara kwa vizuri kutokana na kuzingirwa na giza.

“Tunaiomba Halmashauri yetu itusaidie tuweze kupatiwa huduma ya taa kwani taizo la ukosefu wa taa linatusababishia usumbufu mkubwa na tunashindwa kufanya biashara zetu kwa uhuru kutokana na giza linalokuwa linatanda,” alisema Pengo.

Alisema kuwa ni hatari kwa hali ya usalama wao pamoja na wateja wanaotumia eneo hili la stendi ya Maili Moja ambayo inatumiwa na watu wengi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Maili Moja Chichi Mkongota alikiri juu ya ukosefu wa umeme kwa kipindi hicho na kusema tayari alishatoa taarifa kwa mamlaka husika juu ya tatizo hilo.

Mkongota alisema kuwa alipotoa taarifa Halmashauri aliambiwa kuwa wanafanya utaratibu wa kutatua tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kupata taa za muda ili kukabiliana na tatizo hilo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Jenifa Omolo alisema kuwa tatizo lililopo ni kubwa kidogo kwani taa zilizowekwa zimeharibika na wanafanya mchakato wa kupata nyingine.

Omolo alisema taa zote 16 zilizopo hapo stendi zimeharibika ambapo gharama zake pamoja na kufungwa ni kiasi cha shilingi milioni 18 ambazo wanazitafuta kwa ajili ya kuzifunga.

“Tunafikiria kwa sasa tufunge taa za kawaida kwani hizo zilizopo ziliharibika na si mara ya kwanza kuzifunga kwani kila wakati zimekuwa zikiharibika,” alisema Omolo.

Aidha alisema kuwa wanahangaika kutafuta fedha hizo ili kuondoa changamoto hiyo ambayo imekuwa kero hata kwa wakala wanaokusanya ushuru wa stendi kutokana na usalama kuwa mdogo.

Mwisho.







No comments:

Post a Comment