Monday, August 10, 2015

CCM WATAKIWA KUACHA MAKUNDI

 Na John Gagarini, Kibaha
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kibaha Mjini wametakiwa kuacha tabia ya kukumbatia makundi mara baada ya uchaguzi wa ndani kumalizika kwani yanasababisha chama kushinda kwa tochi.
Hayo yalisemwa juzi na mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Maulid Bundala wakati akiwanadi watia nia waliojitokeza kuwania kuchaguliwa na chama hicho kupeperusha bendera kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Bundala alisema kuwa makundi hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa chama kushindwa kutokana na mshikamano na ushirikiano kutokuwepo kwenye chaguzi mbalimbali ambazo zinahusisha vyama vingi vya siasa.
“Kipindi hichi ni kigumu sana kuwa na kundi siyo tatizo lakini mara atakapopatikana mgombea mmoja wa ubunge makundi yanatakiwa kwisha na kubakia kundi moja tu la CCM ambalo linatakiwa lipambane na wapinzani,” alisema Bundala.
Alisema kuwa kwanini chama kishindwe kwa mbinde kwa ushindi wa tochi wakati kina wanachama wengi ukilinganisha na vyama vya upinzani lakini inaonekana kushindwa kunatokana na kukumbatiwa kwa makundi hayo.
“Makundi yanatakiwa yaishe mara uteuzi wa mwanachama mmoja ambaye atawakilisha chama kwenye uchaguzi tatizo linguine ni wanachama kumpenda mtu badala ya kukipenda chama na kuachana na tabia ya kuwasema vibaya wagombea kwani wote ni Wanaccm,” alisema Bundala.
Aliwataka wanaccm ambao wanasifa ya kupiga kura za maoni za kuchagua mbunge kwenye kura za maoni wanapaswa kuwa hai kwa kulipia kadi za chama, wawe wameorodheshwa kwenye daftari la tawi na wawe na kadi ya kupigia kura.

Mwisho.   

No comments:

Post a Comment