Na John Gagarini, Morogoro
WATUMISHI wa Dini nchini wametakiwa kumtanguliza Mungu katika
utumishi wao ili kuendelea kudumisha amani ya nchi iliyopo hasa katika kipindi
hichi cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Ushauri huo umetolewa huko Lugoba wilayani Bagamoyo mkoani
Pwani na Mtawa Sista Perpetua Mlamwaza (72) wakati wa maandalizi ya Jubilei ya
miaka 50 ya Utawa kwenye kanisa la Katoliki na kusem akuwa siri kubwa ya
mafanikio yake ya utendaji yanatokana na kumtanguliza mbele Mungu.
Mlamwaza alisema kuwa watumishi wa Mungu wana nafasi kubwa ya
kuifanya nchi iendelee kudumu ni kwa wao kumtanguliza Mungu na kuliombea Taifa
letu ili liwe amani ambayo imedumu tangu nchi kupata Uhuru.
“Kipindi hichi tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu hivyo lazima
tupige magoti kumwomba Mungu azidi kutudumishia amani yetu iliyopo kwani yeye
ndiye mwenye uwezo wa kutunusuru na hali yoyote ambayo inaashiria uvunjifu wa
amani,” alisema Mlamwaza.
Mlamwaza ambaye aliwalea kiroho hadi kufanikiwa kupata upadri
Mhashamu Askofu Antony Banzi wa Jimbo la Tanga na padri Peter Kunambi alisema
kuwa watumishi ni kiungo muhimu kati ya wanadamu na Mungu.
“Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuweza kumtumikia Mungu kwa
kipindi chote cha miaka 50 ya utumishi wangu lakini amani hii iliyopo inapaswa
kulindwa na kuendelezwa ili tuendelee kupata mafanikio ya kimaendeleo,” alisema
Mlamwaza.
Aidha alisema kuwa Watanzania wote wanapaswa kufanya maombi
ya kila wakati ikiwa ni pamoja kufunga ili kumwomba Mungu aendelee kutudumishia
amani iliyopo hasa ikizingatiwa Tanzania ni Kisiwa cha amani.
Aliwataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka shule watoto wao
hususani wale wa kike ili waweze kuwarithisha elimu ambayo itakuwa ni mkombozi
katika maisha yao na si mali kama baadhi ya watu wanavyofikiri.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment