Monday, September 26, 2016

MAJALIWA AWASIMAMISHA MAOFISA MISITU RUFIJI

Na John Gagarini,Rufiji
WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Suleiman Bulenga kwa kushindwa kudhibiti na kusimamia mapato yatokanayo na shughuli za misitu hivyo kuikosesha mapato Serikali.
Mbali ya meneja huyo maafisa misitu watatu nao wamesimamishwa kutokana na kushindwa kudhibiti na kusimamia shughuli za uvunaji misitu na kusababisha wilaya kukosa mapato .
Maofisa misitu waliosimamishwa ni pamoja na Ofisa maliasili na mazingira wa wilaya Dk Paul Ligonja,Ofisa misitu Gaudence Tarimo na Jonas Nambua ambao watsimamishwa hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
Majaliwa alichukua hatua hiyo wilayani Rufiji wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji na wananchi wa wilaya hiyo  na kusema kuwa sekta ya misitu ni tatizo kwa kila wilaya na Rufiji ni moja ya wilaya hizo .
“Magogo yanasafirishwa bila utaratibu,na ndio wanakata miti kwenye misitu ya Utete na kupiga nyundo maeneo ya Kilwa,” alisema Majaliwa.
Alisema kuwa hakuna manufaa na TFS hivyo ameamua kusimamisha shughuli zote za uvunaji,katika wilaya hiyo na watumishi hao hadi wizara itakapotoa maelekezo mengine.
“Wilaya ya Rufiji inaongoza katika suala la utoroshaji wa misitu na kuruhusu uvunaji holela suala ambalo halikubaliki na nataka uwajibikaji na uadilifu katika maeneo ya kazi na watumishi wanapaswa wabadilike na waache kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Majaliwa. 
Aidha Majaliwa alikemea utozwaji wa ushuru kwa watu wanaochoma mkaa unaofanywa na halmashauri ya Rufiji kwani kwa kufanya hivyo ni kuruhusu ukataji ovyo wa miti.
“Mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halamshauri ya Rufiji mnapaswa kusimamia mapato na matumizi ya fedha ili kuongeza mapato ya halmashauri iweze kupiga hatua ya kimaendeleo,”alisema Majaliwa.
Naye mbunge wa Rufiji,Mohammed Mchengelwa alisema kuwa nidhamu kwa watumishi inaonekana kupungua kwa baadhi ya watumishi kwenye halmashauri hiyo.

Mwisho




Friday, September 23, 2016

WAWILI WAFA AJALINI MMOJA ACHOMWA MOTO

Na John Gagarini, Kibaha

WATU wawili wamefariki dunia na wengine 11 kujeruhiwa mkoani Pwani kufuatia ajali iliyohusisha mabasi madogo mawili ya abiria kugongana uso kwa uso huko Kiparanganda wilayani Mkuranga.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na Kamanda wa Polisi mkoani humo Bonaventura Mushongi alisema kuwa watu hao walifariki papo hapo.

Mushongi alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Septemba 21 mwaka huu majira ya saa 10:30 jioni T363 DCV likiendeshwa na Zidadu Mohamed (25) mkazi wa Dar es Salaam akielekea Kimazinchana liligongana na T363DHD yote aina ya Toyota Hiace likiendeshwa na Miraji Mlonga (22) akielekea Dar es Salaam.

Aliwataja waliokufa kuwa ni Zuhura Haji (21) na Neema Julius (25) wote wakazi wa Kimazinchana wilaya ya Mkuranga ambapo miili yao imehifadhiwa kwenye Hopsitali ya Wilaya ya Mkuranga kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi.

Aidha aliwataja watu waliojeruhiwa kuwa ni Majeruhi ni Mariamu Aloyce (46) wa Kimazinchana Mariamu Sultan (60) mkzai wa Chanika, Yusufu Maziku (33) mkazi wa Kimazinchana,Kulwa Abdala (30) makzi wa Mbagala,Ibrahim Hamis (3) mkazi wa Mbagala na Fatma Abdul (25) mkazi wa Chanika.

Wengine ni Salum Mohamed (54) mkazi wa Mwalusembe, Litus Mwarami (26) mkazi wa Kimazinchana Kidawa Abdala (30) mkazi wa Mbagala, Issa Hemed (2) mkazi wa Kimazinchana na Greyson Ernest (23) mkazi wa Kimazinchana.

“Tuna washikilia madereva wote waili kutokana na kusababisha ajali hiyo na watafikishwa mahakamani mara upelelezi wa kesi hiyo utakapokamilika ili kujibu tuhuma hizo zinazowakabili,” alisema Mushongi.

Kwenye tukio lingine mkazi wa Kwa Mathias Hamis Tenende (38) aliuwawa kwa kupigwa kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali kwa madai ya kutaka kuiba pikipiki eneo la Umwelani.

Mwisho.
 








Monday, September 12, 2016

WAPONGEZA IDD EL HAJI KUFANYIKA KWA PAMOJA


Na John Gagarini, Kibaha

KUFUATIA sherehe ya Idd el Haji ambayo inahusisha na uchinjaji kufanyika jana ambapo waumini wa dini ya Kiislamu walisherehekea kwa pamoja tofauti na miaka mingine ambapo kila dhehebu lilikuwa likifanya siku tofauti safari hii wamefurahi kufanya kwa pamoja.

Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha baadhi ya waumini wa Kiislamu wamesema kuwa utaratibu wa kusherehekea kwa pamoja ni mzuri kwani unaonyesha umoja na ni vema ukaendelea hata kwa siku zijazo.

Mrisho Halfan “Swagala”  alisema kuwa hakuna sababu wao kama waumini wa imani moja kufanya sherehe kwa wakati tofauti na kufanya kama ni imani tofauti.

“Tunaomba viongozi wa taasisi hizi za dini yetu wakae kwa pamoja na kufanya vitu kwa pamoja kwani kama mwaka huu sikukuu imependeza kwani wote tumejumuika na hali hii imeondoa tofauti na kutufanya kitu kimoja,” alisema Swagala.

Alisema kuwa kuna haja ya kuunganisha umoja wa waislamu kama hivi kwa kiufanya sherehe hiyo ambayo ni kubwa kwa Waislamu kote duniani kukumbuka yale yaliyofanywa na mtume ikiwa ni kufanya mambo yanayompendeza Mungu.

Kwa upande wake Abubakari Lipambila kutoka Masjidi Hazarajii Maili Moja Kibaha alisema kuwa sikukuu hiyo ni kwa ajili ya kurejesha furaha kwa watu wote.

Lipambila alisema kuwa waumini wa dini ya kiislamu wanapaswa kujihadhari na shetani katika kipindi hichi cha sherehe kwani naye yuko kazini kwa kuwapotosha watu ili waende kinyume na imani kwa kujiingiza kwenye vitendo viovu.

Mwisho.

Wednesday, September 7, 2016

BINTI AZAA MTOTO AMTUPA

Na John Gagarini, Kibaha

BINTI aliyetambulika kwa jina la Judith Paulo anayekadiriwa kuwa na umri katia ya miaka (18) na (22) anatuhumiwa kuzaa mtoto wa jinsia ya kike kisha kumtupa mwanae jirani na jalala.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu mwenyekiti wa Kitongoji cha Pera kata ya Pera Chalinze Mjini Hussein Mramba alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 7 majira ya saa 12 asubuhi eneo la Kwa Mwarabu.

Mramba alisema kuwa kichanga hicho chenye uzito wa kilogramu 3.2 kiliokotwa baada ya watoto waliokuwa wakiokota vitu mbalimbali jirani na jalala huku kikiwa kimewekwa kwenye mfuko wa Rambo.

“Watoto hao ndiyo waliogundua na ndipo walipotoa taarifa kwa watu wazima na kwenda kumchukua ambapo walimkuta mtoto huyo akiwa na afya njema huku akiwa hajavalishwa nguo yoyote mwilini mwake na jambo la kumshukuru Mungu kuwa mtoto huyo hakupata madhara yoyote,” alisema Mramba.

Alisema kuwa baada ya hapo ilibidi wasamaria wema wampeleke Hospitali ili kuangalia namna ya kumsaidia mtoto huyo ambaye kwa sasa yuko kwa mama mmoja ambaye amejitolea kukaa naye wakati taratibu nyingine zinafanyika ili apelekwe sehemu stahiki.

“Kwa maelezo tuliyopata baada ya kwenda Kituo cha Afya cha Chalinze ili kujua kama alijifungua hapo ilibainika kuwa binti huyo alijifungua kituoni hapo juzi majira ya saa 4 baada ya kufika hapo majira ya saa 3 usiku akiwa na uchungu wa kujifungua huku akiwa hajaongozana na mtu yoyote,” alisema Mramba.

Mramba ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Chalinze alisema kuwa baada ya kujifungua alikaa kama masaa mawili kisha kuomba kuondoka baada ya kujifungua salama na alimwomba muuguzi aondoke kwani alikuwa hajafunga mlango wa nyumba anayoishi hivyo ana hofu ya kuibiwa vitu vyake.

“Kutokana na utetezi wake huo ilibidi baadhi ya wazazi wamsaidia fedha kwa ajili ya kulipia teksi baada ya kumuonea huruma ambapo yeye alifika hapo kituoni kwa kutumia bodaboda,” alisema Mramba.

Aidha alisema kuwa binti huyo alionekana kuwa na wasiwasi alipofika kituoni hapo lakini hata hivyo baadhi ya wazazi waliokuwa hapo walijaribu kumweka sawa ili aone jambo la uzazi ni la kawaida.

Alisema kuwa taarifa hizo wamezitoa sehemu mbalimbali ikiw ani pamoja na polisi kwa ajili ya kusaidia kupatikana kwa binti huyo ambapo mita kama 100 aliposhushwa na teksi wamejaribu kuulizia lakini inavyoonekana kuwa hakuwa anakaa maeneo hayo kwani jina hilo hakuna mtu anayelifahamu.


Mwisho.

Tuesday, August 30, 2016

BOMOABOMOA YALETA KIZAZAA MAILI MOJA KIBAHA


Na John Gagarini, Kibaha

WANANCHI wa eneo la Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wamelia na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Pwani kuwa wawafikirie kwa kuwalipa fidia wakati wa zoezi la bomobomoa ambalo linatarajiwa kufanyika Novemba 23 mwaka huu.

Hataua hiyo imekuja baada ya TANROADS kutoa barua kwa watu waliojenga kwenye eneo la hifadhi ya barabara inayomilikiwa na wakala hiyo kwa wale waliojenga umbali wa mita 120 kwa kila upande wa barabara kuu ya Dar es Salaam Morogoro kuanzia Kiluvya hadi Tamco waanze kubomoa kabla ya zoezi hilo kwa kuwapa siku 90 kufanya hivyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo mkoa wa Pwani Mrisho Swagala alisema kuwa mbali ya kuwtowlaipa fidia pia eneo linalopitiwa na zoezi hilo ni kubwa sana ikilinganishwa na maeneo mengine.

“Hatukati zoezi hilo kufanyika lakini wangeangalia namna ya kuwafidia wananchi kwani kuwabomolae bila ya kuwapa fidi itakuwa ni kitendo cha ukatili na kinakwenda kinyume cha haki za binaadamu kwani bomoa hiyo itawaacha watu wengi wakiwa hawana mahali pa kuishi na kwa wafanyabiashara hawatakuwa na sehemu ya kufanyia biashara,” alisema Swagala.

Alisema kuwa alisema kuwa sheria ya barabara iliyotungwa mwaka 1932 ambapo inadaiwa kuwa watu walilipwa fidia jambo ambalo kwa kipindi hicho fedha ilikuwa ni ndogo ukilinganisha hali halisi ya sasa hivyo kuna haja ya kuwafikiria.

Naye Ally Gonzi mwenyekiti wa ushirika wa wafanyabiashara wa soko la mkoa la Maili Moja alisema kuwa wao kama wafanyabiashara wansikitishwa na hatua hiyo kwani hadi sasa hawajui watakwenda kufanyia biashara wapi.

Gonzi alisema kuwa waliahidiwa kuwa watajengewa soko la kisasa lakini hadi sasa soko halijajengwa ambapo wao wako hapo kwa zaidi ya miaka 35 na Halmashauri ambao wao wako chini yao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Mtaa wa Maili Moja Athuma Mkongota alisema kuwa wananchi wengi wamekwenda ofisini kwake kwenda kulalamika juu ya zoezi hilo ambalo litawakumba watu wengi ambao wako katikati ya mji huo.

Mkongota alisema kuwa ubomoaji huo umekuja baada ya kuisha kwa kesi iliyofunguliwa na wananchi kupinga hatua hiyo lakini walishindwa hata hivyo alisema kuwa hukumu ya kesi hiyo bado hajaipata.

Awali mkaguzi wa barabara wa mamlaka hiyo Livingston Urio alisema kuwa kwa sasa wanaendelea na zoezi la kutoa barua ambapo idadi kamili ya nyumba na vibanda vya biashara vitakavyobomolewa itajulikana.

Urio alisema kuwa ilikuwa ifanyike mwezi Agosti lakini waliongeza hadi Novemba lakini miaka ya nyuma tayari walishawawekea alama ya X mwaka 2004 lakini zoezi hilo halikufanyika lakini kwa sasa zoezi hilo linafanyika.

Alisema kuwa wananchi walipoenda mahakamani walishinda na kuonekana kuwa eneo hilo ni mali ya mamlaka hiyo na kuwa eneo hilo magari yanakwenda taratibu hivyo barabara kuharibika na baada ya bomoa hiyo eneo hilo litawekwa stendi kubwa na patapangwa vizuri ili mji uonekane vizuri.

“Kulingana na sheria ya barabara ya mwaka 1932 na kufanyiwa marekebisho 1958 kifunga na 52 na marekebisho ya sheria ya barabara na 13 ya mwaka 2007 sambamba na taratibu za sheria za usimamizi wa barabara kifungu na 30 (b) eneo la hifadhi ya barabara sehemu iliyotajwa hapo juu ni mita 120 sawa na futi 400 kwenda kila upande kutoka katikati ya barabara ni marufuku kufanya maendelezo yoyote katika eneo hilo,” alisema Urio.


Mwisho.  

MBUNGE AITAKA DAWASCO KUUNGANISHA MAJI BILA YA UPENDELEO WA FEDHA


Na John Gagarini, Kibaha

MAMLAKA ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) wilaya ya Kibaha mkoani Pwani imetakiwa kuwaunganishia maji wananchi wa Mlandizi bila ya kujali uwezo wa mtu ili kila mtu aweze kunufaika na mradi wa maji kwenye Kitongoji cha Janga.
Hayo yalisemwa na mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijni Hamoud Jumaa wakati alipofanya ziara kutembelea mradi wa maji wa ya mkopo kwenye kitongoji cha Janga kata ya Janga wilayanai Kibaha.

Mbunge huyo alitoa wito huo kufuatia mwenyekiti wa kitongoji hicho Josephine Maendaenda kudai kuwa baadhi ya wananchi wanalalamika kuwa watu wanaotoa fedha taslimu ndiyo wanaounganishiwa maji huku wale wanaokopa kutakiwa kusubiri.

“Kwanza nawapongeza wananchi kwa kuchimba mitaro ya kulaza mabomba hivyo thamani ya nguvu zao lazima zithaminiwe sawa na wale wanaotoa fedha taslimu kwani mitaro hiyo isingechimbwa na wananchi hao maji yasingeweza kufika kwenye maeneo ya watu,” alisema Jumaa.

Alisema kuwa thamani ya watu iko palepale lakini haiwezi kwani wanaotoa fedha na wale waliotumia nguvu zao kuchimba mitaro wamefanya kazi kubwa ambayo inapaswa kuungwa mkono na siyo ya kubezwa.

“Wananchi hawa wameonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kufanyakazi ya kujitolea na ndiyo tunataka utamaduni huu ufanyike kwenye kila jambo na si kusubiri serikali iwafanyie wananchi kila kitu kwani hata kwenye mikoa iliyoendelea kama Moshi na Arusha imefanikiwa kwa wananchi kujitolea kama huku,” alisema Jumaa.

Kwa upande wake meneja wa Dawasco wilaya ya Kibaha Erasto Emanuel alisema kuwa suala hilo watalifanyia kazi kwa kuwaunganishia wananchi bila ya kujali kama ni malipo ya moja kwa moja au mkopo.

Emanuel alisema kuwa hadi sasa wameweza kuwaunganishaia maji wananchi 40 huku wakitarajia kuwafikia wateja 300 katika hatua ya pili huku wakitarajia maji kuanza kutoka mwezi Oktoba na kuwafikia wateja 600.

Alisema kuwa mradi huo ulikumbwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa jambo ambalo lililalamikiwa na wananchi lakini yote hiyo ilitokana na kila mwaka kuwa na zoezi la kufunga mwaka ambalo huambatana na uhakiki wa vifaa.

Naye mwenyekiti wa Kitongoji cha Janga Josephine Maendaenda alisema kuwa changamoto ya maji ni kubwa kwenye kitongoji hicho na wananchi wamekuwa wakilalamika kiu yao kubwa ikiwa ni kupata maji ambapo wamekuwa wakienda mwendo mrefu kufuata maji ambapo huuziwa dumu la lita 20 kwa shilingi 500.

Mwisho. 

KAMPUNI YA UUNGANISHAJI MAGARI YAZIMAMOTO MBIONI KUANZA USZALISHAJI

Na John Gagarini, Kibaha

KAMPUNI ya Equator Suma Jkt inatarajia kuanza kuunganisha magari ya zimamoto na matrekata mwishoni mwa mwaka huu ikiwa ni moja ya njia ya kukabiliana na majanga ya moto pamoja na kuinua kilimo cha Tanzania ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea kiwanda hicho kilichopo Ruvu Mlandizi wilayani Kibaha mkurugenzi Robert Mangazeni alisema kuwa kwa sasa kiwanda hicho kiko kwenye hatua za mwishi ikiwa ni pamoja na uunganishaji wa mitambo na mashine.

Mangazeni alisema kuwa teknolojia ya uunganishaji wa magari ya zimamoto ambapo watatumia magari ya kawaida kwa kuyabadilisha na kuwa ya zimamoto wameitoa nchi ya Urusi kutoka kwenye makampuni ya St Auto na Ural huku ile ya matekta wakiitoa kwenye kampuni za Escort kutoka nchini India na Farmtrac kutoka nchini Poland.

“Tukizungumzia kuhusu uunganishaji wa magari ya zimamoto ni teknolojia ambayo imeboreshwa na kuwa ya kisasa zaidi ambapo tutakuwa na uwezo wa kuunganisha magari ya aina mbalimbali kutegemeana na mteja anavyotaka ambayo yatakuwa na ujazo wa aina tofauti tofauti kuanzia magari makubwa hadi madogo siyo lazima yawe makubwa kama tulivyozoea hivyo hata majanga haya ambayo yamezikumba shule sasa taasisi zitaweza kudhibiti moto,” alisema Mangazeni.

Alisema kuwa ujazo huo utaanzia lita za maji 300 hadi 10,000 kutegemea na ukubwa hivyo kulinagana na miuondombinu ya barabara za mitaani wataunganisha hata magari madogo ili yaweze kufika kwenye eneo lililopata maafa ya moto.

“Ikumbukwe Tanzania itakuwa nchi ya pili kuwa na teknolojia hii ya uunganishaji wa magari ya zimamoto baada ya Afrika Kusini ambapo kwa nchi za Maziwa Makuu itakuwa ni ya kwanza na itaweza kuokoa asilimia 30 ya gharama ya kununua gari jipya la zimamoto pia watakuwa na uwezo wa kuyatengeneza magari hayo badala ya kuagiza wataalamu toka nje ya nchi mara yanapoharibika,”alisema Mangazeni.

Aidha alisema kuwa kwa upande wa matrekta wataweza kuyaunganisha ambapo kwa miaka ijayo watakuwa na uwezo wa kutengeneza trekta ambalo litakuwa ni zao la Tanzania tofauti na ilivyo sasa kuagizwa toka nje ya nchi.

“Miaka ijayo tutatengenza trekta la kwetu ambapo kwa sasa vitakuwa vinakuja vifaa vyake na kuunganishiwa hapa na tatizo la matrekta kufa haraka litakwisha kwani mafundi wa matrekta watazalishwa hapa na yatadumu kwani wengi hawana utaalamu wautengenzaji bali wanatumia uzoefu tu,” alisema Mangazeni.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kibaha Asumter Mshama alisema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho umekuja wakati mwafaka kwa upande wa janga la moto na kilimo bora.

Mshama alisema kuwa kiwanda hicho ambacho kitafanya shghuli hizo kwa pamoja itakuwa mwarobaini wa changamoto hizo ambazo ni kubwa na pia ni kutekeleza sera ya Rais John Magufuli ya kutaka Tanzania kuwa nchi ya viwanda ili baada ya miaka ijayo nchi kuwa na uchumi wa kati.

Ujenzi wa kiwanda hicho ulianza ulianza 2011 ambacho hadi kukamilika kwake kitakuwa na thamani ya shilingi bilioni tatu kitaajiri wafanyakazi 100 na kamapuni hiyo imeingia ubia na Suma Jkt na inaundwa na wanajeshi wastaafu.
 

Mwisho.