Monday, September 26, 2016

MAJALIWA AWASIMAMISHA MAOFISA MISITU RUFIJI

Na John Gagarini,Rufiji
WAZIRI mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Rufiji mkoani Pwani Suleiman Bulenga kwa kushindwa kudhibiti na kusimamia mapato yatokanayo na shughuli za misitu hivyo kuikosesha mapato Serikali.
Mbali ya meneja huyo maafisa misitu watatu nao wamesimamishwa kutokana na kushindwa kudhibiti na kusimamia shughuli za uvunaji misitu na kusababisha wilaya kukosa mapato .
Maofisa misitu waliosimamishwa ni pamoja na Ofisa maliasili na mazingira wa wilaya Dk Paul Ligonja,Ofisa misitu Gaudence Tarimo na Jonas Nambua ambao watsimamishwa hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.
Majaliwa alichukua hatua hiyo wilayani Rufiji wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji na wananchi wa wilaya hiyo  na kusema kuwa sekta ya misitu ni tatizo kwa kila wilaya na Rufiji ni moja ya wilaya hizo .
“Magogo yanasafirishwa bila utaratibu,na ndio wanakata miti kwenye misitu ya Utete na kupiga nyundo maeneo ya Kilwa,” alisema Majaliwa.
Alisema kuwa hakuna manufaa na TFS hivyo ameamua kusimamisha shughuli zote za uvunaji,katika wilaya hiyo na watumishi hao hadi wizara itakapotoa maelekezo mengine.
“Wilaya ya Rufiji inaongoza katika suala la utoroshaji wa misitu na kuruhusu uvunaji holela suala ambalo halikubaliki na nataka uwajibikaji na uadilifu katika maeneo ya kazi na watumishi wanapaswa wabadilike na waache kufanya kazi kwa mazoea,” alisema Majaliwa. 
Aidha Majaliwa alikemea utozwaji wa ushuru kwa watu wanaochoma mkaa unaofanywa na halmashauri ya Rufiji kwani kwa kufanya hivyo ni kuruhusu ukataji ovyo wa miti.
“Mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halamshauri ya Rufiji mnapaswa kusimamia mapato na matumizi ya fedha ili kuongeza mapato ya halmashauri iweze kupiga hatua ya kimaendeleo,”alisema Majaliwa.
Naye mbunge wa Rufiji,Mohammed Mchengelwa alisema kuwa nidhamu kwa watumishi inaonekana kupungua kwa baadhi ya watumishi kwenye halmashauri hiyo.

Mwisho




No comments:

Post a Comment