Na John Gagarini, Kibaha
KUFUATIA sherehe ya Idd el Haji ambayo inahusisha
na uchinjaji kufanyika jana ambapo waumini wa dini ya Kiislamu walisherehekea
kwa pamoja tofauti na miaka mingine ambapo kila dhehebu lilikuwa likifanya siku
tofauti safari hii wamefurahi kufanya kwa pamoja.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha
baadhi ya waumini wa Kiislamu wamesema kuwa utaratibu wa kusherehekea kwa
pamoja ni mzuri kwani unaonyesha umoja na ni vema ukaendelea hata kwa siku
zijazo.
Mrisho Halfan “Swagala” alisema kuwa hakuna sababu wao kama waumini
wa imani moja kufanya sherehe kwa wakati tofauti na kufanya kama ni imani
tofauti.
“Tunaomba viongozi wa taasisi hizi za dini yetu
wakae kwa pamoja na kufanya vitu kwa pamoja kwani kama mwaka huu sikukuu
imependeza kwani wote tumejumuika na hali hii imeondoa tofauti na kutufanya
kitu kimoja,” alisema Swagala.
Alisema kuwa kuna haja ya kuunganisha umoja wa
waislamu kama hivi kwa kiufanya sherehe hiyo ambayo ni kubwa kwa Waislamu kote
duniani kukumbuka yale yaliyofanywa na mtume ikiwa ni kufanya mambo
yanayompendeza Mungu.
Kwa upande wake Abubakari Lipambila kutoka Masjidi
Hazarajii Maili Moja Kibaha alisema kuwa sikukuu hiyo ni kwa ajili ya kurejesha
furaha kwa watu wote.
Lipambila alisema kuwa waumini wa dini ya kiislamu
wanapaswa kujihadhari na shetani katika kipindi hichi cha sherehe kwani naye
yuko kazini kwa kuwapotosha watu ili waende kinyume na imani kwa kujiingiza
kwenye vitendo viovu.
No comments:
Post a Comment