Wednesday, September 7, 2016

BINTI AZAA MTOTO AMTUPA

Na John Gagarini, Kibaha

BINTI aliyetambulika kwa jina la Judith Paulo anayekadiriwa kuwa na umri katia ya miaka (18) na (22) anatuhumiwa kuzaa mtoto wa jinsia ya kike kisha kumtupa mwanae jirani na jalala.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu mwenyekiti wa Kitongoji cha Pera kata ya Pera Chalinze Mjini Hussein Mramba alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 7 majira ya saa 12 asubuhi eneo la Kwa Mwarabu.

Mramba alisema kuwa kichanga hicho chenye uzito wa kilogramu 3.2 kiliokotwa baada ya watoto waliokuwa wakiokota vitu mbalimbali jirani na jalala huku kikiwa kimewekwa kwenye mfuko wa Rambo.

“Watoto hao ndiyo waliogundua na ndipo walipotoa taarifa kwa watu wazima na kwenda kumchukua ambapo walimkuta mtoto huyo akiwa na afya njema huku akiwa hajavalishwa nguo yoyote mwilini mwake na jambo la kumshukuru Mungu kuwa mtoto huyo hakupata madhara yoyote,” alisema Mramba.

Alisema kuwa baada ya hapo ilibidi wasamaria wema wampeleke Hospitali ili kuangalia namna ya kumsaidia mtoto huyo ambaye kwa sasa yuko kwa mama mmoja ambaye amejitolea kukaa naye wakati taratibu nyingine zinafanyika ili apelekwe sehemu stahiki.

“Kwa maelezo tuliyopata baada ya kwenda Kituo cha Afya cha Chalinze ili kujua kama alijifungua hapo ilibainika kuwa binti huyo alijifungua kituoni hapo juzi majira ya saa 4 baada ya kufika hapo majira ya saa 3 usiku akiwa na uchungu wa kujifungua huku akiwa hajaongozana na mtu yoyote,” alisema Mramba.

Mramba ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Chalinze alisema kuwa baada ya kujifungua alikaa kama masaa mawili kisha kuomba kuondoka baada ya kujifungua salama na alimwomba muuguzi aondoke kwani alikuwa hajafunga mlango wa nyumba anayoishi hivyo ana hofu ya kuibiwa vitu vyake.

“Kutokana na utetezi wake huo ilibidi baadhi ya wazazi wamsaidia fedha kwa ajili ya kulipia teksi baada ya kumuonea huruma ambapo yeye alifika hapo kituoni kwa kutumia bodaboda,” alisema Mramba.

Aidha alisema kuwa binti huyo alionekana kuwa na wasiwasi alipofika kituoni hapo lakini hata hivyo baadhi ya wazazi waliokuwa hapo walijaribu kumweka sawa ili aone jambo la uzazi ni la kawaida.

Alisema kuwa taarifa hizo wamezitoa sehemu mbalimbali ikiw ani pamoja na polisi kwa ajili ya kusaidia kupatikana kwa binti huyo ambapo mita kama 100 aliposhushwa na teksi wamejaribu kuulizia lakini inavyoonekana kuwa hakuwa anakaa maeneo hayo kwani jina hilo hakuna mtu anayelifahamu.


Mwisho.

No comments:

Post a Comment