Thursday, August 28, 2014

RT YATAKIWA KUANDAA MKUTANO WA KATIBA

Na John Gagarini, Kibaha
CHAMA cha Riadha Tanzania (RT) kimetakiwa kiandae mkutano mkuu wa chama ili kupitia rasimu ya katiba baada ya mkutano kama huo kuahirishwa Juni na kutakiwa kufanyika Novemba mwaka jana lakini hadi sasa hakuna taarifa ya kufanyika mkutano kama huo .
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mwenyekiti wa chama cha riadha mkoa wa Pwani (CRAA) Joseph Luhende alisema kuwa baada ya kushindikana kufanyika kwa mkutano kwa ajili ya kupitisha rasimu hiyo huko mkoani Morogoro iliamuliwa kuwa mkutano kama huo ufanyike lakini hadi sasa imekuwa kimya.
Luhende alisema kuwa upitishaji wa rasimu ya chama ilishindikana kutokan na kuchelewa hivyo kupangwa Novemba mwaka jana na hadi sasa hakuna taarifa yoyote ya kufanyika mkutano kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo.
“Mbali ya kushindikana kupitishwa kwa rasimu ya katiba hiyo pia vyama vilitakiwa visitumie katiba ya zamani na tulivyouliza tuliambiwa kuwa tusubiri na sasa inakaribia kufika mwaka lakini hakuna lolote linaloendelea hali ambayo inakatisha tamaa,” alisema Luhende.
Alisema mchezo wa riadha unakumbwa na changamoto nyingi hivyo rasimu hiyo ingepitishwa ingesaidia kuboresha riadha lakini utekelezaji umekuwa mgumu na rasimu ndiyo inayopelekea kupata katiba ambayo ni kila kitu sawa na dira ya mwelekeo wa mchezo huo.
“Utendaji kazi unakuwa mgumu kutokana na kutakiwa tusitumie katiba ya zamani hivyo ni vema rasimu hiyo ikapitishwa ili tuweze kupata katiba mpya ambayo itatuongoza,” alisema Luhende.
Aidha alisema kuwa kutokana na mipango ya RT kutokuwa mizuri kumechangia nchi kufanya vibaya kwenye michuano ya kimataifa mfano ile ya Olimpiki ambapo Tanzania iliambulia patupu kwenye mchezo huo na kuwataka viongozi wa shirikisho hilo kuwa makini katika kutekeleza majukumua yao.
Akijibu kuhusiana na suala hilo kwa njia ya simu katibu mkuu wa RT Suleiman Nyambui alisema kuwa tatizo kubwa lililopo ni ukosefu wa fedha ndiyo inapelekea wao kushindwa kuandaa mkutano mkuu wa kupitisha rasimu hiyo ya katiba ili kupata katiba mpya.
“Tunaendelea kuwasiliana na wafadhili mbalimbali ili tuweze kupata fedha kwa ajili ya kuandaa mkutano huo wa kupata katiba ambayo itaongoza chama baada ya mkutano wa awali kushindwa kuendelea baada ya viongozi wa mikoa ambao walisema hawajaisoma vizuri hivyo ikashindika kuijadili rasimu hiyo,” alisema Nyambui.
Nyambui alisema walipeleka katiba mikoani kwa ajili ya wao kutoa mapendekezo lakini hawakuweza kuyapeleka ambapo ni mikoa mitatu tu ndiyo iliyotoa mapendekezo yake  ambayo ni Dar es Salaam, Arusha na Dodoma huku mingine ikiwa bado.
“Tunatarajia kuitisha mkutano mkuu kabla ya mwaka haujaisha ili kukamilisha zoezi la kupata katiba baada ya marekebisho kufanyika kwenye mkutano na kikwazo kikuu ni ukosefu wa fedha,” alisema Nyambui.
Mwisho.



HALMASHAURI ZAKATAZWA KUTOZA USHURU

Na John Gagarini, Kibaha
HATIMAYE mkoa wa Pwani umetoa tamko la kuzizuia Halmashauri za mkoa huo kuendelea kutoza ushuru wa hoteli na nyumba za kulala wageni ambao ulifutwa na bunge mwaka 2009 huku Halmashauri ya mji wa Kibaha ikiwa inaendelea kuutoza na kusababisha malalamiko ya wafanyabiashara hao.
Kufuatia halmashauri hiyo kuendelea kutoza ushuru huo kupitia umoja wao Wamiliki wa Hoteli wilayani Kibaha mkoani Pwani (UGEHOKI) walipeleka malalamiko yao ofisi ya katibu tawala wa mkoa huo kupinga kutozwa ushuruhuo wa asilimia 20.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo Mhandisi Michael Mrema, alisema kuwa halmashauri zote zilipewa miongozo kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) juu ya kusitisha utozaji huo hadi watakapopewa utartibu mwingine wa ukusanyaji.
“Tulipokea barua toka kwa wamiliki hao juu ya kulalamikia ushuruhu huo ambao ulisitishwa wakati wizara zinazohusika zitakapokuwa zimeweka utaratibu mwingine wa namna ya ukusanyaji wa ushuru huo ambao ulilalamikiwa na wamiliki hao kuwa ni mkubwa sana,” alisema Mrema.
Mrema alisema kuwa barua hiyo toka TAMISEMI ya kusitisha ushuru huo yenye kumbukumbu namba Na. FA 2/266/01/10 ya Mei ya mwaka 2014 kwa halmashauri zote nchini ambayo ilitokana na barua yenye kumbukumbu Na. CE.325/387/03/47 ya tarehe 16 ya mwezi wa Aprili mwaka 2014 iliyotoa uafafanuzi zaidi.
“Katika ufafanuzi TAMISEMI ilisema kuwa ushuru wa nyumba za kulala wageni umeainishwa katika sheria ya fedha sura 290 kifungu cha 6(1)(q) na 7(1)(u) na kwamba awali ushuru huo ulikuwa ukitozwa kupitia sheria ya hoteli sura 105 ambayo imefutwa baada ya kutungwa sheria mpya sheria ya Utalii na 29 ya mwaka 2008 na kuanza kutumika rasmi Julai Mosi 2009 baada ya kutangazwa kwenye gazeti la serikali namba 212 la tarehe 1 Julai 2009 ni wazi kuendelea kutozwa ni kukiuka sheria za Utalii,” alisema Mrema.
Aidha Mrema alisema kutokana na barua hizo Halmashauri zilipaswa kutoendelea kutoza ushuru huo hivyo hazipaswi kuendelea kuutoza na zikiendelea kutoza kunaweza kusababisha halmashauri na watoa huduma  hao ni kusababisha migogoro mikubwa ya kisheria na kwa sasa wizara za TAMISEMI, Wizara ya Fedha na Wizara ya Maliasili na Utalii zipo katika majadiliano ya kuamua namna bora ya kurejesha ushuru huo.

Alizitaka halmashauri hizo kutekeleza agizo hilo na maagizo mengine yanayotoka ngazi za juu ili kuepusha migogoro na watoa huduma na wananchi katika suala zima la ukusanyaji wa mapato mbalimbali.

Wednesday, August 27, 2014

WALILIA FIDIA YA MASHAMBA YAO

Na John Gagarini, Kibaha
WAKAZI nane wa kitongoji cha Benki kata ya Igunga wilaya ya Igunga mkoani Tabora wameiomba Halmashauri ya wilaya kuwalipa fidia ya mashamba yao ambayo yamechukuliwa na Halmashauri hiyo kwa ajili ya upanuzi wa hospitali ya wilaya.
Wakazi hao walitoa ombi hilo kufuatia Halmashauri hiyo kuwa kimya kwa muda mrefu baada ya mashamba yao kuchukuliwa tangu mwaka 2010 nakufanyiwa tathmini mwezi Februari mwaka huu lakini hadi sasa bado hawajalipwa fidia za maeneo yao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini Kibaha mwenyekiti wa kamati ya waathirika hao  Daniel Shamalatu alisema kuwa mashamba yao yana ukubwa wa zaidi ya hekari 24 ambazo zilichukuliwa kwa ajili ya upanuzi huo wa hospitali ya wilaya.
Shamalatu alisema kuwa maeno yao yalichukuliwa bila ya wao kupewa taarifa ambapo mazao yao waliyokuwa wameyapanda yalifyekwa na ujenzi kuanza bila ya kupewa fidia.
“Tulipoona kimya tulikwenda mahakamani ili tuweze kulipwa fidia zetu lakini baraza la madiwani liliingilia kati na kututaka tuondoe kesi mahakamani ili tukubaliane nje ya mahakama, kweli tuliondoa kesi hiyo mahakamani lakini hakuna kinachoendelea ambapo sasa ni karibu mwaka umepita lakini tunaona kimya na tunapofuatilia halmashauri tunaambiwa suala letu linashughulikiwa,” alisema Shamalatu.
Alisema kuwa wao hawapingi ujenzi huo lakini wanachotaka ni kulipwa fidia kutokana na ukubwa wa mashamba yao na si kiwanja kimoja kila heka kama walivyotaka kufanya na pia wanataka kujua malipo yao yatafanyika lini.
 Akitolea ufafanuzi suala hilo kwa njia ya simu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Rustika Turuka alisema kuwa ni kweli mashamba yao yalichukuliwa kwa ajili ya upanuzi wa hospitali hivyo kutakiwa kupisha ujenzi huo kufanyika.
Turuka alisema kuwa kwa sasa maeneo hayo tayari yameshafanyiwa tathmini na taarifa ya uthamini imepelekwa wizarani kwa ajili ya kuandaliwa malipo baada ya kujua takwimu sahihi kutokana na maeneo hayo na kiasi ambacho watastahili kulipwa ili halmashauri itenge bajeti kwani maeneo mengine ambayo yalichukuliwa wamelipwa na wao watalipwa mara taratibu zitakapokamilika.
“Mthamini toka Tabora alishafika na kufanya kazi hiyo na kwa sasa tunachokisubiri ni taarifa toka wizarani baada ya kuipitia tathmini hiyo ili watu wanaodai fidia waweze kulipwa hivyo wanapaswa kuwa na subiri kwani mambo haya lazima yafuate taratibu na kila mtu atapewa haki zake pia eneo hilo  kwa sasa ni mji haipaswi kuwa na mashamba,” alisema Turuka
Aidha alisema wanasubiri taarifa hiyo ambayo itaonyesha ni kiasi gani wanastahili kulipwa na ndipo watatafuta fedha hizo kisha kuwalipa watu ambao wanadai ila wanataka walipwe haraka lakini serikali ina taratibu zake za kufanya malipo.
“Masuala ya malipo ya fidia za viwanja si suala la haraka linachukua muda mrefu hivyo lazima wawe na subiri wakati masuala yao yanashughulikiwa ambapo maeneo mengine tayari wameshalipwa hivyo na wao wanapaswa kuwa na subira na kila mtu atapata malipo yake,” alisema Turuka.
Mwisho.

     

Tuesday, August 26, 2014

Na John Gagarini, Kibaha
RAIA wa nchi ya Ethiopia Dawita Alalo (25) amekufa alipokuwa akipatiwa matibabu kwenye kituo cha afya cha Chalinze kata ya Bwiringu wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Marehemu alikuwa ni kati ya raia 48 wa nchi hiyo walikamatwa wakiwa kwenye msitu wa kijiji cha Visakazi Ubena Zomozi tarafa ya Chalinze Agosti 22 mwaka huu, baada ya kuingia nchini bila ya kibali.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kaimu kamanda wa polisi mkoani humo Mrakibu Mwandamizi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa marehemu ni miongoni mwa wahamiaji haramu 11 waliokuwa wamelazwa kituoni hapo wakipatiwa matibabu.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 26 majira saa 7:30 usiku alipokuwa akipatiwa matibabu kituoni hapo baada ya kuugua ugonjwa wa malaria.
Wakati huo huo mlinzi wa baa ya Silent Inn Jamat Mandama (55) amefariki dunia baada ya kunywa pombe nyingi bila ya kula chakula.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 27 mwaka huu majira ya saa 1 usiku huko Umwe kata ya Ikwiri wilayani Rufiji.
Aidha alisema kuwa mlinzi huyo alikutwa amekufa akiwa lindoni kwenye baa hiyo.
Na John Gagarini, Kibaha
ASKARI sita wa jeshi la polisi mkoani Pwani wamenusurika kifo kutokana na ajali ya barabarani baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongwa na lori la mizigo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kaimu kamanda wa polisi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa askari hao walikuwa doria.
Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 26 majira ya saa 9:30 usiku eneo la Maili Moja Ujenzi wailayani Kibaha barabara kuu ya Dar es Salaam Chalinze.
Alisema kuwa gari hilo lenye usajili namba PT 2012 lilikuwa likiingia kwenye kituo cha mafuta cha Delina na kugongwa na lori hilo lenye namba za usajili T 927 CAU na tela namba T 769 CJX.
“Lori hilo bada ya kuligonga gari hilo lapolisi kwa nyuma likaenda kugongana na lori lingine lililokuwa likielekea Jijini Dar es Salaam lenye namba T 672 BAC lenye tela namba T 672 BBW,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alibainisha kuwa askari watatu walijeruhiwa vibaya ambao ni namba F 4333 DC Tamimu ambaye amevunjika mguu wa kulia mara mbili, WP 6100 DC Jaqline ambaye amejeruhiwa kichwani na H 3348 DC Armand ambaye amejeruhiwa kichwani na kifuani.
“Askari wote wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi kwa matibabu zaidi ambapo tunaendelea kumtafuta dereva wa lori lililosababisha ajali hiyo,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Mwisho.

   

Sunday, August 24, 2014

PINGENI VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA

Na John Gagarini, Kibaha
WANAWAKE nchini wametakiwa kutokubali kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuhofia kutengwa na familia zao badala yake wawe watoa taarifa ili kuwadhibiti watu wanaoendeleza vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria na uvunjaji wa haki za binadamu.
Tabia ya kuficha ukatili wa kijinsia imesababisha wahusika kujikuta wakiathirika kutokana na vitendo hivyo ambavyo vimeshamiri kutokana na kuendelea kwa usiri ndani ya familia.
Hayo yalisema jana mjini Kibaha na mkurugenzi wa benki ya Wanawake Tanzania Magreth Chacha, wakati wa uzinduzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Mkoa wa Pwani (PWMO).
Chacha alisema kuwa baadhi ya wanawake wamekuwa wakificha vitendo hivyo vya kikatili ambavyo vimekuwa vikifanywa na baadhi ya wanaume wasiokuwa na huruma.
“Vitendo vya ukatili wa kijinsi vimekuwa vikifanywa ndani ya familia huku wanawake amabao ndiyo wahanga wa matukio hayo wamekuwa wakikaa kimya kuhofia kutengwa na familia zao jambo ambalo limesababisha vitendo hivi kuendelea,” alisema Chacha.
Alisema kuwa baadhi ya vitendo hivyo vimekuwa vikifanywa na watu wa karibu wa familia wakiwemo wanandoa na ndugu hali ambayo inasababisha taarifa hizo kufichwa huku walengwa wakiendelea kuathiriwa na vitendo hivyo viovu na vya ukatili.
“Baadhi ya vitendo hivyo ni pamoja na wanawake kupigwa, kutumikishwa kingono, kubakwa, watoto kubakwa, kulawitiwa, kufanyishwa kazi licha ya kuwa na umri mdogo na vitendo vingine vinavyokwenda kinyume cha sheria na haki za msingi za binadamu,” alisema Chacha.
Kwa upande wake mwenyekiti wa (PWMO) Mwamvua Mwinyi alisema kuwa lengo la kuanzishwa chama hicho mbali ya kutetea haki za waandishi wanawake pia ni kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ndani ya mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.
“Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku kutokana na baadhi ya wanajamii hususani wanawake kutokuwa katika kutoa taarifa za vitendo hivyo hali inayofanya kuongezeka kwa ukatili wa kijinsia,” alisema Mwinyi.
Aliiomba jamii kwa kushirikiana na vyombo vya sheria kwa kutoaa taarifa juu ya watu wanaofanya vitendo hivyo vya ukatili hususani maeneo ya pembezoni mwa miji, chama hicho kilianzishwa mwaka jana na kina jumla ya wanachama 15.

Mwisho.

MWANARIADHA AOMBA WAFADHILI AENDE KAMBINI KENYA

Na John Gagarini, Kibaha
MWANARIADHA John Mwandu wa mkoani Pwani amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia kwa hali na mali ili aweze kwenda kambini Eldoret nchini Kenya kwenye kambi aliyotokea mkimbiaji maarufu duniani David Rudisha wa nchi hiyo.
Rudisha ambaye ni bingwa wa dunia wa mbio za mita 800 amekuwa akiwandaa vijana wengi wa nchi ya Kenya kwa ajili ya kuinua vipaji vya vijana ambapo Mwandu ameomba kujiunga na kambi hiyo na tayari amekubaliwa kujiunga nayo kwa ajili ya mazoezi yam bio za mita 1,500.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha Mwandu alisema kuwa tayari ameruhusiwa kwenda kwenye kambi hiyo kwa mwaka mmoja lengo kubwa likiwa ni kujiandaa na mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2016 yatakayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil.
 “Lengo langu la kwenda Kenya ni kujifunza mbinu wanazozitumia katika mchezo huo na kuwafanya kuwa mabingwa wa dunia wa riadha, kwani Mungu akipenda Olimpiki ijayo nitahakikisha naiwakilisha nchi yangu na kuiletea medali kwani inawezekana na diyo sababu ya kuanza maandalizi mapema,” alisema Mwandu.
Alisema anatarajia kwenda huko mwezi Desemba mwaka huu kwa ajili ya kambi hiyo ambayo ni nzuri na imetoa wakimbiaji wengi na ana uhakika akifanikiwa kwenda huko atarudi akiwa na mbinu nyingi za ukimbiaji ambazo anaamini zitamfanya aweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali.
“Changamoto kubwa niliyonayo ni ukosefu wa fedha za kuweza kunipeleka kwenye kambi hiyo lakini naamini Mungu ataniwezesha kuweza kufanikisha kwenda kwenye kambi hiyo ambapo tayari nimeshafanya mawasiliano na Rudisha na ameahidi kunisaidia,” alisema Mwandu.
Aidha alisema kuwa Tanzania inashindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa kutokana na wachezaji wanaochaguliwa hawana uwezo na huchaguliwa kwa upendeleo na wale wenye uwezo kuachwa hali ianayosababisha kutofanya vizuri.
Alibainisha kuwa aliwahi kushinda kwenye mbio za Afrika Mashariki chini ya miaka 17 akiwa anasoma Tegeta High School alikuwa wa pili, Tabora Marathon kilomita 21, mashindano ya Voda Com kilomita tano ambapo alishika nafasi ya pili na Ruaha Marathon kilomita sita ambapo alishika nafasi ya tatu.
Mwisho.

Saturday, August 23, 2014

PWANI WAZINDUA CHAMA CHA WAANDISHI WA HABARI WANAWAKE (PWMO)

 mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Margareth Chacha akiongea wakati wa uzinduzi wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Pwani, kushoto ni mwenyekiti wa chama hicho Mwamvua Mwinyi na kulia ni mlezi wa chama Selina Koka. 


 mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoani Pwani Mwamvua Mwinyi akiongea wakati wa uzinduzi wa chama hicho uliofanyika mjini Kibaha kulia ni mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Maragareth Chacha

 mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Margareth Chacha katikati akionyesha hati ya busajili ya chama hicho kushoto ni mwenyekiti wa chama hicho Mwamvua Mwinyi na kulia mlezi wa chama Selina Koka.

 mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Margareth Chacha katikati akiongea wakati wa uzinduzi wa chama cha waandishi wa wanawake mkoani Pwani

 mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Margareth Chacha katikati akiakata utepe kama ishara ya uzinduzi wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoani Pwani kulia ni mlezi wa Selna Koka na kushoto mwenyekiti wa chama hicho Mwamvua Mwinyi

 mkurugenzi wa benki ya wanawake Tanzania Margareth Chacha akikata keki wakati wa uzinduzi wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Pwani 

 moja ya wadau wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Pwani akiongea kwenye uzinduzi wa chama hicho uliofanyika mjini Kibaha.

















 moja ya waandishi wa habari ambaye alikuwepo kwenye uzinduzi wa chama cha wandishi wa habari wanawake mkoani Pwani akichangia hoja 

 picha ikiwaonyesha viongozi na wadau wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoani Pwani wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa chama hicho

 wadau wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Pwani wakiongea na mgeni rasmi wa uzinduzi wa chama hicho Margareth Chacha 





 wadau wa chama cha waandishi wa habari wanawake mkoa wa Pwani wakibadilishana mawazo mara baada ya uzinduzi wa chama hicho.