Wednesday, August 21, 2024

DC KIBAHA ATAKA MADIWANI KUKAGUA NA SI KUTEMBELEA MIRADI YA MAENDELEO











MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Kibaha kukagua miradi ya maendeleo na siyo kuitembelea.

John ameyasema hayo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne Aprili hadi Juni kilichofanyika Mlandizi.

Amesema kuwa kukagua miradi ni tofauti na kutembelea ambapo unapokagua unaupata taarifa za kina tofauti na unapoitembelea.

"Tusitembelee miradi bali tuikague kwani pale tutapata fursa ya kujua mambo mengi tofauti na ukitembelea hupati taarifa za kina juu ya miradi ya maendeleo kwa wananchi,"amesema John.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Erasto Makala amesema kuwa wataongeza nguvu katika ukusanyaji mapato ili waweze kufikia malengo.

Makala amesema mafanikio kwenye ukusanyaji mapato ni mkubwa na kadri makusanyo yanavyoongezeka na miradi nayo inaongezeka hivyo kusogeza maendeleo kwa wananchi.

Wakati huo huo Baraza hilo limemchagua Diwani Halima Jongo kuwa makamu mwenyekiti baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Shomari Mwinshehe kumaliza muda wake.

Sambamba na uchaguzi huo wa makamu mwenyekiti ambaye alipata kura zote 17 pia kamati mbalimbali nazo zilichaguwa wenye viti wake.

Jongo alishukuru madiwani wenzake kwa kumchagua kwa kura nyingi na kusema atashirikiana nao pamoja na watumishi wa Halmashauri ili kuleta maendeleo kwa wananchi.


Sunday, August 18, 2024

TAKUKURU PWANI KUTOA ELIMU KUELEKEA UCHAGUZI


KATIKA kukabiliana na vitendo vya rushwa kwenye mchakato wa uchaguzí Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imejipanga kuzuia na kupambana na vitendo hivyo kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali.

Hayo yalisemwa na Naibu Kamanda wa Takukuru mkoani humo Ally Haji wakati akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha wanatarajia kuyafikia makundi yote yanayohusika na masuala ya uchaguzi.

Haji alisema kuwa baadhi ya makundi ni pamoja nan a vyama vya siasa, wasimamizi wa uchaguzi,
waandishi wa habari wananachi na jamii kwa ujumla.

"Kwa kipindi hichi cha mchakato wa uchaguzi tumeshaanza kufanya ufuatiliaji wa vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji utakaofanyika mwaka huu na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani,"alisema Haji.

Alisema kuwa wanatoa elimu ya madhara ya rushwa ambapo ni kosa kisheria endapo ikitumika
itasababisha kupatikana víongozi ambao siyo wazuri na hawataweza kuongoza wananchi kwa
weledi ambapo kauli mbiu inasema Kuzuia Rushwani Jukumu lako na langu Tutimize wajibu wetu. 

"Malengo ya kutoa elimu kwa makundi hayo ni kujiandaa kufanya uchaguzi usiokuwa na vitendo vya rushwa ili kupata viongozi bora wasiotokana na vitendo vya rushwa kwani ni adui wa haki na watu wote wana wajibu wa kupambana na vitendo hivyo,"alisema Haji.

Aidha alisema kuwa wataendelea kufanya udhibiti wa mapato ya serikali na usimamizi wa rasilimali za umma ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

"Tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za kufichua vitendo vya rushwa na wala rushwa kwa kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kuwachukulia hatua wahusika hasa katika kipindi hichi tunapoelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu,"alisema Haji.

Aliwataka watumishi wa umma na wa sekta binafsi watakeleze majukumu yao kwa kuzingatia sheria,
kanuni na taratibu za kazí zao ili kuzuia vitendo vya rushwa na kuleta tija katika kuhudumia wananchi ili
kuwaonyesha njia kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

mwisho.

Friday, August 16, 2024

MUHARAKANI/MKUZA WAITAKA TARURA KUBORESHA BARABARA YA MTAA HUO

KUFUATIA changamoto ya ubovu wa barabara ya Jamaika kupitia shule ya Filbert Bayi wakazi wa Mtaa wa Muharakani Kata ya Picha ya Ndege Wilayani Kibaha wameitaka Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kuifanyia matengenezo barabara hiyo ili kuwaondolea adha.

Wakizungumza na waandishi wa habari Mtaani hapo Mohamed Lukemo, Mathias John na Felix Swai walisema kuwa kutokana na ubovu huo umesababisha kalavati lililopo kwenye barabara hiyo kuwa hatarini kuvunjika ambapo kipindi cha mvua magari yalikuwa yakishindwa kupita.

Walisema kuwa barabara hiyo ilichongwa miaka sita iliyopita hali ambayo imeiacha barabara hiyo kwenye hali mbaya na kufanya wakazi hao kupata changamoto hasa kipindi cha mvua kutokana na kuwa na mashimo mengi.

"Tunawaomba Tarura waikumbuke barabara yetu kwani imeharibika vibaya sana na kwa wagonjwa ni changamoto kubwa sana hata magari yanayobeba wanafunzi yapita kwa taabu pale kwenye kalavati,"walisema wakazi hao

Aidha walisema magari yanapata ubovu na kwa wale wanaotumia pikipiki hupandishiwa nauli hasa kipindi cha mvua au wakati mwingine wanakataa kabisa kubeba abiria wanaopita barabara hiyo.

Ally Mohamed alisema kuwa wanashirikiana na wananchi ambapo wanajitolea kuikarabati barabara hiyo kwa baadhi ya maeneo korofi ili ipitike.

Mohamed alisema kuwa taarifa juu ya ubovu wa barabara hiyo wamezipeleka sehemu husika lakini utekelezaji ndo imekuwa changamoto ambapo waliambiwa wasubiri bajeti ya mwaka huu.

Naye meneja wa Tarura Wilaya ya Kibaha Mhandisi Samwel Ndoveni alikiri kuwa barabara hiyo ina changamoto lakini iko kwenye mpango wa kuchongwa.

Ndoveni alisema kuwa tayari wameshapeleka wataalamu kufanya tathmini na wiki ijayo watachonga barabara pamoja na kukarabati sehemu ya kalavati hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi.


Wednesday, August 14, 2024

SERIKALI YATAKIWA KUWA NA VITUO VYA KULEA VIPAJI VYA WACHEZAJI WA UMISSETA NA UMITASHUMTA ILI KUINUA MICHEZO NCHINI

SERIKALI imetakiwa kuwa na vituo vya kuwaandaa wachezaji wenye vipaji wanaoshinda kwenye michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA ili viweze kushindana kwenye mashindano ya kimataifa.

Aidha imetakiwa kuwezesha shule au vituo vya watu binafsi ambavyo vinakuza vipaji vya wanafunzi ili kuja kupata wanamichezo wenye uwezo na kuliletea sifa Taifa.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya ushiriki wa Tanzania kwenye mashindano ya Kimataifa hususani ya Olimpiki.

Bayi alisema kuwa ili kuwa na timu bora ambazo zitashindana kwenye mashindano za kimataifa lazima kuwe na vituo ambavyo vitawaandaa vijana mahiri ambapo wataandaliwa.

"Siri ya kufanya vizuri ni kuwa na vituo maalum au shule ambazo zitawachukua vijana hao ambao wanafanya vizuri kwenye mashindano hayo na kuwaandaa kwa muda mrefu ili waweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali ikiwa ni pamoja na Olimpiki,"alisema Bayi.

Alisema kuwa kuwe na uwekezaji kwenye kambi maalum siyo kwa ajili ya kushiriki mashindano makubwa bali kuwaandaa wale wenye vipaji ambapo kwa sasa hao wanaofanya vizuri haijulikani wanaenda wapi.

"Tuliambiwa kutakuwa na vituo au shule 56 lakini jatujui imeishia wapi kwani kwa sasa michezo inakwenda kisayansi ambapo wenzetu wamewekeza kwa vijana wao wenye vipaji ambap ndiyo wanaleta mafanikio,"alisema Nyambui.

Alibainisha kuwa fedha zinazorudishwa kwa wananchi kupitia uwekezaji zipelekwe kwenye masuala ya michezo ambapo asilimia tano ya michezo ya kubahatisha inapelekwa Baraza la Michezo BMT lakini ni ndogo inapaswa kuongezwa ili ilete matokeo.

"Kuna shule au vituo kama vile Allince, Kipingu, Makongo, Bagamoyo na Filbert Bayi ni sehemu ambazo zinafanya jitihada kuandaa vijana ni vema vikawezeshwa na serikali ili viweze kuandaa vizuri vijana kwani wanawagharamia vijana hao kwani wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha,"alisema Bayi.

 Akizungumzia timu iliyoshiriki mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika huko Ufaransa alisema wachezaji waliokwenda walikuwa na viwango vizuri lakini ilitokea tu bahati mbaya lakini waliandaliwa vizuri na kushinda au kushindwa ni matokeo tu.

WANANCHI PWANI WATAKIWA KUJITOKEZA KUJIANDIKISHA KUHAKIKI TAARIFA ZAO KWENYE DAFTARI LA MPIGAPICHA

 

WANANCHI Mkoani Pwani wametakiwa kujitokeza kwenye hatua za awali za kujiandikisha au kuboresha taarifa zao kwenye daftari la mpiga kura ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Vijana (YPC) Kibaha Israel Ilunde alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha.

Ilunde alisema kuwa Ypc imepeta mradi wa michakato ya uchaguzi (K-VOTE) ambao unawahamasisha uwepo wa vijana kwenye masuala ya umma, elimu ya mpiga kura, uraia, kuwapatia elimu vijana wanaotaka kuwania nafasi za uongozi.

"Usipojiandikisha hutaruhusiwa kupiga kura na viongozi wabaya huwekwa madarakani na raia wema wasiojitokeza kupiga kura hivyo kuna haja ya wananchi kutumia fursa hiyo ya kujiandikisha au kuboresha taarifa zao mara zoezi hilo litakapofanyika Mkoani Pwani,"alisema Ilunde.

Alisema kuwa vijana milioni tano wataandikishwa kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ambapo Tume Huru ya ya Uchaguzi iko kwenye uandikishaji na uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa ajili ya wapiga kura.

"Tutakuwa tukitoa elimu juu ya elimu ya mpiga kura kwa kushirikiana na mitandao mbalimbali lengo ni kuwahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi kwani ni haki yao ya msingi ya kuchagua au kuchaguliwa,"alisema Ilunde.

Aidha alisema pia elimu hiyo wataitoa ndani na nje ya shule na vyuo ambapo watawahamasisha hata wale ambao walijiandikisha lakini hawapigi kura kwani wasipopiga kura watachaguliwa viongozi ambao watawaamulia na watu wengine.

"Ushiriki wa vijana kwa mwaka 2004 uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2005 vijana walikuwa ni asilimia nane na uchaguzi wa 2015 waliongezeka na kufikia asilimia 50 na tunatarajia mwaka huu na mwakani wataongezeka,"alisema Ilunde.

Aliongeza kuwa vijana hao waligombea nafasi mbalimbali kuanzia serikali za mitaa, udiwani na ubunge na baadhi walichaguliwa kuwa Manaibu Mawaziri wakiwemo Dk Zainab Katimba, Salome Makamba ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum.

"Vijana wapambane kugombea nafasi husika lakini wasinunue kura kwani zinavunja heshima ya nchi na zinaliaibisha taifa kwani wakiingia kwa njia hiyo uongozi wao utakuwa wa kulipa madeni hivyo wafanye siasa safi za heshima na siyo za matusi,"alisema Ilunde.

Aliwataka watoe hoja kwa kuweka utu mbele kwa kuijali jamii na wajue kuwa kuna kushinda na kushindwa na wakubali matokeo kwa kutokufanya fujo ambapo TAMISEMI na Tume Huru ya Uchaguzi watasimamia vyema vyema uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.


Tuesday, August 13, 2024

WIZARA YA MAJI IMEJIPANGA MABWAWA YA MAJI NA TOPE SUMU YANAKIDHI VIGEZO.

 

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Wizara ya Maji kupitia Idara ya Rasilimali za Maji ina jukumu la kuhakikisha mabwawa ya maji na tope sumu yanakidhi vigezo vya usalama wa mabwawa kwa mujibu wa Sheria ya Rasilimali za Maji ili kuepusha madhara yatakayojitokeza katika jamii.

Hayo yamesemwa leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Maji uliopo Mtumba Jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema Wizara ya Maji imeandaa mafunzo ya siku mbili katika kuhakikisha usalama wa mabwawa ya maji na tope sumu unaimarishwa.

Aidha Mhandisi Waziri amesema kuwa mafunzo yatahusisha watalaam kutoka wamiliki wa migodi kwa ajili ya usalama wa mabwawa ya tope sumu, wamiliki wa mabwawa makubwa ya maji, wataalam wa mabwawa waliosajiliwa na wataalam kutoka Serikalini.

Sambamba na hayo Mhandisi Waziri ameongeza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa kushirikiana na Tanzania Chamber of Mines na yatafanyika mkoani Mwanza .

TAKUKURU PWANI YAOKOA BILIONI 1.6

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kutoka vyanzo mbalimbali vya Halmashauri ya Mji Kibaha.

Hayo yamesemwa na Naibu Kamanda wa Takukuru Mkoa huo Ally Haji wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha juu ya kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu.

Haji amesema kuwa walibaini hayo wakati wa ufuatiliaji wa ukusanyaji wa ushuru wa huduma kama mbalimbali kuna viashiria vya uvunjifu wa maadili kwa kushindwa kuwajibika.

"Katika ufuatiliaji tuligundua kuwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri kwenye kitengo cha ukusanyaji wa mapato watumishi kushindwa kufuata sheria, kanuni, na taratibu za ukusanyaji na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 1.6 zilizokuwa zinapotea,"amesema Haji.