Wednesday, August 14, 2024

WANANCHI PWANI WATAKIWA KUJITOKEZA KUJIANDIKISHA KUHAKIKI TAARIFA ZAO KWENYE DAFTARI LA MPIGAPICHA

 

WANANCHI Mkoani Pwani wametakiwa kujitokeza kwenye hatua za awali za kujiandikisha au kuboresha taarifa zao kwenye daftari la mpiga kura ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Vijana (YPC) Kibaha Israel Ilunde alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha.

Ilunde alisema kuwa Ypc imepeta mradi wa michakato ya uchaguzi (K-VOTE) ambao unawahamasisha uwepo wa vijana kwenye masuala ya umma, elimu ya mpiga kura, uraia, kuwapatia elimu vijana wanaotaka kuwania nafasi za uongozi.

"Usipojiandikisha hutaruhusiwa kupiga kura na viongozi wabaya huwekwa madarakani na raia wema wasiojitokeza kupiga kura hivyo kuna haja ya wananchi kutumia fursa hiyo ya kujiandikisha au kuboresha taarifa zao mara zoezi hilo litakapofanyika Mkoani Pwani,"alisema Ilunde.

Alisema kuwa vijana milioni tano wataandikishwa kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ambapo Tume Huru ya ya Uchaguzi iko kwenye uandikishaji na uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa ajili ya wapiga kura.

"Tutakuwa tukitoa elimu juu ya elimu ya mpiga kura kwa kushirikiana na mitandao mbalimbali lengo ni kuwahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi kwani ni haki yao ya msingi ya kuchagua au kuchaguliwa,"alisema Ilunde.

Aidha alisema pia elimu hiyo wataitoa ndani na nje ya shule na vyuo ambapo watawahamasisha hata wale ambao walijiandikisha lakini hawapigi kura kwani wasipopiga kura watachaguliwa viongozi ambao watawaamulia na watu wengine.

"Ushiriki wa vijana kwa mwaka 2004 uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2005 vijana walikuwa ni asilimia nane na uchaguzi wa 2015 waliongezeka na kufikia asilimia 50 na tunatarajia mwaka huu na mwakani wataongezeka,"alisema Ilunde.

Aliongeza kuwa vijana hao waligombea nafasi mbalimbali kuanzia serikali za mitaa, udiwani na ubunge na baadhi walichaguliwa kuwa Manaibu Mawaziri wakiwemo Dk Zainab Katimba, Salome Makamba ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum.

"Vijana wapambane kugombea nafasi husika lakini wasinunue kura kwani zinavunja heshima ya nchi na zinaliaibisha taifa kwani wakiingia kwa njia hiyo uongozi wao utakuwa wa kulipa madeni hivyo wafanye siasa safi za heshima na siyo za matusi,"alisema Ilunde.

Aliwataka watoe hoja kwa kuweka utu mbele kwa kuijali jamii na wajue kuwa kuna kushinda na kushindwa na wakubali matokeo kwa kutokufanya fujo ambapo TAMISEMI na Tume Huru ya Uchaguzi watasimamia vyema vyema uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.


No comments:

Post a Comment