IMEELEZWA kuwa moja ya sababu zinazosababisha maziwa ya akinamama wanaonyonyesha kushindwa kutoka ni msongo wa mawazo.
Aidha wanaume ambao wake zao wananyonyesha wameshsuriwa wasiwaudhi wake zao ili wasisababishe maziwa yashindwe kutoka na kushindwa kunyonyesha watoto wao.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Afya Amour Mohamed ambaye alimwakilisha mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha wakati wa Siku ya Unyonyeshaji Duniani kwa Halmashauri hiyo yaliyofanyika kwenye Zahanati ya Mwendapole.
Mohamed alisema kuwa baadhi ya wanaume wamekuwa wakiwasababishia wake zao wanaonyonyesha msongo wa mawazo hivyo maziwa kushindwa kutoka hivyo watoto kukosa maziwa.
"Wanaume tunapaswa tushiriki katika makuzi ua watoto wetu wachanga kwani ndiyo chakula chao kikuu ambapo moja ya changamoto ni maziwa kushindwa kutoka na moja ya chanzo ni wazazi kuwa na mawazo ambayo wakati mwingine husababishwa na waume zao,"alisema Mohamed.
Alisema kuwa wasiwaudhi wake zao katika kipindi hicho cha unyonyeshaji kwani hudababisha maziwa yasitoke na wanapaswa kuhakikisha wazazi wanapata lishe bora ili makuzi ya watoto yawe mazuri.
Naye Diwani wa Kata ya Kibaha Goodluck Manyama ambaye alikuwa Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo alisema kuwa maziwa ya mama ni muhimu tofauti na maziwa mengine.
Manyama alisema kuwa maziwa ya mama yana kinga nyingi kujikinga na maradhi kuliko ya ng'ombe au ya kopo lakini ya mama yana ubora na ukuzaji wa mtoto kwa haraka.
Kwa upande wake Muuguzi Mkuu na Kaimu Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Mji Kibaha Asteria Massawe alisema kuwa ndani ya saa moja mama aanze kumnyonyesha mtoto.
Massawe alisema kuwa yanayoanza kutoka ni maji hivyo lazima mtoto anyonye vya kutosha ili maziwa yaishe kabisa ndipo uhamishie ziwa lingine na amnyonyeshe mara 10 kwa siku au kila baada ya saa moja.
Akitoa maelekezo juu ya unyonyeshaji sahihi Muuguzi wa Zahanati ya Mwendapole Nyasungi Pepya alisema kuwa mtoto anapaswa kupata vipimo mara tano tangu mama akiwa mjamzito lengo ni mtoto azaliwe akiwa salama.
Pepya alisema kuwa vipimo husaidia kujua hali ya mama na kama akigundulika kuwa na maambukizi atapewa dawa ili kumlinda mtoto.
No comments:
Post a Comment