Sunday, August 4, 2024

YPC YAWATAKA VIJANA KUJITOKEZA KUWANIA NAFASI ZA UONGOZI

VIJANA wa kike na kiume wametakiwa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Vijana (YPC) ya Kibaha Israel Ilunde alipokuwa akizungumza na Habarileo ofisini kwake.

Ilunde alisema kuwa wameanzisha mradi uitwao (K-Vote) unaohamasisha ushiriki wa vijana kwenye masuala ya umma, elimu ya mpiga kura, uraia, kuwasaidia na kuwaelimisha vijana wanaotaka kuwania nafasi za uongozi kwenye chaguzi hizo.

"Tume Huru ya Uchaguzi inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya vijana milioni tano na wale ambao hawakuwahi kupiga kura miaka ya nyuma tunawasihi wajitikeze kuhakiki taarifa zao itakapofika muda wa kufanya hivyo ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi,"alisema Ilunde.

Alisema vijana wanapaswa kushiriki zoezi hilo ambalo ni muhimu sana kwani wasipojiandikisha au kuboresha taarifa zao watakuwa watazamaji na hawataruhusiwa kupiga kura.

"Idadi ya vijana kuwania nafasi mbalimbali za uongozi serikali za mitaa mwaka 2004 na uchaguzi mkuu mwaka 2005 ilikuwa ni asilimia 8 tu na mwaka 2015 iliongezeka na kufikia asilimia 50 na mwaka huu na mwakani itaongezeka,"alisema Ilunde.

Aidha alisema kuwa baadhi ya vijana hao walichaguliwa kwenye nafasi za uongozi ikiwa ni pamoja na ubunge, udiwani, wenyeviti na wajumbe wa serikali za mitaa.

"Tuna mfano wa Dk Zainab Katimba ni Naibu Waziri na mbunge Salome Makamba walifanya vizuri na pia kuachana na dhana kuwa uchaguzi mtaji ni fedha bali ni watu, nidhamu, uchapakazi, kujali watu,"alisema Ilunde.

Aliwataka vijana kutonunua kura kwani zinavunja heshima na zinaaibisha Taifa na uongozi unakuwa wa kulipa madeni pia wafanye siasa za heshima bali ziwe za hoja na kuweka utu mbele na kutofanya vurugu wanaposhindwa na waijali jamii.


No comments:

Post a Comment