MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Kibaha kukagua miradi ya maendeleo na siyo kuitembelea.
John ameyasema hayo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya nne Aprili hadi Juni kilichofanyika Mlandizi.
Amesema kuwa kukagua miradi ni tofauti na kutembelea ambapo unapokagua unaupata taarifa za kina tofauti na unapoitembelea.
"Tusitembelee miradi bali tuikague kwani pale tutapata fursa ya kujua mambo mengi tofauti na ukitembelea hupati taarifa za kina juu ya miradi ya maendeleo kwa wananchi,"amesema John.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Erasto Makala amesema kuwa wataongeza nguvu katika ukusanyaji mapato ili waweze kufikia malengo.
Makala amesema mafanikio kwenye ukusanyaji mapato ni mkubwa na kadri makusanyo yanavyoongezeka na miradi nayo inaongezeka hivyo kusogeza maendeleo kwa wananchi.
Wakati huo huo Baraza hilo limemchagua Diwani Halima Jongo kuwa makamu mwenyekiti baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Shomari Mwinshehe kumaliza muda wake.
Sambamba na uchaguzi huo wa makamu mwenyekiti ambaye alipata kura zote 17 pia kamati mbalimbali nazo zilichaguwa wenye viti wake.
Jongo alishukuru madiwani wenzake kwa kumchagua kwa kura nyingi na kusema atashirikiana nao pamoja na watumishi wa Halmashauri ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment