Friday, August 9, 2024

SELF MICROFINANCE WATAKA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Katika kuadhimisha kilele cha siku ya wakulima na wafugaji Nane Nane, Mfuko wa Fedha wa (SELF MICROFINANCE) ulio chini ya Wizara ya Fedha umewataka  wananchi wote wanaojishughulisha na shuguli za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kuchangamkia fursa za mikopo zinazotolewa na mfuko huo ili kukuza na kuongeza uzalishaji.

Wito huo umetolewa na Bi. Linda Mshana ambaye ni meneja masoko na uhamasishaji kutoka mfuko wa SELF wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la SELF lililopo katika maonesho ya Kitaifa ya Nanenane Jijini Dodoma.

Bi. Linda amesema, Mfuko huo una vifurushi mbalimbali kwaajili ya Wakulima, Wavuvi na wafugaji hivyo amewahimiza kujitokeza kwa wingi na kukopa mikopo hiyo ambayo imewekwa maalumu kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi.

Aidha,  Linda ameongeza kuwa mbali na Mikopo hiyo pia Mfuko wa Self unatoa Mikopo kwa taasisi ndogondogo za kifedha kwaajili ya kuwakopesha wakulima, wafugaji na wavuvi sambamba na mikopo mingine inayolenga kukuza uchumi wa watu mbalimbali.

"Self ina mikopo ya aina mbalimbali, tuna mkopo kwa ajili ya taasisi zinazokopesha, hivyo tunawakaribisha wakope na baadaye wawakopeshe wakulima, wafugaji na wavuvi,"amesema.

Linda amewakaribisha wananchi wote kutembelea banda lao lililopo katika maonesho hayo ili kupata elimu na kujua namna gani wanaweza kunufaika na Mikopo mbalimbali inayotolewa na Mfuko wa SELF.

No comments:

Post a Comment