Wednesday, August 7, 2024

FILBERT BAYI WATAMBA KUFANYA VEMA FEASSA

WANARIADHA tisa kutoka Shule ya Sekondari ya Filbert Bayi ambao wataiwakilisha nchi kwenye mashindano ya shule za sekondari Afrika Mashariki na Kati (FEASSA) yanayotarajiwa kufanyika mwezi huu nchini Uganda wameahidi ushindi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kukabidhi vikombe walivyoshinda huko Tabora kitaifa kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta ofisini kwake Mjini Kibaha mwalimu wa timu hiyo Ally Nyonyi alisema kuwa wanariadha hao ni wa mbio tofauti tofauti.

Nyonyi alisema kuwa wanariadha hao wanaendelea vizuri na mazoezi kwenye uwanja wa shule uliopo Kibaha Mkoani Pwani huku wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

"Wachezaji wetu tisa ambao walichaguliwa kwenye mashindano ya Umisseta yaliyomalizika hivi karibuni mkoani Tabora wanaendelea vizuri na mazoezi kwenye kambi iliyoko pale shule na wote wako vizuri,"alisema Nyonyi.

Alisema kuwa kambi inaendelea vizuri na hakuna mchezaji ambaye ana tatizo wote wako vizuri wanasubiri tu kuingia kwenye kambi ya mwisho itakayokuwa huko Tabora na mwaka huu wamejiandaa vizuri.

"Tangu mashindano ya Raidha ya Taifa yaliyofanyika mkoani Tabora timu iliingia kambini na hadi sasa inaendelea na mazoezi na hawana muda wa kusubiri kwani sisi ndiyo utaratibu wetu wa kufanya mazoezi kila siku,"alisema Nyonyi.

Aidha alisema kuwa wana mazoezi ya kutosha na wana morali ya hali ya juu na hakuna changamoto yoyote inayowakabili na wako vizuri wakiwa na afya nzuri.

"Sisi ni mabingwa wa Umisseta hapa nchini kwa miaka mitatu mfululizo siri kubwa ya wachezaji wangu kufanya vizuri ni nidhamu na kufuata maelekezo ya mwalimu na vifaa vipo mazingira ni rafiki,"alisema Nyonyi.

Aliomba wadau wa mchezo huo kuwaunga mkono kwa kuwasaidia baadhi ya vitu ikiwa ni pamoja na maji, matunda na motisha ili waweze kufanya vyema.

Kwa upande wa mwanariadha Emanuel Amos alisema kuwa amejipanga vizuri na anategemea kushinda kwani atahakikisha anafanya juhudi ili kufanikisha kushinda.

Amos alisema kuwa amepata uzoefu mkubwa kwani hayo yatakuwa mashindano yake ya pili ambapo mara ya kwanza hakuweza kufanya vizuri sana kwani ilikuwa ni mara yake ya kwanza kushiriki hivyo hakuwa na uzoefu.

Naye Elizabeth Kelaryo alisema kuwa wamejiandaa vyema na watavitumia vyema vipaji vyao na watahakikisha wanapambana kwani shuleni kwao wamefundishwa kupambana.

Kelaryo alisema kuwa wanajiamini na kikubwa ni ushirikiano walionao ndiyo unaowafanya waweze kufanya vizuri na maandalizi wanayoyafanya na mbinu bora za mwalimu wao watafanya vyema.

Wachezaji wanaounda timu hiyo ni Emanuel Amos anayekimbia mbio mita 100 na 200, Kimana Kibase 100 na 200, Wiliam Makaranga kupokezana vijiti mita 400, Yohana Samwel 400, Sharifa Mawazo kupokezana vijiti mita 400.

Wengine ni Eliza Kelaryo kutupa mkuki, Sara Masalu mita 1,500, Lucia Pius mita 400 kupokezana vijiti, Salma Samwel 800 na kupokezana vijiti mita 400.



 




No comments:

Post a Comment