WANAFUNZI wanaohitimu masomo ya kidato cha nne na darasa la saba nchini watakiwa kuepukana na tamaa na vishawishi ili visikatishe ndoto zao za kuendelea na masomo.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chuo cha Diplomasia Jacob Nduye wakati wa mahafali ya Darasa la saba na Kidato cha nne Shule za Filbert Bayi.
Nduye alisema kuwa ili wanafunzi hao waweze kufikia ndoto zao wanapaswa kujiepusha na tamaa na vishawishi ambavyo vimekuwa kikwazo kufikia kule walikopanga kufika.
"Epukeni tamaa na vishawishi na vitu ambavyo havina maadili kwani ili ufikie malengo yako unapaswa kukaa mbali navyo ili ufikie ndoto zako ambazo umejiwekea,"alisema Nduye.
Alisema kuwa wazazi wanawasomesha wanatumia gharama kubwa wanajinyima ili wasome lakini baadhi wamekuwa wakikatisha masomo kutokana na kujiingiza kwenye vishawishi.
"Nyie ni tegemeo la Taifa kwa siku za baadaye lakini ili muwe tegemeo lazima msome na kuachana na matendo yasiyofaa ndani ya jamii hivyo lazima mjilinde,"alisema Nduye.
Aidha alisema kuwa wazazi nao wanapaswa kuwalea watoto wao kwenye maadili mema na washirikiane na walimu katika kuwalea watoto ili wawe na maadili mema kwani ni viongozi wa baadaye.
Naye Mwenyekiti wa bodi Taasisi ya Filbert Bayi alisema kuwa mbali ya shule hizo kufanya vizuri lakini inakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara.
Bayi alisema barabara inayotoka Picha ya Ndege kwenda Jamaica na kutoka Jamaica kwenda Picha ya Ndege barabara hiyo ambayo inapita kwenye shule hizo ni mbaya na haijachongwa muda mrefu hivyo jamii inayozunguka shule inapata changamoto kubwa kwenda kupata huduma ya afya kwenye zahanati ya Bayi.
Akisoma risala ya wahitimu wa kidato cha nne Mariam Msabaha alisema kuwa mbali ya masomo ya kawaida pia walisoma masomo ya ujasiriamali ambayo yatawasaidia mara wamalizapo shule.
Msabaha alisema kuwa masomo hayo ni pamoja na ususi, mapishi, upambaji na utunzaji wa mazingira na masuala ya michezo ambapo shule imekuwa ikifanya vizuri kitaifa na kimataifa.
No comments:
Post a Comment