Wednesday, March 20, 2024

MAMLAKA ZA MAJI ZATAKIWA KULIPA MADENI YATOKANAYO NA TOZO

SERIKALI kupitia wizara ya Maji imezitaka Mamlaka za Maji zote  zinazodaiwa kuwasilisha deni la tozo zake ili kuiwezesha EWURA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi hii nikutokana na deni la tozo kwa Mamlaka za Maji kufikia takribani shilingi bilioni 4.6. 

Akizindua Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira kwa kipindi cha mwaka 2022/23 ambayo ni ya 15 kutolewa na EWURA, Mhandisi Mwajuma Waziri  Katibu Mkuu wa wizara ya Maji  amezitaka mamlaka hizo  zinazodaiwa ankara za maji  zilipe madeni yake mapema ili kuziwezesha kujiendesha na kuweza kutoa huduma kwa ufanisi.

"Kwa Mamlaka za Maji ambazo utendaji wake hauridhishi niseme wazi hatutasita kuzichukulia hatua, nafahamu kuwa baadhi zinashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za bei ya maji kuwa chini ikilinganishwa na gharama za uendeshaji". Amesema.

Aidha,Katibu mkuu huyo amewasisitiza watendaji wanaohusika katika usimamizi wa miradi ya Maji nchini kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Sheria.

"Kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi hii, wahakikishe wanaikamilisha kwa wakati'tunafahamu moja ya changamoto zinazoikabili sekta ya maji nchini ni pamoja na kuchelewa kutekelezwa kwa miradi,sitovumilia kuona hili likijitokeza katika miradi hii mikubwa na yenye maslahi makubwa  kwa taifa"Amesisitiza 

Licha ya hayo,ameziagiza Mamlaka za Maji kushirikiana na  Halmashauri zote za Wilaya kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua katika ngazi zote hasa katika kipindi hiki ambapo mvua zinaendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.

"Tumejionea mvua hizi katika baadhi yua maeneo zimeleta madhara makubwa, hivyo basi,endapo tutavuna maji haya tutapunguza kama siyo kuondoa kabisa athari zake na pia  kutaiwezesha nchi yetu na wananchi kuwa na akiba ya maji ambayo yatatusaidia kipindi cha ukame". Amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt. James Andilile amesema taarifa iliyozinduliwa leo ni ya 15 tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo miaka 18 iliyopita na inahusisha uchambuzi wa utendaji wa mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira 85 zikiwemo; mamlaka 25 za mikoa, saba (7) za miradi ya kitaifa, 47 za wilaya na Sita (6) za miji midogo.

Dkt.Andilile amesema  Utendaji wa mamlaka za maji na usafi wa mazingira umeendelea kuimarika ambapo kwa mwaka 2022/23, Mamlaka za Maji 78 kati ya 85 zilipata alama kuanzia wastani hadi vizuri sana katika utendaji wa ujumla ikilinganishwa na mamlaka 77 kati ya 90 kwa mwaka 2021/22.

Ameyataja Maeneo yaliyoimarika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2021/22 kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha maji yaliyozalishwa kutoka mita za ujazo milioni 393 hadi 400 sawa na asilimia 1.8 , kuimarika kwa uwiano kati ya watumishi na wateja kutoka 4.2 hadi 3.8 kwa kila wateja 1000 , kuimarika kwa Uwiano wa maunganisho yaliyofungwa dira za maji kufikia asilimia 92 ikilinganishwa na asilimia 90 ,kuongezeka kwa kiwango cha ubora wa maji yanayosambazwa kwa wateja kutoka asilimia 91 hadi 94;

Maeneo mengine ni kuongezeka kwa wateja wa maji wa majisafi kutoka kutoka 1,385,485 hadi 1,532,362 sawa na asilimia 11 na kuongezeka kwa wateja wa mtandao wa uondoaji majitaka kutoka wateja 55,996 hadi wateja 56,899 sawa na asilimia 16.

“Nafahamu kuwa mafanikio hayo hayakuja bure. Naomba nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wewe Mheshimiwa Waziri kwa usimamizi wako mahiri wa sekta ya maji kwa kufanya uwekezaji mkubwa kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani na kuimarisha ustawi wa watanzania wote, kwani maji ni uhai,” amesema Dkt. Andilile

Uzinduzi huo umekwenda sambamba na utoaji wa tuzo mbalimbali Kwa Mamlaka zilizofanya vizuri huku zikigawanywa katika makundi Matatu tofauti kulingana na idadi ya wateja inayowahudumia ambapo kundi la kwanza ni Mamlaka za maji zenye wateja chini ya 5000, kundi la pili ni mamlaka za maji zenye wateja chini kati ya 5000 na 20,000 na kundi la Tatu ni mamlaka za maji zenye wateja zaidi ya 20,000.


Tuesday, March 19, 2024

WANANCHI MSANGANI WATAKIWA KUMCHAGUA CHONGELA KUWA DIWANI

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani Jackson Kituka amewataka wananchi wa Kata ya Msangani kumchagua mgombea Udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Gunze Chongela kwenye uchaguzi mdogo utakaofanyika kesho Machi 20.

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wa kata ya Msangani Wilaya ya Kibaha Leonard Mlowe kufariki dunia hivi karibuni.

Kituka ameyasema hayo wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo kwenye uwanja wa Juhudi Msangani.

Amesema kuwa wamchague mgombea huyo wa CCM kwani ni mchapakazi mwadilifu na mwaminifu na wasipoteze muda kuchagua wagombea wa vyama vingine.

Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka amesema kuwa mgombea huyo ndiyo chaguo sahihi katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa kata hiyo.

Nyamka amesema kuwa diwani aliyefariki aliacha mipango mingi ya maendeleo ambayo lazima iendelezwe na diwani anayetokana na CCM hivyo wasipoteze muda kuchagua mgombea wa chama kingine.

Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba amesema kuwa Kata hiyo imetengewa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 900 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Ndomba amesema kuwa fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya miradi mbalimbali kwenye sekta mbalimbali za kijamii.

Mkutano huo uliwahusisha madiwani viongozi wa chama wa ngazi mbalimbali na wanachama wa CCM pamoja na mbunge wa viti maalum Dk Allice Kaijage.

Monday, March 18, 2024

SERIKALI KUIWEZESHA SEKTA YA MADINI KUONDOA CHANGAMOTO WACHIMBAJI WADOGO WADOGO


 Na Wellu Mtaki, Dodoma 

Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuiwezesha sekta ya madini kwa kuchangia asilimia 10 kwenye pato la Taifa ifikapo mwaka 2025 kwa kuondoa changamoto zote zinazowakabili wachimbaji wa madini wadogo wadogo ili kuwezesha shughuli hiyo kuendelea kukua na kukuza uchumi wa nchi ambapo mpaka sasa mchango wa sekta ya madini kwenye pato la nchi umeongezeka kufikia asilimia 9.7

Akizungumza na waandshi wa habari  jijini Dodoma Mkurugenzi wa taasisi ya Tanzanite Fashion na Miss Utalii Eva Raphael amesema madini ya Tanzanite ambayo mauzo yake hufikia mpaka Dola Milioni hamsini kwa mwaka ndiyo upekee  wa kuadhimisha shughuli yetu hi Tanzanite Fashion week.

Aidha amesema kuwa kutakuwa  na  tamasha kubwa la Kitaifa la Tanzanite Fashion week linatarajiwa kufanyika tarehe 4 mwezi 5 Mwaka 2024 jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mabeyo Complex. tamasha hilo litaenda kutangaza Utalii wa Madini na Mali asili mbalimbali zilizopo hapa nchini.

"Tunapenda kuwaalika wachimbaji mbalimbali wa Madini, wachimbaji Wanawake na vyama vyao vyote vya Madini, taasisi mbalimbali za kiserikali na binafsi kwenda kushirikiana na sisi katika wiki ya Tanzanite Fashion"Amesema

Aidha amesema kuwa wiki hiyo ni wiki iliyojaa Maudhui mengi,mafundisho pamoja na dhamira nyingi ya kwenda kuigusa jamii na kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Naye Afisa Utamaduni Wizara ya Utamaduni Sana na Michezo Alice John amempongeza Eva kwa ubunifu huo wa kuandaa tamasha hilo na kusema kuwa anaenda kuieleza na kutumia sanaa kama njia bora ya kufikisha ujumbe

"Tunamshukuru dada Eva kwa kuiona sanaa ni njia bora na anakwenda kutumia Sanaa kutangaza Madini"Amesema John

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kanzidata ya madini taasisi ya Jiologia na utafiti wa madini amesema kuwa Madini ya Tanzanite ndo Madini pekee yanayopatikana hapa nchini ndo maana ameyachagua katika wiki ya Tanzanite Fashion week tumeona ni vema kumuunga mkono ili tuweze kuyatangaza madini na Wizara ya Madini imeona  frusa hii ni bora kwa wachimbaji wadogo Wanawake.

UMOJA WANAWAKE VIONGOZI WATOA MSAADA HOSPITALI YA RUFAA DODOMA GENERAL

Na Wellu Mtaki, Dodoma 

Umoja wa Wanawake Viongozi na Viongozi wanaochipukia kutoka Taasisi mbalimbali (ESWLT) umetoa msaada wa vifaa mbalimbali katika 

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma General imepokea msaada wa vifaa mbalimbali kutoka  Umoja wa Wanawake Viongozi na Viongozi wanaochipukia kutoka Taasisi mbalimbali (ESWLT)   ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo Hospitalini hapo na kutembelea katika wodi ya wakinamama Katibu wa Umoja huo Sakina Mwinyimkuu amesema kuwa kitendo cha kutoa vifaa hivyo ni miongoni mwa malengo yao ya kusaidia jamii.

Aidha amesema kuwa Umoja huo una lengo la kusaidia vijana Wanawake hasa mabinti ambao wanatarajia baada ya miaka kadhaa wataingia katika Utumishi katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kusaidia jamii.

Pia ameongeza kuwa Kwa kupitia umoja huu wanawasaidia na kuwalea ili waweze kuwa wazalendo katika nchi pamoja na kulenga kutumia viongozi waliostaafu kwa kupata mazuri ambayo wamefanya na niwazoefu na kwa kupitia wao watajifunza zaidi katika eneo la uongozi

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt.Grace Magembe ameushukuru umoja wa Wanawake hao kwa kuchagua eneo hilo kutoa msaada huo kwa sababu eneo walilolichagua ni eneo nyeti

"Kina mama wanaojifungua pamoja na watoto wao wanahitaji Sana mashuka ambayo safi ili kuzuia maambukizi ya magonjwa"Amesema

Aidha amewaahidi Wanawake wa Umoja huo kwa niaba ya Wizara ya Afya kuwa wataendelea kujituma,na Siku nyingine wasisite kwenda kutoa msaada.

Sunday, March 17, 2024

*MAKARANI WAONGOZAJI WA UCHAGUZI WAFUNDWA;KIBAHA*

 


Na Byarugaba Innocent,Kibaha

Ikiwa imesalia siku tatu tu kabla ya Uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Msangani Jimbo la Kibaha Mjini unatarijiwa kufanyika Siku ya Jumatano tarehe 20 Machi,2024.

Mapema Machi 16,2024  Makarani waongozaji wamepata Mafunzo pamoja na kuapa kiapo cha kutunza Siri Chini ya Kanuni ya 16(1) (a) na 50 (4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge,2020 na Kanuni ya 14 (1)(a),(2) na 43(4) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani),2020 Mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Salum Papen.

Aidha,Mafunzo hayo yametolewa na Maria Israel,Benjamin Mputtu wakisaidiana na Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Optuna Kasanda ambao wamewasisitiza kwenda kufanyakazi kwa kuzingatia Sheria,Kanuni na taratibu za Uchaguzi

Akifungua Mafunzo hayo,Msimamizi wa Uchaguzi,Mwanasheria nguli wa Mahakama kuu na zilizochini yake Salum Papen amesema.." _Tume imewateua ninyi kwa mujibu wa sheria na Kwa kuzingatia uzoefu wenu katika masuala ya Uchaguzi_ "katendeni haki amesisitiza Papen

Papen ametoa rai kwa Makarani waongozaji kujiamini na kujitambua,kufanyakazi kwa kuzingatia Katiba ya Nchi,Sheria za Uchaguzi na Kanuni zake,Maadili ya Uchaguzi na Maelekezo mbambali yanayotolewa na Tume

Katika hatua nyingine Makarani wametia tamko la kujitoa uanachama au kutokuwa na Chama cha Siasa chini ya Kanuni ya 16 (1)(b) na ( 3 ) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge,2020 na Kanuni 14(1) (b) na (3) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,(Uchaguzi wa Madiwani),2020 mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi,Mwanasheria Salum Papen

Aidha,Andrea Isamaki Ofisa kutoka Tume ya Taifa ya  Uchaguzi (NEC) ameshiriki kushuhudia Mafunzo,kiapo cha kutunza Siri na tamko la kujitoa uanachama kwa Makarani waongozaji


Nadia Issa na Benson Shawa,Makarani waongozaji wamesema wanakwenda kufanya kazi kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia Sheria,Kanuni na taratibu za Uchaguzi 


Uchaguzi mdogo Kata ya Msangani unafanyika kutokana na kifo cha Mhe.Leonard Mlowe kilichotokea tarehe 23 Disemba,2023 ambapo jumla ya vyama nane (8) vya Siasa vinatarajia kushiriki.

Friday, March 15, 2024

BAADHI YA WANAWAKE WAFANYIWA UKATILI NA WENZA WAO

 Na Wellu Mtaki, Dodoma 

Tafiti zilizofanywa nchini Tanzania zinaonesha kuwa asilimia  40 za wanawake waliopo kwenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia ikiwemo kupigwa, kukatwa viungo  na kuchomwa moto ambapo kati ya wanawake 100 , 40 wameumizwa na wenza wao .

Aidha chimbuko la ukatili huo ni ukosefu wa kutambua usawa  kati ya wanawake na wanaume, ikiwa ni imani na mazoea kwamba ukatili wa kijinsia unakubalika ndani ya jamii

Tafiti hizo zimetolewa na Kaimu Kamishna Wizara ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Tullo Masanja katika siku ya utepe mweupe ambapo uhadhimishwa kila mwaka ifikapo March 15 .

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uchechemuzi na Mawasiliano  Save The  Children  Victoria  Marijani amesema kuwa katika kuunga juhudi za Serikali

Wanashirikiana na serikali katika kuhakikisha watoto wanatambua haki zao za msingi pamoja na kutambua  maeneo ya kwenda Kutoa Taarifa endapo watafanyiwa vitendo vya ukatili.

"Lengo ni kumfanya mtoto apate haki ya kuishi,haki ya kulindwa, haki ya kujifunza na kupata lishe iliyo bora ili Taifa liwe na rasilimali watu ambao wenye nguvu na tija". amesema Masanja 

Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya watoto na vijana Save The Children Tanzania Nancy Kasembo amesema kama Bodi ya ushauri anawakilisha vijana katika kutoa maoni chanya na masuala ya ukatili namna gani watoto na vijana kuwa vinara wa kupinga ukatili lakini pia wakatoa Elimu kwa vijana na watoto wakapaza sauti zao katika kuhakikisha wanatengeneza Taifa lililobora na imara.

Kauli mbiu ya  mwaka huu inasema kujenga kizazi kilicho salama kwa kukomesha ukatili wa kijinsia na watoto Tanzania kwa kupitia vijana wa shule.

TUENDELEE KUUNGANA KUKABILIANA NA MAAFA NCHINI” MKURUGENZI MSAIDIZI JANE

NA MWANDISHI WETU,DODOMA

Mkurugenzi Msaidizi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Jane Kikunya amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau mbalimnali katika masuala ya uratibu wa maafa nchini ili kuendelea kuwa na stahimilivu na maafa. 

Ameyasema hayo wakati akifungua Warsha ya siku moja iliyowakutanisha wadau kutoka Serikalini, Makampuni ya simu, Taasisi zinazotoa Misaada ya kibinadamu kwa lengo la kujadili fursa na kutoa maoni kuhusu njia sahihi ya ujumuishaji wa teknolojia ya simu katika mifumo ya kutoa tahadhari ya Awali (Early Warning System – EWS) iliyofanyika tarehe 14 Machi, 2024 Jijini Dodoma.

Warsha hiyo ilihudhuriwa na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maji, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo pamoja na Taasisi ikiwemo TCRA, TMA, REDCROSS, makampuni ya simu pamoja na Airtel, Vodacom, Tigo/Zanztel.

Aidha alitumia fursa hiyo kueleza majukumu ya msingi ya Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ni kuratibu masuala ya menejimenti ya maafa nchini huku akiwaasa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika mzingo wa menejimenti ya maafa ikiwemo wa kuzuia, kujiandaa, kukabili pamoja kurejesha hali pindi maafa yanatokea.

“Tumienie warsha hii kwa matokeo chanya yaliyokusudiwa kwa kuongeza ujuzi na kushirikishana uzoefu katika masuala yanayohusu fursa mbalimbali kuhusu njia sahihi za kutumia teknolojia ya simu katika mifumo na kutoa taarifa za tahadhari za awali ili kuendelea kuwa na utayari katika kukabili maafa,” alieleza Bi. Jane

Aliongezea kuwa nchi ya Tanzania imekuwa ikikumbwa na maafa ya asili na yale yasiyo ya asili ikiwemo ya mafuriko, matetemeko ya ardhi, moto, maporomoko ya tope na mawe, ukame, upepo mkali, magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama hivyo warsha hiyo ni muhimu kwa kuzingatia umuhimu wa taarifa za tahadhari za awali ili kuendelea kujiandaa kisha kukabili kwa wakati na kupunguza madhara yanayoweza kutokea wakati wa maafa hayo.

Alifafanua kuwa, taarifa za awali zinaipa jamii uelewa wa hatua za awali za kuchukua kabla ya madhara ya maafa kuwa makubwa hivyo upo umuhimu wa kuendelea kuzijengea uwezo jamii juu ya matumizi sahihi ya taarifa hizo.

Awali aliwakumbusha kuendelea kupiga namba 190 endapo kunatokea majanga, maafa au dharura ili kupata msaada zaidi kupitia Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu.