Sunday, February 25, 2024

NEC YATOA VIBALI VYA ELMU YA MPIGA KURA NA WATAZAMAJI WA UCHAGUZI MDOGO WA UDIWANI KATA 23.

 

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika kikao chake cha tarehe 24 Februari, 2024, kilichofanyika katika Ofisi za Tume Jijini Dodoma imetoa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mdogo wa Udiwani katika kata 23 za Tanzania Bara utakaofanyika tarehe 20 Machi, 2024 kwa asasi za kiraia 11.

Kwa Mujibu wa Taarifa kwa Vyombo vya Habari iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima, R. K imeainisha Asasi za kiraia 11 ambazo zimekidhi vigezo na kupewa vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura pamoja na kata walizoomba kutoa elimu  hiyo kuwa ni Mbogwe Legal Aid Organization (MBOLAO) Isebya iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe, Sustainable Hub for Policy Initiatives (SHPI) Mshikamano iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.

Asasi zingine ni Promotion and Women Development Association (PWDA) Kasingirima iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Bagamoyo Community Capacity Empowerment and Education (BCCEE) Fukayosi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Action for Democratic Governance (A4DG) Kimbiji iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni.

Asasi zingine ni Vanessa Foundation ambayo itatoa elimu katika kata ya Nkokwa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Tanzania Centre for Disability Development Initiatives (TCDDI) Nkokwa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Safe Society Platform Tanzania (SSPT) Busegwe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama na Isebya iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe

Asasi zingine za kiraia zilizopata kibali ni Youth Against Aids and Poverty Association (YAAPA) ambayo itatoa elmu katika kata ya Kasingirima iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Musoma Municipal Paralegal Organisation (MMPO) Mshikamano iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma.

Asasi nyingine iliyopata kibali ni Shirika la Elimu ya Uraia na Uzalendo “Civic Education and Patriotism Association” iliyoomba kutoa Elimu katika kata za Kimbiji iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, Msangani iliyopo katika Halmashauri ya Mji Kibaha, Fukayosi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Mlanzi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti na Kibata iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.

Wakati huo huo, Tume pia imetoa kibali kwa asasi za kiraia tatu ambazo zimekidhi vigezo ili ziweze kutazama uchaguzi mdogo wa Udiwani katika Kata 23 za Tanzania Bara.

Asasi hizo tatu zitakazoenda kutazama uchaguzi Mdogo wa udiwani siku ya Jumatano tarehe 20 Machi, 2024 ni Tanzania Alliance for Disability Development Initiatives itakayokuwa katika kata ya Mhande iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Bridge Development Trust Organisation itakuwa katika kata ya Buzilasoga iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na Promotion and Women Development Association itayokuwa katika Kata ya Kasingirima iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji.

Aidha, katika kikao hicho, Tume imezitaka asasi za kiraia zilizopata kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura, kuzingatia Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura wa Mwaka 2020 katika kipindi chote cha kutoa elimu hiyo katika uchaguzi mdogo.

MAMA KOKA AFANYE KWELI AGAWA DOTI ZA VITENGE KUELEKEA SIKU YA MWANAMKE DUNIANI

 

NA MWANDISHI WETU

Mke wa Mbunge wa  Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka  amegawa doti za  sare 125 za vitenge  kwa ajili ya sherehe za maadhimisho ya siku ya  Mwanamke Duniani zilizogharimu kiasi cha shilingi milioni 2.

Sare hizo ambazo zimegawiwa katikka makundi mbali mbali ikiwemo Jumuiya ya wazazi, Wajumbe wa Baraza la UWT Kibaha Mjini, Wajumbe Wanawake wa Baraza la Wazazi la Wilaya, Wajumbe wanawake wa Baraza la UVCCM Kibaha Mjini Pamoja na Wajumbe Wanawake wa Halmashauri kuu ya CCM Wilaya Kibaha Mjini. 

Akikabidhi sare hizo kwa niaba ya Mama Selina Koka Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mji Method Mselewa  amesema huu ni Utaratibu wa Ofisi ya Mbunge kupitia kwa Mama Koka kugawa sare kwa wanawake kila mwaka na kila zinapofika Sherehe hizo pamoja na Makongamano mbalimbali. 

Kwa Upande wake Mama Selina Koka akizungumza katika mahojiano maalumu kwa njia ya simu alisema kwamba ameamua kutoa sare hizo kwa lengo la kuungana na wanawake wenzake katika kusherekea kwa pamoja siku hiyo.

"Nimetoa sare zipatazo 125 kwa ajili ya  makundi mbali mbali ya wanawake,ikiwemo kundi la Uwt,Uvccm,Wazazi,pamoja na chama chenyewe cha Ccm  ambapo wao ndio watawakilisha wanawake wengine wote wa Jimbo la Kibaha mjini,"alisema Selina Koka.

Mama Koka alisema kwamba amekuwa akishirikiana bega kwa bega na wanawake wenzake katika mambo mbali mbali ya kijamii ambayo yamekuwa yakifanyika ikiwemo hili la kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Pia aliahidi kuendelea kushirikiana kwa dhati na wanawake wenzake na kuwatakia kila la kheri katika sherehe hizo ambazo kiwilaya zinatarajiiwa kufanyika machi 5 mwaka huu mjini Kibaha.

Mama Koka  alifafanua kwamba ameamua kutumia jumuiya  hizo ikiwa kama wawakilishi wa wanawake wengine wote wa Jimbo zima  la Kibaha mjini kwani sio rahisi kwa kila mmoja kupata sare hiyo kwa ajili ya sherehe hizo.

Katika hatua nyingine amesema kwamba anawapenda wanawake wote na kwamba wajitokeze kwa wingi siku hiyo kwa ajili ya kusherekea siku yao ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuonana na kubadilishana mawazo.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya umoja wa wanawake (UWT) Wilaya ya Kibaha Mjini Elina Mgonja amemshukuru kwa dhati Mama Koka pamoja na  Mbunge kwa kujali wanawake wa Kibaha na kwamba tunapaswa kumtia moyo.

Mgonja alisema kwamba wanawake wa Kibaha wamepata Mama ambaye amekuwa ni mstari wa mbele katika kusaidia mambo mbali mbali ya kijamii pamoja hivyo anastahili sifa  na kumthamini.

"Kwa kweli  tumefarijika sana kupokea sare hizi za vitenge kiukweli mama Selina koka ni mfano wa kuigwa kutokana na kuonyesha mashirikiano na mahusiano mema katika kila jambo,"alisema Mgonja.

Aidha Mwenyekiti Mgonja alisema kwamba Mama koka amekuwa ni kichocheo kikubwa katika kila nyanja ikiwepo sambamba na kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapatia mitaji na fedha.

Naye Katibu wa UWT Cecilia Ndalu amesema kuwa kitendo cha Mama Koka kujali wanawake ni kitendo cha kipekee sana  kwani kuwa mke wa Mbunge hawajibik kwa wanawake moja kwa moja lakini amejigusa na kujali sana. 

Wajumbe wengi waliopokea sare hizo wameendelea kuishukuru familia ya Mhe Koka kwa kujitoa na wameahidi kuendelea kumuunga mkono Mhe Koka katika kuhakikisha shughuli zake za utekelezaji wa ilani unaenda vyema. 

Sherehe za Mwanamke zinaadhimishwa Duniani kote na kwa upande wa  Kibaha Mjini kilele kitakuwa siku ya tarehe 05/03/2024 katika viwanja vya Mailimoja. 



        MWISHO

Saturday, February 24, 2024

SHULE YA EL-SHADDAI YAWASHIKA MKONO WATHIRIKA WA MAAFA HANANG.

 

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

UONGOZI wa shule ya Msingi  El shaddai  iliyopo Dodoma umekabidhi misaada ya kibinadamu ikiwemo mchele, unga, maharagwe, nguo, dawa za meno na vyombo mbalimbali vya kupikia kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope, mawe na miti kutoka mlima Hanang’ yaliyotokea tarehe 3 Disemba 2024 mkoani Manyara.

Akipokea misaada iliyotolewa na shule hiyo tarehe 23 Februari, 2024 kwaniaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi,  Kaimu Mkurugenzi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Jane Kikunya amesema Ofisi inatambua mchango mkubwa wa Taasisi zinazoendelea kushiriki katika kurejesha hali kwa waathirika wa maafa hayo kwa namna wanavyoendelea kutoa misaada mbalimbali ili kusaidia hatua ya urejeshaji hali inayoendelea.

"kipekee kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu naomba kuwashukuru kwa moyo mliouonesha na nia katika kuchangia na kutoa msaada kwaajili ya waathirika wa maafa, tunashukuru kwa Shule yenu kwa kujitokeza na kuchangia misaada muhimu kwaajili ya waathirika wa Hanang, misaada iliyotolewa itawafikia waathirika wote kwa utaratibu uliowekwa na Ofisi."alisema Bi. Jane Kikunya.

Alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea kurejesha hali za waathirika wa maafa hayo yaliyosababisha vifo, uharibifu wa makazi, miundombinu ya barabara, umeme na mashamba, huku akitoa wito kwa wadau kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kufanikisha hatua zilizopo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shule hiyo  Bi. Juliana Kallinga amesema uongozi wa shule na wafanyakazi wa shule hiyo wameandaa baadhi ya vitu ambavyo ni ishara ya kuwafariji waathirika hao.

"Kama familia ya El-Shaddai tunapenda kuwafariji Watanzanaia wenzetu walioathirika kwa kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo mchele, unga, maharagwe, nguo mbalimbali kwa wakubwa na wadogo, dawa za meno na vyombo mbalimbali vya kupikia,lakini pia tunamuomba Mungu aendelee kuwapa mfaraja na nguvu kila aliyepotelewa na ndugu jamaa na marafiki, hakika shule yetu iliguswa na changamoto hii."alisema Bi. Juliana.




CAPTIONS


P 1.

Kaimu Mkurugenzi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bi. Jane Kikunya akizungumza mara baada ya kupokea msaada ya kibinadamu kutoka kwa uongozi pamoja na walimu wa shule ya Msingi El-shaddai Februari 23, 2024 Jijini Dodoma.



P 2.

Mkurugenzi wa Shule ya Msingi  El-shaddai Bi. Juliana Kallinga akisoma taarifa ya msaada waliyoitoa kwa waathirika wa maporomoko ya tope, mawe na miti Wilaya ya Hanang’ mkoani Manyara.



P 3.

Mkurugenzi Idara ya Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Condrad Millinga akipokea taarifa msaada iliyosomwa na Mkurugenzi wa Shule ya Msingi  El-shadai Bi. Juliana Kallinga.


P 4.

Baadhi ya vitu vilivyopokelewa ikiwemo mchele, unga, maharagwe, nguo, dawa za meno na vyombo mbalimbali vya kupikia kwa ajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope, mawe na miti kutoka mlima Hanang’.


(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Friday, February 23, 2024

KIJANA WA KITANZANIA AGUNDUA MFUMO WA KITAALUMA KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA MSINGI HADI CHUO KIKUU

NA WELLU MTAKI Dodoma.

KIJANA wa Kitanzania Alpha Mbennah mwenye taaluma ya Uhandisi amegundua Mfumo wa Uchakataji,Uhifadhi na Uandaaji wa Taarifa za Kitaaluma za wanafunzi kuanzia ngazi ya Elimu msingi mpaka Vyuo Vikuu uitwao "SPIN-ED Academic Performance Management System utakaowezesha kuleta ufanisi katika kazi.

Akizindua mfumo huo  Jijini Dodoma katika Mkutano wake na Wanahabari Mhandisi Mbennah amesema kuwa mfumo huo unamruhusu mwalimu katika ngazi tajwa kuweza kukusanya na kuingiza alama za mwanafunzi aliyesajiliwa katika mfumo kisha huchukua alama hizo na kuzichakata kwa kutengeneza wastani uliopimwa au usiopimwa kubaini gredi ya alama hizo, yaani A, B, C, n.k.

“Pia huu mfumo unaweza kubaini wastani wa darasa husika, nafasi aliyoshika kila mwanafunzi katika somo husika na katika darasa kwa ujumla pamoja na kutengenza ripoti ya maendeleo ya kitaalamu kwa kila mwanafunzi aliyesajiliwa kwenye mfumo, katika darasa husika, kutoa maoni ama comments zinazohusiana na ufaulu wa mwanafunzi na kuchora grafu ya maendeleo ya kitaaluma kwa kila mwanafunzi".

Mbenah amesema kuwa vyote hivyo hufanywa moja kwa moja huku akisema kuwa hivo ni baadhi ya vipengele vilivyopo katika mfumo wa SPIN-ED.

“Niseme tu kwamba vina umuhimu mkubwa sana katika uchakataji wa taarifa za kitaaluma za wanafunzi kwani huwasaidia walimu na wadau mbalimbali wa elimu kufanya maamuzi mbalimbali na hatimae kuongeza ufanisi katika mbinu za ufundishaji na ujifunzaji".

Aidha amesema sababu kubwa ya yeye kufanya ugunduzi wa mfumo huu wa SPIN-ED ni kutokana na changamoto alizoziona wakati akiwa mwalimu wa kujitolea katika moja ya shule hapa nchini, hususan katika uandaaji wa ripoti za maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi.

wakati mwingine huchukua muda mrefu kwa Walimu kuandaa na hata wakati mwingine Walimu kukosa hamasa ya kutoa majaribio ya mitihani ya Mara kwa Mara ya kuwapima wanafunzi wakihofia kuchukua muda kwa uandaaji wa ripoti na Maendeleo yao.

Mfumo huu wa SPIN-ED ameugundua mwaka 2021 na kuanza kufanya kazi mwaka huohuo ambapo mpaka kufika sasa zipo shule 3 zinazotumia mfumo huu.

SERIKALI KUENDELEA KUDHIBITI DAWA ZA KULEVYA NA RUSHWA



NA WELLU MTAKI , DODOMA.

SERIKALI inaendelea kukabiliana na masuala ya  biashara ya dawa za kulevya na rushwa nchini  ili kuhakikisha wanajenga taifa lililo imara kwa kutoa Elimu kuanzia shule za msingi mpaka vyuo vikuu.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya  Aretas Lyimo Jijini Dodoma   wakati  akifunga mafunzo kuhusu mkakati  wa habari , Elimu , mawasiliano  na programu ya TAKUKURU rafiki pamoja na  tatizo za dawa za kulevya , mapambano dhidi ya rushwa kwa maafisa wanaohusika na uelimishaji umma na mawasiliano.    

Lyimo amesema kupitia mafunzo waliopewa maafisa wanaohusika na uelimishaji umma na mawasiliano yatasaidia kuleta matokeo chanya ya  kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya na Rushwa kwani ni vitu vinavyofanana.

“Naamini kupitia muunganiko wetu na klabu ambazo tayari tumeshanzianzisha huko mashuleni itasaidia kuwafikia kwa uharaka zaidi watu katika ngazi za mitaa hadi huko kwenye Halmashauri  wanafunzi wengi wanatokea kwani huko,”amesema. Lyimo

Amesema matunda ya ushirikiano kati ya TAKUKURU na taasisi ya kupambana dawa za kulevya tayari yameanza kuonekana kwani vitu hivyo vimekuwa vikiisumbua serikali katika kuhakikisha wote wanao husika wanatiwa mbaroni na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Nitoe wito kwa wadau kuwa nyenzo pekee ya kuepusha watu kujiingiza kwenye Rushwa na dawa za kulevya ni kutoa elimu hata tukiendelea kukamata kwa namna gani lazima tuhakikishe tunatoa elimu pamoja na kushirikiana na vyombo vya habari ili watusaidie kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja,”amesema.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu TAKUKURU Bi. Neema Mwakalile amesema kilichotokea kwenye mafunzo hayo kinadhihirisha ushirikiano  uliopo kati ya TAKUKURU na Mamlaka ya Kupambana na dawa za Kulevya ni mkubwa kwani vitu hivyo vinafanana na mapambano yanapaswa kuimarishwa zaidi.

Mwakalile amesema kuwa washiriki wamejifunza juu ya tatizo la dawa za kulevya, sababu za matumizi ya dawa hizo pamoja na kutambua dawa tiba ambapo vijana wengi wameonekana kujiingizia kwa kiasi kikubwa katika janga hilo huku akiongeza kuwa elimu waliyo wapatia washiriki katika mkutano huo itaenda kuumarisha zaidi mapambano na hatimaye kufikia hazma ya Serikali.

“Washiriki walipitishwa kwenye mkakati wa kupambana na Rushwa ili kuelewa zaidi na namna ya kwenda kuelimisha wanafunzi pia mafunzo haya yatasaidia jamii kuichukia Rushwa na kuepukana na Dawa za kulevya,”amesema.Mwakalile

Pia ameongeza kuwa katika mambo mengi waliyowafundisha wataenda kutoa elimu hasa kwa wanafunzi kwani swala hilo limekuwa mtambuka. 

 “Ni lazima kuanza kuwajenga wanafunzi wa shule msingi na sekondari kwani wao ndio watakuwa msingi mzuri kwenda kupinga na kukataa dawa za kulevya pia  Rushwa na dawa za kulevya vina madhara makubwa kwenye nyanja zote elimu na uchumi,”ameongeza.

Taasisi ya kupambana na Rushwa na TAKUKURU waliingia makubaliano 20/5 2023 kwaajili ya kutoa elimu kuhusu rushwa na dawa za kulevya.

Thursday, February 22, 2024

CHESTMOKA MABINGWA KIBAHA VIJANA CUP

TIMU ya soka ya Chestmoka imetwaa ubingwa wa Kibaha Vijana Cup kwa kuifunga Muharakani kwa penati 6-5 na kujinyakulia kiasi cha shilingi milioni 1.

Mchezo huo wa fainali ulichezwa kwenye uwanja wa Mwendapole Wilayani Kibaha Muharakani walijinyakulia kiasi cha shilingi 500,000 na washindi watatu Tp Pwani wakijinyakulia seti ya jezi.

Mgeni rasmi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mussa Ndomba ambaye alimwakilisha mdhamini wa ligi hiyo Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka amesema michezo ni afya na ajira.

Ndomba amesema kuwa Halmashauri itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya michezo ili vijana waweze kucheza na kujipatia ajira.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani COREFA Mohamed Lacha amesema kuwa malengo ni kutaka soka lichezwe ndani ya mkoa huo.

Lacha amesema ili soka likue ni kuwa na michezo mingi ili kuibua vipaji vingi na kuviendeleza ili kuwa na timu nzuri.

Naye meneja wa mashindano hayo Walter Mwemezi amesema jumla ya timu 16 zilichuana kwenye mashindano hayo.

Mwemezi amesema kuwa matarajio yao kwa mwakani ni kushirikisha timu nyingi ili mashindano hayo yawe na msisimko zaidi.

Kwa upande wake mwakilishi wa Koka Said Mbecha amesema kuwa Mbunge ameahidi kuendelea kusaidia michezo ili vijana wengi wapate fursa mbalimbali zilizopo kwenye michezo.